Jumapili, 21 Septemba 2025

Hospitali ya Shifaa ‘yawaita’ wenye NHIF kupata huduma

 - Yasema haibagui ipo kwa ajili ya Watanzania wote

- Majengo yasiwaogopeshe

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Uongozi wa Hospitali ya Shifaa ya Dar es Salaam umewashauri wananchi wenye changamoto za kiafya na maradhi mbalimbali walio na bima ya afya ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), kufika hospitalini hapo ili wapatiwe huduma na kuacha fikra kwamba hospitali hiyo haipokei wagonjwa wanaotumia bima ya NHIF.

Sehemu ya Jengo la Hospitali ya Shifaa iliyopo Kinondoni, Dar es Salaam linavyoonekana.

Akizungumza ofisini kwake jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali hiyo, Bashir Haroun ametoa ushauri huo akieleza kuwa kumekuwepo dhana potofu kwamba Hospitali ya Shifaa haipokei wagonjwa wanaotumia Bima ya Afya ya NHIF, jambo ambalo amesema halina ukweli.

Hospitali hiyo ya kisasa ya Shirika la Shifaa Pan African Hospitals Limited chini ya Kundi la Makampuni ya Oil Com, iliyoanza kazi miaka miwili iliyopita, ipo maeneo ya Kinondoni, Barabara ya Msese, ikiwa na kauli mbiu ya kuboresha huduma za afya nchini, uwekezaji wake ukigharimu Dola za Marekani milioni 60, takriban Shilingi bilioni 162.

“Hospitali ya Shifaa inatoa huduma kwa wote bila kubagua hali ya maisha, tunapokea na kuwatibu pia wananchi wanaotumia bima za kampuni mbalimbali hata Bima ya Afya ya NHIF, tofauti na mtazamo wa baadhi ya watu, wenye lengo la kuwakosesha wananchi huduma bora na za kisasa za hospitali yetu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Shifaa, Bashir Haroon

Hata wale wanaosita kuja kwa kuogopeshwa na mazingira bora ya jengo la hospitali, wasiogope kuja hilo ni moja ya lengo letu kutoa huduma bora za afya katika mazingira bora,” amesema Bashir.

Ameongeza: “Hospitali ya Shifaa imejengwa kuunga mkono juhudi za Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan za kutoa huduma bora za afya kwa wananchi wote bila ubaguzi.

Hapa tunapokea wagonjwa wenye bima ya afya ikiwamo Bima ya Afya ya NHIF, waje tu tutawapa hudumia bora za kisasa bila kikwazo, pia tunapokea na kuwahudumia wanaolipa pesa taslimu.”

Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo Mtendaji, ujenzi wa Shifaa Hospitali umezingatia mambo matatu muhimu ambayo ni pamoja na miundombinu bora ya kisasa, vifaa tiba bora na vya kisasa ikiwamo vipimo na watoa huduma wenye viwango bora vya taaluma.

Moja ya maeneo ya kuhudumia wananchi katika Hospitali ya Shifaa, Dar es Salaam.

Bashir amesisitiza; “Tupo kwa ajili ya Watanzania, tunaunga mkono juhudi za Serikali kutoa huduma bora za afya. Hapa hatubagui bima ya afya, pia tuna kitengo cha ustawi wa jamii. Muhimu Watanzania wapate huduma bora za afya.”

Alhamisi, 18 Septemba 2025

NHC YAKABIDHI MSAADA KWA WATU WENYE ULEMAVU UBUNGO

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), kupitia kwa Ofisa wake Mkuu wa Habari, Yahya Charahani, limekabidhi msaada wa vifaa vya kusaidia watu wenye ulemavu kwa Chama cha Watu Wenye Ulemavu katika Manispaa ya Ubungo, jijini Dar es Salaam.

Ofisa Mkuu wa Habari wa Shirika la Nyumba Tanzania (NHC), Yahya Charahani, akikabidhi msaada wa vifaa vya kusaidia watu wenye ulemavu kwa Chama cha Watu Wenye Ulemavu katika Manispaa ya Ubungo, jijini Dar es Salaam, leo Septemba 18,2025.

