MAWAKILI SERIKALI WATAKIWA KUSHIKA, KUZINGATIA SHERIA, KANUNI ZA HIFADHI YA JAMII
Mwandishi Wetu,daimatznews@gmail.com
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza S. Johari amewataka Mawakili wa Serikali kuhakikisha kuwa Sheria na Kanuni za Hifadhi ya Jamii zinalinda na kusimamia haki na maslahi ya Wanachama wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii nchini.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kuhusu Hifadhi ya Jamii kwa Mawakili wa Serikali yaliyoandaliwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa PSSSF yanayofanyika Septemba 18 hadi19 Setpemba, 2025 katika Chuo cha Uongozi Mwalimu Nyerere Kibaha, mkoani Pwani.
Johari amesema kuwa mafunzo hayo yatawanufaisha Mawakili wa Serikali kwa kuongeza ujuzi kwenye masuala mbalimbali hasa sheria zinazohusiana na Hifadhi ya Jamii ikiwemo , Sheria ya Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma [Sura ya 371], Sheria ya Mikataba [Sura ya 345], Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini [Sura ya 366], pamoja na Usimamizi wa Fedha na Uwekezaji.
“Ni matarajio yangu kuwa mafunzo haya yatajikita katika maeneo Muhimu ya Kisheria na Kiutawala ikiwemo Muundo wa kisheria wa PSSSF na majukumu yake ya msingi, Haki na Wajibu wa wanachama, wastaafu na wategemezi wao,” amesema Mwanasheria Mkuu huyo wa Serikali
Ameeleza kuwa kupitia mafunzo hayo Mawakili wa Serikali wataweza kuwa na uelewa mpana wa kushauri na kushughulikia masuala ya kisheria yanayohusu Mfuko wa PSSSF, kupunguza migogoro inayoweza kupelekea kesi Mahakamani kwa kutumia mbinu za usuluhishi na mazungumzo.
Kwa mujibu wa Johari wanasheria na mawakili hao wataweza kuweka misingi thabiti ya kisheria katika utekelezaji wa shughuli za kila siku za Mfuko na kujenga uhusiano wa karibu kati ya PSSSF na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa manufaa ya Taifa.Wanasheria wa Serikali wakifuatilia mafunzo yaliyoandaliwa na PSSSF, Kibaha mkoani Pwani leo Septemba 18,2025.
Ametoa wito kwa Mawakili wa Serikali wanaoshiriki mafunzo hayo kuwa na ari na kuhakikisha kuwa maarifa watakayoyapata wanayaweka katika Vitendo na kuhakikisha kuwa PSSSF inaendeshwa kwa ufanisi na kwa mujibu wa Sheria na Kanuni.
Maoni
Chapisha Maoni