WAZAZI WAASWA KUTOACHA MALEZI KWA WALIMU PEKEE
Mwandishi Wetu, Kahama
Wazazi wametakiwa kuendelea kushiriki kikamilifu katika kufuatilia maendeleo ya watoto wao kielimu na kimaadili, badala ya jukumu hilo kuwaachia walimu pekee.
Wito huo ulitolewa na Mthibiti Ubora wa Shule wilayani Kahama, Athuman Abeid Al - Jabriy, alipohutubia mahafali ya darasa la saba katika Shule ya Msingi Greenstar, yaliyofanyika mwishoni mwa wiki.
Abeid amesema kuwa dunia ya sasa inakabiliwa na mmomonyoko mkubwa wa maadili, na hivyo ni muhimu kwa wazazi kushirikiana kwa karibu na walimu katika malezi na maendeleo ya watoto.
“Mtoto anapokabidhiwa shule kuanzia awali hadi darasa la saba, ni kipindi cha zaidi ya miaka minane. Kama mzazi hutafuatilia maendeleo yake, na walimu wakipoteza mwelekeo, mzigo wa marekebisho utakuwa juu yako. Tushirikiane katika malezi kwa manufaa ya baadaye ya watoto wetu,” amesema Abeid.
Aidha, amewasihi wahitimu wa darasa la saba kutambua kuwa mahafali si mwisho wa safari ya elimu, bali ni mwanzo wa hatua nyingine muhimu. Alisisitiza kuwa mtihani wa taifa unaokuja unapaswa kupewa kipaumbele cha hali ya juu.
Katika mahafali hayo, Mkurugenzi wa Taasisi wa Shule za Greenstar, Daniel Nchenga alieleza kuwa taasisi hiyo imefanikiwa kuanzisha shule mbili za sekondari; moja ya wavulana na nyingine ya wasichana, ikiwa ni sehemu ya kupanua wigo wa elimu kwa wanafunzi wanaohitimu shule ya msingi.
Nchenga ametumia fursa hiyo kutangaza mpango wa kubadilisha jina la Shule ya Sekondari ya Sister Irene kuwa Greenstar Boys, ambapo aliiomba Ofisi ya Elimu kushirikiana katika kukamilisha mchakato huo kabla ya Januari mwakani.
“Naomba wazazi muendelee kuwahamasisha watoto wenu warudi kujiunga na sekondari zetu. Tunataka jina jipya litambulike mapema ili maandalizi ya kitaaluma yaanze kwa wakati,” amesema Nchenga.
Kwa upande wao, baadhi ya wazazi walioshiriki mahafali hayo wametoa pongezi kwa walimu wa shule hiyo kwa kazi kubwa ya kusimamia taaluma na maadili ya watoto wao.
“Tumeona watoto wetu wakibadilika na kukua kitaaluma na kimaadili. Tunawashukuru walimu kwa juhudi zao kubwa,” Mama Sophia amesema mzazi mmoja kwa niaba ya wenzake.
Mahafali hayo yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa elimu, walimu, wazazi na wanafunzi, huku yakipambwa na burudani mbalimbali kutoka kwa wanafunzi wa shule hiyo.
Maoni
Chapisha Maoni