Msaada huo umejumuisha magongo ya kutembelea (crutches), baiskeli za walemavu, na vifaa vingine vya kusaidia watu wenye uhitaji maalum kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za kijamii na kiuchumi.

Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano, Charahani alisema:"Tumefika hapa leo kwa niaba ya Shirika la Nyumba la Taifa kuonyesha mshikamano wetu na watu wenye ulemavu. Tunatambua changamoto wanazopitia, na msaada huu ni sehemu ndogo ya mchango wetu kwa jamii ambayo sisi pia ni sehemu yake."

Ameongeza kuwa shirika hilo limeweka sera za kijamii zinazolenga kusaidia makundi maalum katika nyanja za elimu, majanga, na ustawi wa watu wenye ulemavu, akisisitiza kuwa hakuna mtu anayejua lini maisha yanaweza kubadilika.

 "Sisi sote ni walemavu watarajiwa. Leo hii ni wao, kesho inaweza kuwa mimi au wewe. Tunaposaidia, hatufanyi hivyo kwa sababu tuna ziada, bali kwa sababu tunatambua utu wa kila mmoja," amesisitiza Charahani.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Watu Wenye Ulemavu Wilaya ya Ubungo, Athmani Hassani Sembe, ameishukuru NHC kwa niaba ya wanachama wake akieleza:

 "Tunashukuru sana kwa moyo wa upendo mlioonyesha. Wanachama wetu watafurahia sana msaada huu, hasa wale ambao walikuwa hawana vifaa vya kutembelea. Huu ni msaada unaogusa maisha moja kwa moja."

Naye Naibu Katibu wa chama hicho, Saidi Mbogo, ameeleza kuwa msaada huo sio tu umeleta matumaini, bali pia umeonyesha kuwa bado kuna mashirika yanayowajali watu wenye ulemavu:

 "Ni mashirika machache sana yenye moyo kama huu. Tunawashukuru sana NHC. Vifaa hivi ni kama miguu ya tatu kwa wengi wetu, vinaongeza uwezo wa kujitegemea na kushiriki kikamilifu katika jamii."

Maofisa wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), wakishusha vifaa mbalimbali kwa ajili ya kutoa msaada kwa watu wenye ulemavu wilayani Ubungo, Dar es Salaam, Septemba 18,2025.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na wanachama wa chama hicho, maofisa wa NHC na wanahabari, huku ikihitimishwa kwa maombi na pongezi kwa mshikamano ulioonyeshwa baina ya sekta ya umma na jamii.


MAWAKILI SERIKALI WATAKIWA KUSHIKA, KUZINGATIA SHERIA, KANUNI ZA HIFADHI YA JAMII

 Mwandishi Wetu,daimatznews@gmail.com

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza S. Johari amewataka Mawakili wa Serikali kuhakikisha kuwa Sheria na Kanuni za Hifadhi ya Jamii zinalinda na kusimamia haki na maslahi ya Wanachama wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii nchini.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari akizungumza wakati wa kufungua mafunzo kwa mawakili wa Serikali yaliyoandaliwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa PSSSF mjini Kibaha, Pwani leo Septemba 18,2025.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kuhusu Hifadhi ya Jamii kwa Mawakili wa Serikali yaliyoandaliwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa PSSSF yanayofanyika Septemba 18 hadi19 Setpemba, 2025 katika Chuo cha Uongozi Mwalimu Nyerere Kibaha, mkoani Pwani.

Johari amesema kuwa mafunzo hayo yatawanufaisha Mawakili wa Serikali kwa kuongeza ujuzi kwenye masuala mbalimbali hasa sheria zinazohusiana na Hifadhi ya Jamii ikiwemo , Sheria ya Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma [Sura ya 371], Sheria ya Mikataba [Sura ya 345], Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini [Sura ya 366], pamoja na Usimamizi wa Fedha na Uwekezaji.

“Ni matarajio yangu kuwa mafunzo haya yatajikita katika maeneo Muhimu ya Kisheria na Kiutawala ikiwemo Muundo wa kisheria wa PSSSF na majukumu yake ya msingi, Haki na Wajibu wa wanachama, wastaafu na wategemezi wao,” amesema Mwanasheria Mkuu huyo wa Serikali

Ameeleza kuwa  kupitia mafunzo hayo Mawakili wa Serikali wataweza kuwa na uelewa mpana wa kushauri na kushughulikia masuala ya kisheria yanayohusu Mfuko wa PSSSF, kupunguza migogoro inayoweza kupelekea kesi Mahakamani kwa kutumia mbinu za usuluhishi na mazungumzo.

Kwa mujibu wa Johari wanasheria na mawakili hao wataweza kuweka misingi thabiti ya kisheria katika utekelezaji wa shughuli za kila siku za Mfuko na kujenga uhusiano wa karibu kati ya PSSSF na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa manufaa ya Taifa.

Wanasheria wa Serikali wakifuatilia mafunzo yaliyoandaliwa na PSSSF, Kibaha mkoani Pwani leo Septemba 18,2025.

Ametoa wito kwa Mawakili wa Serikali wanaoshiriki mafunzo hayo kuwa na ari  na kuhakikisha kuwa maarifa watakayoyapata wanayaweka katika Vitendo na kuhakikisha kuwa PSSSF inaendeshwa kwa ufanisi na kwa mujibu wa Sheria na Kanuni.

Jumatano, 17 Septemba 2025

Ada Cottrell yawasaidia watoto wenye mahitaji Zanzibar

 Mwandishi Wetu, Zanzibar

Taasisi ya Ada Cottrell Foundation kwa kushirikiana na Taasisi ya Labayka Development Foundation (LDF), imetoa msaada kwa watoto wanaoishi kwenye mazingila magumu ili kuwawezesha kujikimu kwa mahitaji yao.

Baadhi ya watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu eneo la Nungwi Zanzibar wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kukabidhiwa msaada kutoka taasisi ya Ada Cottrell Foundation ya Marekani kwa kushirikiana na Taasisi ya Labayka Development Foundation (LDF) ikiwa ni sehemu ya kumuenzi marehemu Robert Cottrell.

Msaada huo umetolewa kwa Watoto hao walio katika Kata ya Nungwi, Kijiji cha Nungwi, Wilaya ya Kaskazini A na Mkoa wa Kaskazini Unguja, visiwani  Zanzibar.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukabidhi msaada huo, Mkurungezi Muwakilishi wa taasisi ya Ada Cottrell Foundation, Shedrack Gabriel Albert amesema hatua hiyo ni mwendelezo wa utaratibu unaofanywa kila mwaka na taasisi hiyo, ikiwa ni kumbukizi ya marehemu Robert Cottrell, raia ya Marekani kila ifikapo Agosti kwa kuwa ndio mwezi aliofariki.

Robart alikuwa Marekani na alifariki dunia Agosti 2018 kwa ugonjwa wa saratani, ameacha mke, Joyce  Cottrell na mtoto wa kike, Ada Cottrell ambaye ndiye msimamizi wa taasisi ya Ada Cottrell Foundation ya Marekani na tawi lake kwa sasa lipo nchini Tanzania.

Hata hivyo, Shedrack amesema pamoja na msaada ukliotolewa na taasisi yake, visiwa vya Unguja bado vinakabiliwa na changamoto ya watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu, hivyo bado wanahitaji msaada zaidi.

Akizungumza  baada ya Watoto hao kukabidhiwa msaada huo, mwenyeji wa Taasisi ya Ada Cottrell, Khamis Juma Mtwana kutoka taasisi   ya Labayka Development Foundation(LDF), iliyopo Nungwi ameahidi kushirikiana vyema kuhakikisha wanapunguza tatizo la watoto wenye uhitaji mjini humo.

