'Maendeleo yanavyotafuna vijana kimaadili'
Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
Ukuaji wa utandawazi umetajwa kuchangia kundi kubwa la vijana nchini kutokana na kukua na kuenea kwa sayansi na teknolojia inayogusa kwa karibu vijana, ikielezwa sehemu kubwa ya kundi hilo limetafunwa na maendeleo hayo kwa kupotoka kimadili.
Mkufunzi wa Shirika la Kutetea Uhai Tanzania (ProLifeTz), Godfrey Mkaikuta pichani juu, amesema hayo Aprili 16, 2024 wakati akijadili Mada ya Maisha ya Vijana katika Dunia ya Leo, iliyoandaliwa na ProLifeTz kwa vijana wa Jimbo Katoliki Ifakara.
"Wazazi na walezi wa Tanzania, ulimwengu unatudai kubaki katika msingi wa malezi ya tamaduni na asili za kiafrika kwa kuwafanya vijana na watoto kupenda na kuheshimu maadili yao, pia kujiepusha na tamaduni za mataifa ya nje," amesema Mkaikuta.
Katika tafakari yake, Mkaikuta amesema vijana wengi wameutoa utu wao wa ndani waliopewa na Mungu kwa kukimbilia mambo ya kigeni, wakijidanganya kwamba ni mabadiliko na ukuaji wa sayansi na teknolojia.
"Ifike pahali tuone si jambo la kawaida kukuta kijana wa kiume amevaa hereni, au amevaa mavazi yampasayo mwanamke. Tukemee kwa uwazi na tusidanganywe na teknolojia kwamba ni sawa au ni sanaa. Tusione kawaida mwanafunzi kukatisha masomo kwa sababu ya mimba, tukemee ngono na matumizi ya vitu vinavyoharibu utu wa vijana wa leo" amesema Mkaikuta.
Ametahadharisha kwamba, teknolojia ya sasa isiwafanye wazazi na walezi kuona ni sawa kwa mtoto kuwa huru kutumia mifumo ya kisasa kwa uhuru pasipo uangalizi wa wazazi nyumbani na kusahau kwamba mifumo hiyo imewekwa vitu vingi viovu vinavyoweza kuharibu makuzi ya mtoto ambaye ni kijana wa baadae, baba au mama wa kesho.
Kwa mujibu wa Mkalukuta, utandawazi umesabisha kushamiri kwa matumizi ya vitu vingi viovu, ikiwemo, vidhibiti mimba na ushoga miongoni mwa vijana, hali aliyosema inaharibu utu wao na uwezo wao wa baadae wa kuwa mama na baba.
Mkufunzi huyo amesema kilio na mahangaiko yanayowakuta wanandoa wa sasa, kupungua kwa uwezo wa wanaume katika tendo la ndoa na wanawake kupoteza uwezo wa kubeba mimba ni matokeo ya utandawazi unaopambwa na lugha nzuri ya mpango wa uzazi na kusahau kwamba mpango huo unaharibu na kuua uwezo wa mwanamke kubeba mimba.
Amesema tangu kuanza kwa utandawazi miaka ya 1990, mmomonyoko wa maadili katika jamii hasa vijana umeongezeka, ikiwemo mimba za utotoni, vijana kujiingiza kwenye matumizi ya dawa za kulevya, unywaji pombe uliokidhiri na uchezaji wa michezo ya kubahatisha ambayo imedumaza akili zao kwa kutaka pesa za harakaharaka, wakisahau kuwa wao ni wazazi wa kesho.
Amesema matokeo ya mmomonyoko wa maadili kwa jamii unashuhudia pia kuongezeka kwa ukahaba na uasherati kabla ya ndoa ambavyo husababisha mimba za utotoni, vijana kudumaa katika ukuaji kimwili, kiakili na kiimani, pia kushamiri kwa magonjwa ya zinaa, viungo vya uzazi kuchakaa kuzeeka kabla ya wakati wake.
Mkalukuta amesisitiza kuwa ulimwengu unawadai wazazi wa Tanzania kubaki katika misimamo wa kimaadili ya kiafrika ili kukabili mmomonyoko wa maadili unaopoteza vijana na watoto wengi walio taifa la kesho, ambao sasa wanaharibiwa kile wanachokiona kwenye mitandao wakitamani kujaribu kila kitu.
Maoni
Chapisha Maoni