Sanamu ya Bikira Maria yaonekana ndani ya Hifadhi ya Taifa Saadani

 -Maajabu mapya ya kipekee

Exuperius Kachenje

Sanamu yenye mwonekano wa Bikira Maria (Mariam), anayetajwa na vitabu vitakatifu vya Biblia Takatifu na Qur’an Tukufu (Mariam), ndiye mama wa Yesu Kristo (Nabii Issa bin Mariam), imegundulika ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Saadani, ikitajwa kuwa ni maajabu mapya yasiyo ya kawaida kwa watalii ndani na nje ya Tanzania, inayoongeza upekee wa hifadhi hiyo kwa utalii.

Mti wa mbuyu wenye sanamu yenye mwonekano wa Bikira Maria uliopo ndani ya Hifadhi ya Taifa Saadan. Picha na Exuperius Kachenje
Ofisa Mhifadhi kitengo cha uta;ii, Hifadhi ya Taifa Saadani (SANAPA) Daud Gordon amebainisha hayo Juni 26, 2025 akieleza kwamba kivutio hicho kipya ni nyenzo muhimu katika kukuza utalii wa kiimani, hata kuweza kuwa sehemu ya hija kwa waamini, hasa wanaoamini na kumheshimu mama huyo kadiri ya mapokeo ya imani zao,mfano ukiwa Kanisa Katoliki.

Gordon amesema kuwa sanamu hiyo ya asili inaonekana katikati ya mti wa mbuyu, eneo la Buyuni  ndani ya hifadhi hiyo, inaweza kuwapa watalii fursa nzuri ya kutafakari kuhusu uumbaji wa Mungu,ukuu wakee na imani wanazozishikilia, huku wakiwa katikati ya maajabu ya asili.

“Jambo hili ni la kipekee, mtajionea, wala sio hadithi.  Ni uhalisia, sanamu hiyo, inaonekana ndani ya mti wa mbuyu, watalii wanaofika hapa wanaweza kujionea, nanyi wanahabari mliotembelea hifadhi yetu,” amesema Gordon.  

Kwa mujibu wa Gordon, sanamu hiyo ipo ndani ya Hifadhi ya Saadani yenye ukubwa wa Kilometa za Mraba 1,100 iliyopo katika mikoa ya Pwani Wilaya ya Bagamoyo na Tanga, Wilaya ya Pangani naHandeni ikiwa hifadhi pekee nchini inayopakana moja kwa moja na Bahari ya Hindi.”

Amesema tayari watalii wa  ndani na nje wameanza kutembelea sanamu hiyo, huku akihimiza watalii zaidi hasa wa  ndani kufika ili kujionea maajabu hayo, pamoja vivutio vingine ndani ya Hifadhi ya Taifa Saadan.

Kaimu Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Saadani (SANAPA) Daud Gordon,akizungumza na wanahabari waliotembelea hifadhi hiyo Juni 25/26-2025.Picha na Exuperius Kachenje

Akitoa maelezo zaidi, mwongoza watalii katika hifadhi hiyo, Fredy Nesto amesema sanamu hiyo iligundulika mwaka 2019.

Amesema mbuyu huo una zaidi ya miaka 100 huku historia ikionyesha kuwa kwa kipindi fulani wakoloni waliutumia kunyongea watumwa.

“Sanamu hiyo ya Bikira Maria inaonekana vizuri zaidi mtu akiwa umbali wa wastani, lakini ukiwa karibu inapotea, hayo pia ni majabu ya sanamu hiyo,”  amesema Nesto  akiongeza kuwa taarifa za uwepo wa sanamu hiyo zimelifikia Kanisa Katoliki, huku bahari za ndani zikionyesha kanisa hilo linafuatilia taarifa hizo kwa karibu.

Amesema tayari watalii kutoka maeneo mbalimbali wameanza kufika eneo hilo na kuitumia kwa maombi kwa shida mbalimbali walizonazo, baadhi wakirudi kueleza maombowaliyofanya eneohilo yamefanikisha kuondoa shida zao.

Kaimu Mkuu wa hifadhi amesema upekee wa Hifadhi ya Taifa Saadan hauishii  kwenye mandhari ya kuvutia ya pwani, bali pia wanyamapori kama simba, tembo na pundamilia, huweza kuonekana wakifika ufukweni kupumzika, jambo ambalo ni adimu duniani.”

Kwa mujibu wa Gordon, hifadhi hiyo pia ina mazalia ya kasa wa baharini, ambao huvutwa na mazingira ya hifadhi hiyo wakati wa msimu wa kuzaliana kutoka maeneo mbalimbali ya Bahari duniani.

Ametaja pia mchanganyiko wa maji kati ya Mto Pangani na Bahari ya Hindi kuwa unaongeza uzuri wa kiasili wa hifadhi hiyo.

Mhifadhi huyo ametaja uwepo wa aina nne kati ya tano za wanyama wakubwa wa Afrika, ambao ni Tembo, Simba, Twiga na Nyati, huku Faru pekee akikosekana.

Amesema  hayo yote kwa pamoja yanaifanya Hifadhi ya Taifa Saadani kuwa hifadhi ya kipekee nchini Tanzania na barani Afrika.

 

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Kapteni Traole afuata huduma za afya nchini

Wawekezaji wa Oman watua nchini, wateta na NHC kuchochea mapinduzi sekta ya makazi