Ngome ya Jeshi la Ujerumani, JWTZ kivutio kipya cha utalii wa ndani Serengeti
-Watanzania waitwa kutalii
Na Exuperius Kachenje,daimatznews@gmail.com
Ngome ya Jeshi ya zamani y Jeshi la Ujerumani na
Jeshi la Wananchi wa Tanzania, maarufu kwa Jina la Fort Ikoma iliyopo Hifadhi
ya Taifa Serengeti, imetajwa kuwa eneo la kipekee linalovutia watalii ndani ya
hifadhi hiyo na tasnia ya utalii nchini likiunganisha historia na asili, huku
watanzania wakihimizwa kufanya utalii wa ndani ili kujifunza na kufurahia
utajiri wa rasilimali za taifa.Twiga wakijivinjari maeneo ya Fort Ikoma, ndani ya Hifadhi ya Taifa Serengeti. Picha zote na Exuperius Kachenje.
Ofisa Uhusiano ya Jamii wa Hifadhi ya Taifa Serengeti,
Abed Mwesigwa amebainisha hayo ndani ya eneo hilo alipokuwa akieleza kuhusu
utajiri wa historia na rasilimali zilizopo ndani ya hifadhi hiyo mbele ya
waandishi wa habari waliofanya ziara hifadhini hapo jana.
Mwesigwa amesema: “Mtalii yeyote akifika
Serengeti bila kutembelea Fort Ikoma atakuwa amekosa kupata utajiri wa historia
na asili kwani eneo hilo ndipo asili inayojumuisha wanyamapori na ekolojia ya
hifadhi zinakutanishwa na historia ya ngome hiyo yenye masimulizi ya
kusisimua.”
Mwesigwa amebainisha kwamba, Fort Ikoma
ilijengwa na wakoloni Wajerumani mwaka 1905, ikiwa ngome yao ya kijeshi wakati ikiitawala
Tanzania Bara (Tanganyika), ikiwa katika pembe ya Kaskazini Magharibi ya hifadhi
maarufu duniani ya Serengeti iliyo chini ya Shirika la Hifadhi za Taifa
(TANAPA), iliyobeba tuzo za kimataifa za ubora duniani kwa miaka sita mfululizo
ya European Award for Quality Choice Achievement 2025.
“Ukidhani Serengeti ni simba, nyumbu na uwanda
usio na mwisho pekee, fikiria tena na uje kuishuhudia Fort Ikoma na kujua
historia yake. Kukosa kuitembelea ni sawa na kusoma riwaya ya kusisimua kwa kuiruka
sura ya kwanza,” amesema Mwesigwa.
Waandishi wa Habari waliotembelea Hifadhi ya
Taifa Serengeti, inayoshikilia tuzo ya Hifadhi Bora Afrika kwa miaka mitano
mfululizo mwaka 2019 -2023, waliishuhudia Fort Ikoma, majengo yake yaliyojengwa
kwa mawe na kuwekwa nakshi zinazovutia licha ya kujengwa zaidi ya miaka mia moja
iliyopita.
Kwa mujibu wa Mwesigwa, jengo hilo ni ishara ya
nguvu na utawala wa Ujerumani kwa wakati huo, likiwa kwenye muinuko wa juu,
uliowawezesha kuona maadui kwa mbali kutoka pande zote, hivyo kujihami kwa
urahisi huku historia ikionyesha, Wajerumani walinyang’anywa koloni lao
Tanganyika na kupewa Uingereza, baada ya Vita Kuu ya Dunia mwaka1914 - 1918,
hivyo Fort Ikoma ikawa mikononi mwa Uingereza.Wanahabari, wakiingia Fort Ikoma kushuhudia eneo hilo la kihistoria,
“Leo, watalii wanaweza kutembelea magofu hayo, kutembea katika mapango yake yenye hadithi ya kusisimua na kujiwekea picha ya wanajeshi, viongozi na jamii za wenyeji waliowahi kuipa uhai ngome hiyo iliyojaa matundu ya risasi yaliyotokana na mapambano.” amesema Mwesigwa na kuongeza:
Fort Ikoma ipo
katikati ya mfumo wa ikolojia wa Serengeti, hivyo ni mahali bora pa kushuhudia uhamaji
wa wanyama, kuona wawindaji wakifanya yao na kufurahia machweo ya jua
yanayoangaza savanna na kuta za kale kwa mwanga wa dhahabu.
Mwesigwa anasema kuwa baada ya kupata uhuru
mwaka 1961, Serikali chini ya Rais wa kwanza na mwasisi wa Tanzania, Hayati
Mwalimu Julius Nyerere ililitwaa eneo hilo kutoka kwa Wakoloni wa Uingereza na
kulifanya kuwa kambi ya Jeshi la Wananchi (JWTZ).
Hata hivyo, Mwesigwa ameeleza kwamba mwaka
1997, Serikali ilifanya uamuzi mkubwa wa mabadiliko, ambapo ikaliweka eneo la Fort
Ikoma kuwa chini ya Mamlaka ya Hifadhi za Taifa. (TANAPA), ikiwa sehemu ya
Hifadhi ya Taifa Serengeti, pia Ofisi Kuu ya Uhusiano na Jamii.
“Serikali iliona Fort Ikoma isingeendelea kuwa
kambi ya kijeshi, bali kuwa sehemu ya mtandao wa Hifadhi za Taifa (TANAPA),
hivyo ikaingizwa rasmi ndani ya mipaka ya Hifadhi ya Serengeti. Tangu wakati
huo, Fort Ikoma imeibuka si tu kama kivutio cha kihistoria, urithi wa utalii na
daraja kati ya historia,wanyamapori na uoto wa asili.Waandishi wa habari wakishuhudia sehemu ya ngome (Fort Ikoma) wakati walipotembelea eneo hilo.,
Mwesigwa amesema msafiri anayependa kutembelea Fort
Ikoma siyo tu kituo cha kupita bali sehemu ya kupata ujumbe, ukumbusho kuwa
Serengeti siyo safari tu ya kuona Wanyama bali ni jumba la makumbusho hai la
historia, mapambano na mabadiliko.
Maoni
Chapisha Maoni