Dk. Samia: Tutawaanzishia wakulima vituo kukodi matrekta
-Asema zana zingine pia zitakodishwa
Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
Mgombea Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais Samia Suluhu Hassan amesema akichaguliwa kuiongoza Tanzania katika uchaguzi ujao Oktoba 29,2025 ataanzisha vituo vya ukodishaji matrekta na zana zingine za kilimo kwa wakulima nchini.
Akizungumza katika Uwanja wa Samora ulipofanyika mkutano wa Kampeni za CCM leo Septemba 7 mkoani Iringa, Rais Samia pichani juu, amesema matrekta na zana hizo za kilimo zitakuwa zikikodishwa kwa nusu ya bei ya matrekta ya watu binafsi.
"Endapo Wananchi watanipa ridhaa ya kuongoza tena nchi kwa kunichagua katika Uchaguzi Mkuu Oktoba 29, 2025, Serikali yangu itaendelea kutoa ruzuku ya mbolea na pembejeo kwa wakulima nchini," amesema mgombea.
Kwa mujibu wa mgombea urais huyo kitendo cha Serikali kutoa ruzuku katika mbolea kumeleta tija ya uzalishaji wa mazao na hasa mahindi, yaliyoifanya Tanzania kushika nafasi ya pili kwa uzalishaji Afrika kutokana na kuzalisha zaidi ya tani milioni 10 .
Ameongeza kuwa akipewa ridhaa hiyo kuiongoza Tanzania ataendelea kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo ya miundombinu ya barabara, maji, elimu na afya.
Katika mkutano huo mkubwa uliohitimisha kampeni zake mkoani Iringa, mbali ya kujinadi, Rais Samia pia amewanadi na kuwaombea kura wagombea ubunge na udiwani wa CCM.Akiwa mkoani humo, Rais Samia jana alijinadi eneo la Nyororo na Mafinga wilayani Mufindi pamoja na Kalenga Wilaya ya Iringa Vijijini

Maoni
Chapisha Maoni