Alhamisi, 30 Januari 2025

Mtoto wa Mbowe hatarini kutupwa 'lupango'

-Yupo mikononi mwa Jaji -Ni kukaidi amri ya mahakama -Mishahara ya wanahabari yamponza Na Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com Mkurugenzi wa Gazeti la Tanzania Daima, Dudley Mbowe yupo hatarini kutupwa gerezani, baada ya maombi ya wanahabari 10 wanaomdai malimbikizo ya mishahara kufika mbele ya Jaji, Dk Modesta Opiyo, katika Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi.
Dudley Mbowe
Waandishi hao wamewasilisha ombi la kutaka Dudley ambaye ni mtoto wa Mwenyekiti Mstaafu wa Chadema,Freeman Mbowe akamatwe na kutupwa gerezani baada ya Mkurugenzi huyo wa Gazeti Tanzania Daima kushindwa kuwalipa fedha hizo. 

Wadai ambao ni Maregesi Paul na wenzake 9 waliwasilisha maombi mahakamani hapo ya kumkamata Dudley na kumtupa gerezani kama mfungwa wa kiraia baada ya kushinda tuzo ambayo Dudley hakuitekeleza. 

Januari 14 mwaka huu mahakama hiyo ilimuonya Dudley mbele ya Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Mary Mrio akielezwa hajawahi kufika mahakama licha ya kuahidi kufanya hivyo, huku akiamriwa kufika mahakamani na kulipa malimbikizo hayo kabla ya Januari 31,2025. Siku hiyo, 

Wakili Samadani Mngumi aliyemwakilisha Dudley mahakamani, alidai mbele ya Msajili Mrio kwamba alikuwa hajazungumza na mteja wake zaidi ya kupokea maelekezo ya kufika mahakamani kuomba udhuru. 

Awali Mahakama hiyo ilitoa amri ya waandishi hao kulipwa baada ya kupitia hoja za washinda tuzo katika Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) Julai 2023. Shauri hilo namba 28461 la mwaka 2023, wadai Maregesi Paul na wenzake tisa dhidi ya Mkurugenzi wa Gazeti la Tanzania Daima, Dudley Mbowe. 

Maregesi nawenzake 9 walipata tuzo Julai 17 mwaka 2023 mbele ya Msuluhidhi wa CMA Ilala, Bonasia Mollel. 
Madai ya awali yalikuwa jumla ya Sh, milioni 114.lakini baada ya kukaa mezani kwa majadiliano, kiwango hicho cha fedha kilishuka na kufikia Sh. milioni 62.7.

Mkurugenzi wa Tanzania Daima (Dudley), alikubali kulipa fedha hizo kwa awamu tatu, Oktoba 30, Desemba 30 mwaka 2023 na awamu ya mwisho ilikuwa mwishoni Februari mwaka jana, hata hivyo hakulipa. 

Dudley aliingia makubaliano ya kulipa malimbikizo hayo nje ya Mahakama Aprili hadi Mei mwaka jana, lakini pia hajafanya hivyo.

Jumanne, 14 Januari 2025

Miaka minne ya Rais Samia madarakani ilivyoifungua NHC

- Mapato yaongezeka hadi Sh. bilioni 9.4  - Thamani yapaa kufikia Sh. trilioni 5.47

- Miradi, ndoto makazi bora vyatekelezwa

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Rais Samia Suluhu Hassan akiapa kuiongoza Tanzania, Machi 19,2021. Kiongozi huyo atatimiza miaka minne madarakani Machi 19, mwaka huu.  


Unapozungumzia mageuzi katika sekta ya nyumba Tanzania, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), litakuwa la kwanza kulitaja. Hii inatokana na ukweli usiopingika kwamba NHC ndiyo chachu ya mageuzi hayo makubwa nchini.
Hakuna kificho kwamba jukumu pekee na kubwa la NHC tangu kuundwa kwake muda mfupi baada ya Uhuru wa Tanzania Bara mwaka 1961 ni kuwawezesha Watanzania kupata makazi bora.
Ikumbukwe kuwa Shirika la Nyumba la Taifa, limeanzishwa mwaka 1962 chini ya Sheria ya Bunge Na. 45 na tangu wakati huo, limekuwa likitimiza jukumu lake hilo la kipekee kwa Watanzania kuwapatia makazi bora. 

