Jumanne, 5 Agosti 2025

Mikakati, miradi ya NHC 2025-2026 iliyowasilisha kwa Waziri wa Ardhi hii hapa

 

-  Ni ujenzi wa makazi, mifumo ya kibiashara wapaa

-Yaja na majawabu changamoto upungufu nyumba bora

-Yaendelea kuwa kinara miradi ya kimkakati 

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Katika kipindi hiki ambapo Tanzania inawekeza kwa kasi katika maendeleo ya miundombinu, ustawi wa jamii na ukuaji wa uchumi jumuishi, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limewasilisha taarifa ya miradi na mwelekeo wa mikakati yake mbele ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi, huku likiendelea kuwa chombo muhimu katika kusukuma mbele ajenda ya Taifa ya makazi bora kwa Watanzania wote. 

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi

NHC imetekeleza hilo hivi karibuni, wakati Waziri  Ndejembi, alipotembelea Makao Makuu ya NHC, akiongozana na uongozi wa juu wa wizara,ambapo alikutana na menejimenti ya NHC kwa lengo la kujionea hatua za utekelezaji wa miradi mbalimbali na kutoa mwongozo wa kisera.

Katika ziara hiyo NHC ilitoa maelezo ya kina kuhusu utekelezaji wa miradi yake ya kimkakati kote nchini, ikieleza kuwa haikujikita tu katika ujenzi wa majengo ya kisasa, bali pia inajenga matumaini, heshima ya jamii na kubadilisha mandhari ya mijini na vijijini.

Mwaka 2025 unaashiria ukurasa mpya kwa Shirika hili la umma. Kupitia miongozo ya Dira ya Taifa na mahitaji halisi ya wananchi, NHC likiendelea kujidhihirisha kuwa muhimili wa maendeleo katika sekta ya makazi, likitekeleza pia miradi yenye tija kwa taifa.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi(Kushoto), akisaini kitabu cha wageni, wakati alipofanya ziara Makao Makuu ya NHC hivi karibuni. Kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah.

Katika kikao hicho, Mkurugenzi wa Ujenzi wa NHC, Mhandisi Godwin Maro, aliwasilisha taarifa ya maendeleo ya miradi mikubwa inayoendelea, akibainisha kuwa NHC sio tu linaboresha makazi ya wananchi, bali pia linachochea uchumi, linatoa ajira, na kuchangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha taswira ya miji na mikoa mbalimbali.

Dodoma: Jiji Kuu linalokua kwa kasi

Akitoa taarifa yake mbele ya Waziri Ndejembi, Mhandisi Maro anaeleza kuwa, katika Jiji la Dodoma, ambako Serikali imewekeza sana kulifanya kuwa kitovu cha utawala wa kisasa, NHC linaendelea na ujenzi wa Mradi wa Samia Iyumbu Apartments. Mradi huu unatarajiwa kutoa zaidi ya nyumba 300 kwa wananchi wa kipato cha kati na cha juu.

Mradi huo umesanifiwa kwa kuzingatia mahitaji ya kisasa ya familia, na una miundombinu muhimu kama barabara, maji safi, umeme, shule na huduma za afya. “Mradi huu ni kielelezo cha miradi ya makazi inayojibu mahitaji ya sasa ya miji inayopanuka kwa kasi,” amesema Maro.

Dar es Salaam: Miradi ya kibiashara na makazi

Akizungumzia Dar es Salaam, Mhandisi Maro anasema NHC ina mradi unaoendelea katika eneo la Mtanda, inpojengwa Mtanda Commercial Complex ambao sasa umefikia asilimia 75.

Anasema kazi za kumalizia sehemu za nje ya jengo zimeanza, na maandalizi ya kupokea wapangaji wa muda mrefu yanaendelea. Mradi huu wa thamani ya Shilingi bilioni 4.2 unatarajiwa kuwa kitovu kipya cha biashara jijini.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi(Mbele), akizungumza  na Menejimenti ya NHC, wakati alipofanya ziara Makao Makuu ya shirika hilo hivi karibuni. 

Vilevile, katika Wilaya ya Temeke, NHC linaendelea na Samia Kijichi Housing Scheme, mradi wa nyumba zaidi ya 300, unaolenga kuwasaidia wananchi wa kipato cha kati kupata makazi ya gharama nafuu yenye huduma muhimu. Miradi ya maghala yenye ubunifu kwa maendeleo

Kwa mujibu wa NHC katika eneo la Kawe, Dar es Salaam, linaendelea na Samia Housing Scheme, mradi mkubwa wa nyumba 560 zilizokamilika, huku nyingine 560 zikiwa katika maandalizi ya ujenzi. Mradi huu ni mfano bora wa makazi ya gharama nafuu yenye viwango vya kisasa.

Pia, NHC linaendelea na ujenzi wa maghala matatu ya kisasa kwa ajili ya kuhifadhi bidhaa na vifaa, likilenga kuongeza mapato yake na kutoa huduma muhimu kwa wafanyabiashara katika sekta ya usafirishaji na usambazaji.