Watoto wanaoishi katika mazingira magumi Nungwi mjini Zanzibar, wakiwa katika pia ya pamoja na watendaji wa taasisi za Ada Cottrell Foundation ya Marekani kwa kushirikiana na Taasisi ya Labayka Development Foundation (LDF) ambao walitoa msaada wa vitu mbalimbali kwa watoto hao.

Pamoja na ugawaji wa mahitaji hayo pia ilifanyika dua maalum ya kumuombea Robart Cottrell ikiwa sehemu ya kumbukumbu yake, iliyoongozwa na Sheikh Apite Haji Ali, Jinala.

 

 

 

  

Jumanne, 16 Septemba 2025

Madaktari Bingwa wapiga kambi Hospitali ya Kitengule kuhudumia wananchi


 

BENJAMIN NGAYIWA AAHIDI KUTOKOMEZA MIGOGORO YA ARDHI

Mwandishi Wetu, Kahama

Mgombea Ubunge wa Jimbo la Kahama Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Benjamin Ngayiwa, ameweka wazi dhamira yake ya kumaliza kabisa changamoto ya migogoro ya ardhi inayowakumba wakazi wa jimbo hilo kwa muda mrefu.

 Akiwa kwenye uzinduzi wa kampeni za CCM ngazi ya jimbo, uliofanyika katika viwanja vya Phantom, Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, mkoani Shinyanga, Ngayiwa amewahakikishia wananchi kuwa ardhi haitakuwa chanzo cha migogoro tena endapo atapewa ridhaa ya kuwa Mbunge wao.

Katika hotuba yake, Ngayiwa alisisitiza kuwa atashirikiana kwa karibu na Madiwani pamoja na Wenyeviti wa Mitaa ili kuhakikisha kuwa migogoro yote ya ardhi inatatuliwa kwa haki na kwa wakati.

Aidha, Ngayiwa ametoa wito maalum kwa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa kuacha mara moja tabia ya kupima na kuwauzia watu zaidi ya mmoja kiwanja kimoja. 

Amesema kuwa utaratibu huo siyo tu unawanyima haki wananchi, bali pia umekuwa chanzo kikuu cha migogoro isiyokwisha ya ardhi katika maeneo mengi ya Kahama.

Katika kuhakikisha wananchi wanamwelewa vyema, mgombea wao, viongozi mbalimbali wa CCM walijitokeza kumpigia debe. Emanuel Cherehani, Mgombea Ubunge wa Jimbo la Ushetu, akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa, amesema kuwa Ngayiwa ni chaguo sahihi kwa wana Kahama.

 Amesema kuwa ana imani kubwa kuwa Ngayiwa atakuwa kiungo muhimu kati ya wananchi na Serikali katika kuhakikisha ndoto za wananchi wa Jimbo hilo zinatimia.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa, amewaomba wananchi wa Kahama kuwapa kura zote wagombea wa CCM – kuanzia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Benjamin Ngayiwa, hadi Madiwani – ili kuhakikisha kuwa maendeleo ya kweli yanapatikana kwa kasi na kwa usawa katika Jimbo la Kahama.