Hayo ndio maono ya NHC, iliyoyaakisi kutoka kwa muasisi wake, Rais wa Kwanza wa Tanzania, Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, yaliyoendelezwa na viongozi wa awamu zilizofuata na sasa taifa likiwa katika Awamu ya Sita ya uongozi, chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, anayetimiza miaka minne madarakani Machi 19, mwaka huu 2025.

Hakuna wa kubisha kwamba utendaji wa NHC unaongozwa na Dira ya Maendeleo Endelevu ya Makazi, ambayo imepata msukumo na kasi mpya, zilizozaa mafanikio makubwa ya kupigiwa mfano, yaliyoacha historia ya kipekee kwa Watanzania ndani ya kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.

Safari ya mafanikio NHC 

Mkurugenzi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Hamad Abdallah (mbele), akimuongoza Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uwekezaji Mitaji ya Umma (PIC), Augustine Vuma (nyuma yake) na wajumbe wengine wa kamati hiyo kutembelea mradi wa  ofisi za  kudumu za wizara nane za Serikali wenye thamani ya Sh. bilioni 186.8 kwenye Mji wa Serikali, Mtumba, Dodoma, Oktoba 26,2024

NHC ambayo hadi sasa imeshaongozwa na wakurugenzi tofauti 12 tangu kuanzishwa kwake, awali ilitekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi wa nyumba za makazi na majengo ya umma, ikiwamo kuwajengea na kuwauzia wananchi kwa gharama nafuu. Hata hivyo, baadaye kuliibuka changamoto za kiuchumi na kisheria, ambazo ziliathiri utendaji wa NHC, lakini zilitafutiwa ufumbuzi.

Ufumbuzi huo ni pamoja na kufanyika kwa mageuzi yanayotajwa kuwa ya kihistoria hadi mwaka 2008. Wakati huo kulitokea mabadiliko ya kuziondoa sheria zisizo rafiki katika maendeleo ya sekta ya nyumba.

Ndipo Shirika la Nyumba la Taifa, lilipewa mamlaka mapya ya kujiendesha kibiashara, lakini bila kusahau jukumu lake la msingi. Hatua hizi ziliweka msingi wa kuboresha huduma za makazi kwa Watanzania. Hata hivyo, katika kipindi cha uongozi wa Rais Dk. Samia, kasi ya utekelezaji wa miradi ya nyumba imeongezeka kwa kiwango cha kipekee.

Ukuaji Mapato NHC

Sera imara za Serikali ya Awamu ya Sita, zimewezesha ukuaji wa NHC, ambapo sasa ankara za kodi ya nyumba zimepanda kutoka shilingi 7.5 bilioni mwaka 2021 hadi kufikia shilingi 9.4 bilioni. Makusanyo ya kodi hiyo yamefikia zaidi ya asilimia 100. 

Mwaka 2021, NHC lilikuwa na maeneo yasiyopangishwa yanayofikia nyumba 700, lakini sasa maeneo hayo yameshapangishwa kwa asilimia 80. Hii ni kutokana na kuimarika kwa uchumi na biashara za Watanzania.

Upande wa madeni, NHC imefanikiwa kukusanya madeni yake, ambapo katika kipindi miaka minne zimekusanywa Shillingi 8.3 bilioni. 

Mbali na hayo, NHC pia imeongeza mauzo ya nyumba mpya, huku takwimu zikionyesha katika Mradi wa Kawe pekee nyumba zote 560 zimeshauzwa kabla mradi kukamilika.

Hali hiyo inatajwa kutokana na kipato cha wananchi kuimarika wakiwemo wapangaji wa nyumba na majengo ya NHC kote nchini.

Thamani rasilimali NHC yaimarika

Hadi kufikia Juni 2024 kwa hesabu zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), thamani ya rasilimali za NHC imeimarika na kufikia Shilingi 5.47 trilioni, ikilinganishwa na mwaka 2021 ambao zilikuwa Shilingi 5.04 trillioni. 

Ukuaji huo unaelezwa ni kutokana na kuongezeka kwa milki za Shirika ukichagiwa na kukamilika nyumba mpya na umiliki wa maeneo mbalimbali, ikiwemo NHC kufanikiwa kununua ardhi na majengo katika eneo la Urafiki, Dar es Salaam, yaliyokuwa yakimilikiwa awali na Kampuni ya Tanzania-China Friendship Textile Mills Co (Urafiki). 

