Kapteni Traole afuata huduma za afya nchini
- Aichagua JKCI kupata huduma za kibingwa
- Burkina Faso yasaini makubaliano na JKCI
Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
Rais wa Burkina Faso,Kapteni Ibrahim Traore amefuata huduma bora za afya zinazotolewa nchini, hasa za magonjwa ya moyo.
![]() |
Rais wa Burkina Faso, Kapteni Ibrahim Traore |
Ndivyo unavyoweza kueleza, baada kiongozi huyo maarufu duniani,kutuma mwakilishi wake wa masuala ya afya Burkina Faso nchini kuzungumza na kutiliana saini hati ya makubaliano na Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), katika kutoa huduma bobezi ya matibabu ya magonjwa ya moyo.
Kwa mujibu wa JKCI, hati hizo zimesainiwa kati ya Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya
Kikwete (JKCI), Dk. Peter Kisenge na Mshauri wa Rais wa Burkina Faso na Mratibu
wa Kitaifa wa Mpango wa Afya wa Rais, Drissa Traore, jana jijini Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya kusaini
makubaliano hayo, Dk. Kisenge amesema makubaliano hayo yataimarisha utoaji
wa huduma za matibabu ya moyo nchini Burkina Faso na kuokoa maisha
ya wananchi wenye matatizo ya moyo.
“Tumekubaliana kuwasaidia katika kufanya tatifi, kuwafundisha wataalamu wa afya wakiwemo madaktari, wauguzi na wataalamu wa vifaa tiba jinsi ya kuwatibu wagonjwa wa moyo na namna ya kutumia vifaa tiba vya moyo, pia watatuma wagonjwa walioshindwa kuwafanyia upasuaji, waje kutibiwa kwenye taasisi yetu.”
“Katika kutoa mafunzo ya kutibu
wagonjwa ya moyo kuna wataalamu wetu watakwenda Burkina Faso kufundisha
na kuna wataalamu kutoka nchini humo watakaokuja kujifunza katika
taasisi yetu,” amesema Dk. Kisenge
Dk. Kisenge ambaye pia ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo, amesema kuhusu upatikanaji wa vifaa tiba, wamekubaliana wanunue katika Bohari ya Dawa nchini(MSD), ambao ni
wasambazaji wa vifaa hivyo JKCI.
“Kwa namna ya kipekee namshukuru sana Mhe. Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kuimarisha tiba ya magonjwa ya moyo katika taasisi yetu, kitu ambacho kimesababisha nchi mbalimbali kuja kujifunza namna ya kutoa matibabu ya moyo katika nchi zao, pia kuwaleta wagonjwa wao kutibiwa JKCI;
“Pia ninamshukuru Rais wa Bukina
Faso, Kapteni Ibrahim Traore kwa kuiamini nchi yetu na kuwatuma
wataalamu wake, ambao tumesaini makubaliano nao ili nao kupitia sisi wawe
taasisi bora ya matibabu ya moyo na kufika hatua tuliyoifikia sisi.Leo
tumeingia katika historia na Burkina Faso ya kutangaza utalii tiba, ambao
umekuja katika afya,” amesema Dk. Kisenge.
Kwa upande wake, Mshauri wa Rais wa Burkina Faso na Mratibu wa Kitaifa wa Mpango wa Afya wa Rais, Drissa Traore ambaye kwa mara ya pili ameongoza timu hiyo ya wataalamu kuja hapa nchini, amesema siku ya kwanza walipotembelea JKCI walivutiwa kwa huduma wanazozitoa pamoja na uhusiano mzuri wa uongozi na manejimenti uliokuwepo, baada ya kurudi nchini kwao walivichukua hivyo vyote na kuvifanyia kazi.
“Ninawashukuru maraisi wetu wa
Burkina Faso, Kapteni Ibrahim Traore na wa Tanzania Mhe. Dk.
Samia Suluhu Hassan kwa kuwa tayari kuimarisha huduma za afya katika nchi zao,
nimevutiwa na JKCI kwani haitoi huduma tu Tanzania, bali Afrika
nzima na ndiyo maana nasi tumekuja kujifunza. Tunawategemea sana katika
mafunzo, tafiti na matibabu ya moyo kwa afya za watu wa Burkina Faso”, alisema
Traore.
Mapema mwezi wa pili mwaka huu, Rais
wa Burkina Faso, Kapteni Ibrahim Traore alituma timu ya wataalamu kwenda
kujifunza katika taasisi hiyo na kuona hatua walizopitia katika tiba
ya moyo hadi kuwa moja ya Taasisi zinazoongoza Barani Afrika kutoa huduma za
kibingwa bobezi ili nao waweze kujifunza na kuboresha huduma za matibabu ya
moyo nchini humo.
Utiaji saini wa makubaliano hayo ni
jitihada zilizofanywa na Ubalozi wa Tanzania nchini Burkina Faso, unaowakilisha
nchi hiyo kutokea Abuja, Nigeria unaoongozwa na Balozi Selestine Kakele, ambao waliratibu mawasiliano ya JKCI na Burkina Faso hatimaye kufanikisha kusainiwa kwa hati ya makubaliano ya ushirikiano
huo.
Maoni
Chapisha Maoni