NHC YAKABIDHI MSAADA KWA WATU WENYE ULEMAVU UBUNGO
Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), kupitia kwa Ofisa wake Mkuu wa Habari, Yahya Charahani, limekabidhi msaada wa vifaa vya kusaidia watu wenye ulemavu kwa Chama cha Watu Wenye Ulemavu katika Manispaa ya Ubungo, jijini Dar es Salaam.
Msaada huo umejumuisha magongo ya kutembelea (crutches), baiskeli za walemavu, na vifaa vingine vya kusaidia watu wenye uhitaji maalum kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za kijamii na kiuchumi.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano, Charahani alisema:"Tumefika hapa leo kwa niaba ya Shirika la Nyumba la Taifa kuonyesha mshikamano wetu na watu wenye ulemavu. Tunatambua changamoto wanazopitia, na msaada huu ni sehemu ndogo ya mchango wetu kwa jamii ambayo sisi pia ni sehemu yake."
Ameongeza kuwa shirika hilo limeweka sera za kijamii zinazolenga kusaidia makundi maalum katika nyanja za elimu, majanga, na ustawi wa watu wenye ulemavu, akisisitiza kuwa hakuna mtu anayejua lini maisha yanaweza kubadilika.
"Sisi sote ni walemavu watarajiwa. Leo hii ni wao, kesho inaweza kuwa mimi au wewe. Tunaposaidia, hatufanyi hivyo kwa sababu tuna ziada, bali kwa sababu tunatambua utu wa kila mmoja," amesisitiza Charahani.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Watu Wenye Ulemavu Wilaya ya Ubungo, Athmani Hassani Sembe, ameishukuru NHC kwa niaba ya wanachama wake akieleza:
"Tunashukuru sana kwa moyo wa upendo mlioonyesha. Wanachama wetu watafurahia sana msaada huu, hasa wale ambao walikuwa hawana vifaa vya kutembelea. Huu ni msaada unaogusa maisha moja kwa moja."
Naye Naibu Katibu wa chama hicho, Saidi Mbogo, ameeleza kuwa msaada huo sio tu umeleta matumaini, bali pia umeonyesha kuwa bado kuna mashirika yanayowajali watu wenye ulemavu:
"Ni mashirika machache sana yenye moyo kama huu. Tunawashukuru sana NHC. Vifaa hivi ni kama miguu ya tatu kwa wengi wetu, vinaongeza uwezo wa kujitegemea na kushiriki kikamilifu katika jamii."Maofisa wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), wakishusha vifaa mbalimbali kwa ajili ya kutoa msaada kwa watu wenye ulemavu wilayani Ubungo, Dar es Salaam, Septemba 18,2025.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na wanachama wa chama hicho, maofisa wa NHC na wanahabari, huku ikihitimishwa kwa maombi na pongezi kwa mshikamano ulioonyeshwa baina ya sekta ya umma na jamii.
Maoni
Chapisha Maoni