WAZAZI WAASWA KUTOACHA MALEZI KWA WALIMU PEKEE

Mwandishi Wetu, Kahama

Wazazi wametakiwa kuendelea kushiriki kikamilifu katika kufuatilia maendeleo ya watoto wao kielimu na kimaadili, badala ya jukumu hilo kuwaachia walimu  pekee.
Wito huo ulitolewa na Mthibiti Ubora wa Shule wilayani Kahama, Athuman Abeid Al - Jabriy, alipohutubia mahafali ya darasa la saba katika Shule ya Msingi Greenstar, yaliyofanyika mwishoni mwa wiki.
Abeid amesema kuwa dunia ya sasa inakabiliwa na mmomonyoko mkubwa wa maadili, na hivyo ni muhimu kwa wazazi kushirikiana kwa karibu na walimu katika malezi na maendeleo ya watoto.
“Mtoto anapokabidhiwa shule kuanzia awali hadi darasa la saba, ni kipindi cha zaidi ya miaka minane. Kama mzazi hutafuatilia maendeleo yake, na walimu wakipoteza mwelekeo, mzigo wa marekebisho utakuwa juu yako. Tushirikiane katika malezi kwa manufaa ya baadaye ya watoto wetu,” amesema Abeid.
Aidha, amewasihi wahitimu wa darasa la saba kutambua kuwa mahafali si mwisho wa safari ya elimu, bali ni mwanzo wa hatua nyingine muhimu. Alisisitiza kuwa mtihani wa taifa unaokuja unapaswa kupewa kipaumbele cha hali ya juu.
Katika mahafali hayo, Mkurugenzi wa Taasisi wa Shule za Greenstar,  Daniel Nchenga alieleza kuwa taasisi hiyo imefanikiwa kuanzisha shule mbili za sekondari; moja ya wavulana na nyingine ya wasichana, ikiwa ni sehemu ya kupanua wigo wa elimu kwa wanafunzi wanaohitimu shule ya msingi.
Nchenga ametumia fursa hiyo kutangaza mpango wa kubadilisha jina la Shule ya Sekondari ya Sister Irene kuwa Greenstar Boys, ambapo aliiomba Ofisi ya Elimu kushirikiana katika kukamilisha mchakato huo kabla ya Januari mwakani.
 “Naomba wazazi muendelee kuwahamasisha watoto wenu warudi kujiunga na sekondari zetu. Tunataka jina jipya litambulike mapema ili maandalizi ya kitaaluma yaanze kwa wakati,” amesema Nchenga.
Kwa upande wao, baadhi ya wazazi walioshiriki mahafali hayo wametoa pongezi kwa walimu wa shule hiyo kwa kazi kubwa ya kusimamia taaluma na maadili ya watoto wao.
 “Tumeona watoto wetu wakibadilika na kukua kitaaluma na kimaadili. Tunawashukuru walimu kwa juhudi zao kubwa,” Mama Sophia amesema mzazi mmoja kwa niaba ya wenzake.

Mahafali hayo yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa elimu, walimu, wazazi na wanafunzi, huku yakipambwa na burudani mbalimbali kutoka kwa wanafunzi wa shule hiyo.

Jumapili, 7 Septemba 2025

Salum Mwalimu aja na kuwekezesha vijana kuanzisha kampuni za utalii, biashara

 Mgombea Urais kupitia Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA), Salum Mwalimu, ameahidi kuanzisha mfuko maalumu wa kuwawezesha vijana kuwekeza katika sekta ya utalii, iwapo atachaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu, utakaofanyika Oktoba 29,2025.

Ametoa ahadi hiyo alipokuwa akiiwahutubia wananchi wa Mkoa wa Arusha, ambapo amesema mpango huo utahusisha utoaji wa magari ya kuanzia, mitaji midogo na mafunzo maalum kwa vijana wenye ndoto ya kuingia kwenye biashara ya utalii.

"Mpango huo ni sehemu ya ajenda ya CHAUMMA ya kupanua wigo wa ajira kwa vijana," amesema Mwalimu.

Mgombea urais huyo wa CHAUMMA ameitaka jamii kuwa tayari kuunga mkono juhudi hizo kwa kushiriki kikamilifu kwenye mabadiliko ya kiuchumi kupitia sekta zenye fursa.

Dk. Samia: Tutawaanzishia wakulima vituo kukodi matrekta

-Asema zana zingine pia zitakodishwa

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Mgombea Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Samia Suluhu Hassan amesema akichaguliwa kuiongoza Tanzania katika uchaguzi ujao Oktoba 29,2025 ataanzisha vituo vya ukodishaji matrekta na zana zingine za kilimo kwa wakulima nchini.

Akizungumza katika Uwanja wa Samora ulipofanyika mkutano wa Kampeni za CCM leo Septemba 7 mkoani Iringa, Rais Samia pichani juu, amesema matrekta na zana hizo za kilimo  zitakuwa zikikodishwa kwa nusu ya bei ya matrekta ya watu binafsi.

