BENJAMIN NGAYIWA AAHIDI KUTOKOMEZA MIGOGORO YA ARDHI

Mwandishi Wetu, Kahama

Mgombea Ubunge wa Jimbo la Kahama Mjini kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Benjamin Ngayiwa, ameweka wazi dhamira yake ya kumaliza kabisa changamoto ya migogoro ya ardhi inayowakumba wakazi wa jimbo hilo kwa muda mrefu.

 Akiwa kwenye uzinduzi wa kampeni za CCM ngazi ya jimbo, uliofanyika katika viwanja vya Phantom, Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, mkoani Shinyanga, Ngayiwa amewahakikishia wananchi kuwa ardhi haitakuwa chanzo cha migogoro tena endapo atapewa ridhaa ya kuwa Mbunge wao.

Katika hotuba yake, Ngayiwa alisisitiza kuwa atashirikiana kwa karibu na Madiwani pamoja na Wenyeviti wa Mitaa ili kuhakikisha kuwa migogoro yote ya ardhi inatatuliwa kwa haki na kwa wakati.

Aidha, Ngayiwa ametoa wito maalum kwa Wenyeviti wa Serikali za Mitaa kuacha mara moja tabia ya kupima na kuwauzia watu zaidi ya mmoja kiwanja kimoja. 

Amesema kuwa utaratibu huo siyo tu unawanyima haki wananchi, bali pia umekuwa chanzo kikuu cha migogoro isiyokwisha ya ardhi katika maeneo mengi ya Kahama.

Katika kuhakikisha wananchi wanamwelewa vyema, mgombea wao, viongozi mbalimbali wa CCM walijitokeza kumpigia debe. Emanuel Cherehani, Mgombea Ubunge wa Jimbo la Ushetu, akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa, amesema kuwa Ngayiwa ni chaguo sahihi kwa wana Kahama.

 Amesema kuwa ana imani kubwa kuwa Ngayiwa atakuwa kiungo muhimu kati ya wananchi na Serikali katika kuhakikisha ndoto za wananchi wa Jimbo hilo zinatimia.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Mabala Mlolwa, amewaomba wananchi wa Kahama kuwapa kura zote wagombea wa CCM – kuanzia Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Benjamin Ngayiwa, hadi Madiwani – ili kuhakikisha kuwa maendeleo ya kweli yanapatikana kwa kasi na kwa usawa katika Jimbo la Kahama.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Sanamu ya Bikira Maria yaonekana ndani ya Hifadhi ya Taifa Saadani

Kapteni Traole afuata huduma za afya nchini

Wawekezaji wa Oman watua nchini, wateta na NHC kuchochea mapinduzi sekta ya makazi