TCU yatoa siku 18 udahili awamu ya pili Vyuo Vikuu
-Udahili kuongezeka
Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), imetangaza kufunguliwa kwa Awamu ya pili ya udahili wa Shahada ya Kwanza kwa Mwaka wa Masomo 2025/2026, utakaofanyika kwa siku 18 ukianzia leo Septemba 3 hadi 21, 2025.Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa, akizungumza na wanahabari leo mkoani Dar es Salaam,
Akizungumza na wanahabari leo mkoani Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa, amewataka waombaji walioshindwa kutuma maombi ya udahili au kukosa nafasi katika awamu ya kwanza ya udahili kwa sababu mbalimbali kutumia fursa hiyo kuomba udahili.
Profesa Kihampa, amesema kwamba kufunguliwa kwa dirisha hilo ni hatua iliyofuata kukamilika kwa Awamu ya Kwanza ya Udahili wa Shahada ya Kwanza katika Taasisi za Elimu ya Juu nchini kwa mwaka wa masomo 2025/2026.
"Majina ya waliodahiliwa katika awamu ya kwanza yatatangazwa na vyuo husika kwa mujibu wa utaratibu,"amesema Profesa Kihampa akiongeza:.
"TCU inaelekeza Vyuo vya Elimu ya Juu nchini kutangaza programu ambazo bado zina nafasi na waombaji udahili na vyuo wanapaswa kuzingatia utaratibu wa udahili wa Awamu ya Pili, kama inavyooneshwa kwenye Kalenda ya Udahili iliyoko katika tovuti ya TCU – www.tcu.go.tz."
Kuhusu kukamilika kwa Awamu ya Kwanza ya Udahili, Katibu Mtendaji huyo wa TCU amesema jumla ya waombaji 146,879 walituma maombi ya kujiunga katika vyuo 88 vilivyoidhinishwa kudahili wanafunzi wa Shahada ya Kwanza.
Amefafanua kwamba jumla ya programu 894 za masomo zimeruhusiwa kudahili kwa mwaka wa masomo 2025/2026, ikilinganishwa na programu 856 mwaka 2024/2025, ambalo ni ongezeko la programu 38 za masomo.
Profesa Kihampa amesema kwa upande wa nafasi za udahili, mwaka huu kuna jumla ya nafasi 205,652 zikilinganishwa na nafasi 198,986 mwaka uliopita.
“Hapo kuna ongezeko la nafasi 6,666 ambalo ni sawa na asilimia 3.3 katika programu za Shahada ya Kwanza. Lakini katika Awamu ya Kwanza ya Udahili, jumla ya waombaji 116,596 sawa na asilimia 79.4 ya waombaji wote walioomba udahili wamedahiliwa kwenye vyuo walivyoomba. Katika Awamu ya Pili ya Udahili, idadi ya waombaji na watakaodahiliwa inatarajiwa kuongezeka," anasema Profesa Kihampa.
Amebainisha kwamba waombaji waliodahiliwa katika chuo zaidi ya kimoja wanapaswa kuthibitisha udahili wao katika chuo kimojawapo kuanzia leo Septemba 3, hadi Septemba 21, 2025 na kwamba uthibitisho huo unafanyika kwa kutumia namba maalum ya siri iliyotumwa kwa ujumbe mfupi kupitia namba zao za simu, au barua pepe walizotumia wakati wa kuomba udahili.
“Wale ambao hawatapata ujumbe huo kwa wakati, wanashauriwa kuingia kwenye mifumo ya udahili ya vyuo walivyodahiliwa na kuomba kutumiwa ujumbe mfupi wenye namba maalum ya siri ili kuithibitisha katika chuo husika” amehitimisha.
Maoni
Chapisha Maoni