"Endapo Wananchi watanipa ridhaa ya kuongoza tena nchi kwa kunichagua katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025, Serikali yangu itaendelea kutoa ruzuku ya mbolea na pembejeo kwa wakulima nchini," amesema mgombea.

Kwa mujibu wa mgombea urais huyo kitendo cha Serikali kutoa ruzuku katika mbolea kumeleta tija ya uzalishaji wa mazao na hasa mahindi, yaliyoifanya Tanzania kushika nafasi ya pili kwa uzalishaji Afrika kutokana na kuzalisha zaidi ya tani milioni 10 .

Ameongeza kuwa akipewa ridhaa hiyo kuiongoza Tanzania ataendelea kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo ya miundombinu ya barabara, maji, elimu na afya.

Katika mkutano huo mkubwa uliohitimisha kampeni zake mkoani Iringa, mbali ya kujinadi, Rais Samia pia amewanadi na kuwaombea kura wagombea ubunge na udiwani wa CCM.

‎Akiwa mkoani humo, Rais Samia jana alijinadi eneo la Nyororo na Mafinga wilayani Mufindi pamoja na Kalenga Wilaya ya Iringa Vijijini

Tukio la kihistoria la Kupatwa kwa Mwezi usiku huu Septemba 7, 2025

 Picha tofauti zatukio la Kupatwa kwa Mwezi kama lilivyonaswa na kamera ya daimatznews blogspot usiku huu;









Kairuki: Mkinichagua Kibamba itabamba

 Mgombea Ubunge Jimbo la Kibamba kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM), Angela Kairuki  (Pichani chini kushoto), amezindua kampeni za kuwania kiti hicho leo Septemba 7,2025, akisema kuwa iwapo wananchi wa jimbo hilo watamchagua kuwa mbunge wao katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29,2025 basi 'Kibamba Itabamba.'

Kairuki ametoa kauli hiyo kwenye mkutano wake wa kwanza wa kampeni eneo la Mbezi Stendi jimboni humo mkoani Dar es Salaam ambapo amesema anazijua changamoto za jimbo hilo na matarajio yao, kwa kuwa yeye ni 'mtoto' wa Kibamba na kuwaahidi wananchi kwamba atawatatulia changamoto zote zilizopo jimboni humo.

"...Mimi ni mtoto wa Kibamba, nimekulia Kibamba, nimeyaishi maisha ya Kibamba, nimeyaishi mafanikio ya Kibamba, lakini pia changamoto za Kibamba, najua matamanio, nayajua pia matamanio ya wana Kiamba.

Niwahakikishie, nimedhamiria kuunganisha nguvu zangu na zenu, ili kupata majawabu ya changamoto za Kibamba. Niwahakikishie, endapo mtamchagua Dk. Samia Suluhu Hassan kwa nafasi ya urais,  endapo mtanichagua mimi kuwa mbunge wenu na madiwani wote wa CCM, Kibamba itabamba, itakuwa haina mbambamba" amesema Kairuki na kuongeza: 

"Mimi ni mtoto wenu, ... mtumishi wenu na mgombea wenu wa nafasi ya ubunge kwa tiketi CCM."


Jumatano, 3 Septemba 2025

NUKUU TATU ZA MGOMBEA URAIS CHAUMMA SALUM MWALIM LEO HIZI HAPA

                 NUKUU TATU ZA MGOMBEA URAIS CHAUMA KOROGWE 03/09/2025

1."Vijana wenzangu jengeni imani kwangu ili tutatue kero zetu, uwezo ninao na sifa ninazo za kuzalisha ajira, wanawake mtajifungua kwa stara na siyo kubeba vifaa kama mnakwenda kuanza shule ya msingi" 

2. "Msikubali kufanywa mazwazwa, wanaokufa ni watoto na wazazi wenu kwa sababu mmeikubatia CCM, uamuzi wa kuikataa  wakwenu ili kukichagua chama kingine muonje radha yake" Mgombea Salum Mwalimu - CHAUMMA Korogwe Vijijini.