Wajumbe wa Menejimenti wa NHC wakifuatilia kikao chao na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi(Hayupo pichani), wakati waziri huyo alipofanya ziara Makao Makuu ya shirika hilo.

Tanga, Singida na mikoa ya pembezoni

Katika Jiji la Tanga, Mhandisi Maro anabainisha kwamba NHC linaendelea na ujenzi wa Mradi wa Mkwakwani, wenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 7. Anasema: “Eneo hili lilikuwa halijashuhudia uwekezaji mkubwa katika makazi ya kisasa kwa muda mrefu, hivyo mradi huu unatarajiwa kufungua fursa za ajira na kuamsha ari ya uwekezaji katika ukanda wa kaskazini.”

Anaweka wazi kuwa katika Manispaa ya Singida, kuna Mradi wa 2F, ambao umefikia hatua ya kuweka ubamba wa zege (slab) wa ghorofa ya chini. Anasema mbali na kuongeza nyumba bora kwa wakazi wa Singida, mradi huu unawanufaisha mafundi, wauzaji wa vifaa vya ujenzi na watoa huduma wa ndani.

Sekta ya Madini: Soko la Kisasa Mirerani

Kuhusu Sekta ya Madini, Mhandisi Maro alimweleza Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuwa, katika Mkoa wa Manyara, eneo la Mirerani, NHC linaendelea na ujenzi wa Soko la Kisasa la Madini.

Anasema mradi huo unalenga kuboresha mazingira ya biashara ya madini, kuongeza usalama na thamani ya Tanzanite. Soko hili ni sehemu ya mpango wa Serikali wa kuwainua wachimbaji wadogo na kufanikisha biashara rasmi ya madini.

Morogoro na Kagera, majibu kwa mahitaji ya makazi

Katika Jiji la Morogoro, NHC linaendelea na Mradi wa 2H Plaza, wenye thamani ya Shilingi bilioni 2.6 na tayari baadhi ya nyumba zimeuzwa kabla ya ujenzi kukamilika, ikionesha imani kubwa ya wananchi kwa ubora wa bidhaa za NHC.

Waziri Ndejembi ameelezwa kuwa katika Mkoa wa Kagera, Mradi wa Kashozi umeshaingia katika awamu ya kwanza ya ujenzi, ukiwa na thamani ya Shilingi bilioni 1.8. “Mradi huu unapanua wigo wa upatikanaji wa nyumba bora katika mikoa ya pembezoni, ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikisubiri uwekezaji wa aina hii,” anasema Mhandisi Maro.

Tabora, Arusha na Dodoma: Miji ya kimkakati

Kwa mujibu wa Mkurugenzi  huyo wa Ujenzi wa NHC, katika Mji wa Tabora, NHC linaendelea na ujenzi wa Tabora Commercial Complex, ambacho ni kituo cha kisasa cha huduma mbalimbali kinacholenga kuongeza huduma karibu na wananchi na kuchochea shughuli za kiuchumi katika eneo hilo.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Ndejembi, akisisitiza jambo wakati wa kikao chake na Menejimenti ya NHC, alipofanya ziara Makao Makuu ya shirika hilo, Dar es Salam hivi karibuni.

Katika Jiji la Arusha, kuna Mradi wa Meru Shops, ambao umeboreshwa kutoka jengo la ghorofa moja hadi mbili, ili kukidhi mahitaji ya wafanyabiashara wadogo na wa kati na kuongeza mapato ya ndani ya Shirika.

Huku wajumbe wengine wa Menejmenti ya NHC wakifuatilia maelezo hayo mbele ya Waziri Ndejembi, Mhandisi Maro anaeleza kuwa katika eneo la Njendengwa jijini Dodoma, NHC linaendelea na ujenzi wa nyumba zaidi ya 120, hasa kwa ajili ya watumishi wa umma na sekta binafsi, likiwa ni jibu kwa ongezeko la idadi ya watu na kasi ya uwekezaji serikalini.

Kukarabati miradi ya zamani, kuhifadhi urithi, kuendana na wakati

Mbali na miradi mipya, NHC linafanyia ukarabati mkubwa majengo ya zamani, likiboresha mifumo ya umeme, maji, barabara za ndani na mandhari ya nje. Hatua hii inalenga kuyawezesha majengo hayo kuendana na mahitaji ya sasa pasipo kupoteza uzito wake wa kihistoria.

NHC inajenga zaidi ya nyumba

Kwa ujumla, utekelezaji wa miradi hii si tu unaleta nyumba bora kwa wananchi, bali pia unatoa ajira, unachochea uchumi, na unaendeleza miji kwa namna endelevu. NHC haijengi tu kuta na paa, bali linajenga heshima, utu na mustakabali mpya wa Watanzania.

Kwa kasi hii ya utekelezaji, ubunifu na uwajibikaji, bila shaka NHC ni mshirika madhubuti wa maendeleo ya taifa na dira ya makazi bora kwa wote inazidi kuwa karibu kuliko ilivyowahi kuwa

 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni