-Yanufaisha kampuni kubwa
-Sekta binafsi yaongoza
Exuperius Kachenje, daimatznews@gmail.com
Benki ya Maendeleo (TIB) imefanikiwa kutekeleza majukumu yake manne ya msingi (mafiga), ambapo sasa imefikia uwekezaji wa shilingi bilioni 980.
Akizungumza katika mkutano wake na wahahriri wa vyombo vya Habari chini ya usimamizi wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, Oktoba 16, 2023, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TIB, Lilian Mbassy amesema benki hiyo imetekeleza malengo hayo kwa ukamilifu hata kufikia uwekezaji huo wa shilingi bilioni 980.
Utekelezaji kikamilifu wa majukumu hayo sasa umeweza kuipaisha benki hiyo siyo tu kufikia uwekezaji wa shilingi bilioni 980, bali sekta binafsi kuongoza kufaidika.
Katika mkutano huo, pamoja na mambo mengine, Mbassy ametaja 'mafiga' manne iliyopewa TIB kisheria kuwa ni pamoja na kuwezesha upatikanaji wa mitaji ya muda mrefu na wa kati kwa ajili ya maendeleo ya kiuchumi, kutoa msaada wa kiufundi na ushauri kwa ajili ya kuwezesha maendeleo ya viwanda.
Mengine ni kusimamia mfuko maalum kama itakavyohitajiwa na Serikali pamoja na kuendeesha shughuli nyingine za kimaendeleo kadiri inavyoonekana zinahitajiwa, ili kuwezesha benki kutimiza malengo ya kuanzishwa kwake.
“Mpaka kufikia Septemba 2023 Benki imewekeza jumla ya Sh bilioni 980, asilimia 93 ya miradi yetu ni ya sekta binafsi. Asilimia 93 ya miradi iliyofadhiliwa na TIB yote ni ya Sekta binafsi,” amesema Mbassy.
Kwa mujibu wa Mbassy, kati ya uwekezaji huo, asilimia 7 tu ya miradi ndio imefadhiliwa kwa Sekta ya Umma na asilimia 80 ikiwa miradi ya zaidi ya miaka mitano.
Mbassy ameyataja baadhi ya mashirika yaliyonufaika na uwekezaji huo kuwa ni pamoja na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), kupitia uwekezaji kwenye miradi ya ujenzi wa makazi, Kampuni ya Huduma za Meli kupitia uwekezaji miradi ya ukarabati wa meli nchini, uwekezaji kwenye upanuzi wa viwanda vya sukari.
Umo pia upanuzi katika mradi wa upanuzi wa Kiwanda cha Kuzalisha Mambomba cha (PIPES Industries Ltd) na upanuzi wa bandari kavu.
Mengine ni Serikali za Mitaa kupitia uwekezaji katika sekjta ya miundombinu na kwamba TIB itazingatia miradi yenye kuwiana na Mipango ya Serikali katika kuuda mfumo wa msaada na uratibu wa LGAs.
Mkurugenzi huyo amesema kwamba utekelezaji wa TIB katika uwekezaji huo wa shilingi bilioni 980, unazingatia Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025, Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa miaka mitano, Mpangio Mkuu wa Uendelezaji Sekta ya Fedha na Vipaumbele vya Serikali.
Mbassy amebainisha kuwa TIB pia inatoa huduma maalum za ushauri wa kitaalam katika miradi ya kimkakati na kutaja baadi ya mashirika yaliyonufaika na mhuduma hiyo kuwa ni Pamoja na Shirika la Ndege Tanzania(ATCL), Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC), Tanesco, DART, Mamlaka ya Bandari na Kampuni ya Reli nchini TRL, pamoja na Mradi wa Bomba la Mafuta la Afrka Mashariki (EACOP).
Akihitimisha Mbassy aliweka hadharani mpango mkakati wa TIB mwaka 2023/2024, ambapo alibainisha kwamba unalenga sekta za kimkakati ambazo ni maji, nishati na kilimo.
0 Maoni