3." Tunatakiwa kuwa na kilimo cha utashi ili kulima.mazao yote ya biashara katika mikoa yote ili kuiondoa Tanzania katika umaskini, tuchagueni  CHAUMMA ili neema aliyotujaalia tuitumie ya kuwekeza katika kilimo hata tukajenga kiwanda kidogo cha juisi ili watu wapate ajira" Mgombea wa CHAUMMA Salum Mwaiim Jimbo la Muheza.



TCU yatoa siku 18 udahili awamu ya pili Vyuo Vikuu

 -Udahili kuongezeka

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), imetangaza kufunguliwa kwa Awamu ya pili ya udahili wa Shahada ya Kwanza kwa Mwaka wa Masomo 2025/2026, utakaofanyika kwa siku 18 ukianzia leo Septemba 3 hadi 21, 2025.

Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa, akizungumza na wanahabari leo mkoani Dar es Salaam, 

Akizungumza na wanahabari leo mkoani Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa, amewataka waombaji walioshindwa kutuma maombi ya udahili au kukosa  nafasi katika awamu ya kwanza ya udahili kwa sababu mbalimbali kutumia fursa hiyo kuomba udahili.

Profesa Kihampa, amesema kwamba kufunguliwa kwa dirisha hilo ni hatua iliyofuata  kukamilika kwa Awamu ya Kwanza ya Udahili wa Shahada ya Kwanza katika Taasisi za Elimu ya Juu nchini kwa mwaka wa masomo 2025/2026.

"Majina ya waliodahiliwa katika awamu ya kwanza yatatangazwa na vyuo husika kwa mujibu wa utaratibu,"amesema Profesa Kihampa akiongeza:.

"TCU inaelekeza Vyuo vya Elimu ya Juu nchini kutangaza programu ambazo bado zina nafasi na waombaji udahili na vyuo wanapaswa kuzingatia utaratibu wa udahili wa Awamu ya Pili, kama inavyooneshwa kwenye Kalenda ya Udahili iliyoko katika tovuti ya TCU – www.tcu.go.tz."

Kuhusu kukamilika kwa Awamu ya Kwanza ya Udahili, Katibu Mtendaji huyo wa TCU amesema jumla ya waombaji 146,879 walituma maombi ya kujiunga katika vyuo 88 vilivyoidhinishwa kudahili wanafunzi wa Shahada ya Kwanza.

Amefafanua kwamba jumla ya programu 894 za masomo zimeruhusiwa kudahili kwa mwaka wa masomo 2025/2026, ikilinganishwa na programu 856 mwaka 2024/2025, ambalo ni ongezeko la programu 38 za masomo.

Profesa Kihampa amesema kwa upande wa nafasi za udahili, mwaka huu kuna jumla ya nafasi 205,652 zikilinganishwa na nafasi 198,986 mwaka uliopita. 

“Hapo kuna ongezeko la nafasi 6,666 ambalo ni sawa na asilimia 3.3 katika programu za Shahada ya Kwanza. Lakini katika Awamu ya Kwanza ya Udahili, jumla ya waombaji 116,596 sawa na asilimia 79.4 ya waombaji wote walioomba udahili wamedahiliwa kwenye vyuo walivyoomba. Katika Awamu ya Pili ya Udahili, idadi ya waombaji na watakaodahiliwa inatarajiwa kuongezeka," anasema Profesa Kihampa.

Amebainisha kwamba waombaji waliodahiliwa katika chuo zaidi ya kimoja wanapaswa kuthibitisha udahili wao katika chuo kimojawapo kuanzia leo Septemba 3, hadi Septemba 21, 2025 na kwamba uthibitisho huo unafanyika kwa kutumia namba maalum ya siri iliyotumwa kwa ujumbe mfupi kupitia namba zao za simu, au barua pepe walizotumia wakati wa kuomba udahili.

“Wale ambao hawatapata  ujumbe huo kwa wakati, wanashauriwa kuingia kwenye mifumo ya udahili ya vyuo walivyodahiliwa na kuomba kutumiwa ujumbe mfupi wenye namba maalum ya siri ili kuithibitisha katika chuo husika” amehitimisha.