Ushirikiano na Sekta ya Fedha 

Maofisa Mikopo kutoka Benki tofauti saba wakiwa katika ziara, kutembelea nyumba za makazi za Medeli Dodoma,  walifanya ziara hiyo ili kupata uelewa kuhusu nyumba hizo zilivyo na ikiwa pia  ni sehemu ya ushirikiano wa taasisi hizo na NHC.

Kupitia ushirikiano na benki zaidi ya 22, NHC limewezesha wananchi kupata mikopo ya nyumba ya muda mrefu. Sera ya ubia iliyohuishwa mwaka 2022 pia imefungua milango kwa sekta binafsi kushiriki katika miradi ya nyumba yenye thamani ya Shilingi 191 bilioni.

Miradi Awamu ya Sita

Katika kipindi hicho cha Awamu ya Sita madarakani, NHC imekamilisha miradi mikubwa ya nyumba za makazi. Miradi hiyo ni pamoja na; Mradi wa vyumba 887 za makazi katika eneo la Iyumbu na Chamwino, mkoani Dodoma.

Miradi hiyo imejengwa eneo la Iyumbu (303) na Chamwino (101) Jijini Dodoma, nyumba nyingine mpya 68 ujenzi unaendelea eneo la Iyumbu uliofikia asilimia 90; Pia kuna  na ujenzi wa nyumba 521 za makazi na biashara katika maeneo ya Dar es Salaam; Medeli Dodoma na Mtukula-Kagera. 

Kwa mujibu wa takwimu za shirika hilo, tangu lilipoanzishwa hadi sasa, limefanikiwa kujenga nyumba 30,000 za makazi, huku likiendelea kujenga nyumba za kuuza nyumba na kupangishwa.              Ikumbukwe kuwa katika Mwaka 2015, NHC lilianzisha Mpango Mkakati wa Miaka 10 (2015/16 – 2024/25), uliolenga kujenga nyumba 10,000 na kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi. Katika kipindi cha Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, NHC imekamilisha miradi mikubwa ya nyumba za makazi. 

Miradi miwili mikubwa Awamu ya Sita

Ndani ya kipindi hicho, NHC lilipanga kukamilisha miradi mikubwa ambayo ilisimama tangu mwaka 2018, ambapo Rais Dk. Samia alipoingia madarakani, aliinusuru hivyo pia kuliruhusu Shirika la Nyumba la Taifa kwa kuliwezesha kukopa fedha za kuikamilisha miradi hiyo ya kimkakati. 

Kawe 711

Sehemu ya Mradi wa Kawe unaoendelea kujengwa 

Januari mwaka 2024, Mkandarasi ambaye ni Kampuni ya Estim Construction Company Limited ilirejea kazini na ujenzi wa mradi wa nyumba 422 pamoja na sehemu za biashara sasa unaendelea katika mradi wa Kawe 711, wenye thamani ya Shilingi 169 bilioni, ambao sasa ujenzi wake umefikia asilimia 50, ukitarajiwa kukamilika Aprili 2026.

‘Samia Housing Scheme’

Sehemu ya Mradi wa Samia Housing Scheme

Katika kutambua mchango wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuendeleza sekta ya nyumba tangu alipoingia madarakani, NHC ilibuni mradi wa nyumba 5,000 uliopewa jina la Samia Housing Scheme, ulioleta matumaini mapya kwa wananchi. 

Mradi huo unatekelezwa eneo la Kawe, Dar es Salaam, ambapo ujenzi wa nyumba 560 ulikwishaanza ukifikia asilimia 80 na unatarajiwa kukamilika Februari mwaka huu 2025.

Samia Housing Scheme utawezesha ujenzi wa nyumba 5,000 katika maeneo mbalimbali nchini zote zikigharimu Shilingi 466 bilioni. 

Tayari NHC imekamilisha mauzo ya nyumba 560 eneo la Kawe huku shirika hilo likijiandaa kuanza awamu ya pili ya mradi huo na Medeli Dodoma  (100). 

Morocco Square

Jengo la Morocco Square linavyoonekana 

Miaka minne ya uongozi wa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, Shirika la Nyumba la Taifa pia limefanikiwa kukamilisha mradi wa Morocco Square kwa asilimia 100. 

NHC inaendelea kuuza na kupangisha, ambapo maeneo ya maduka (Retail Mall) yamepangishwa kwa asilimia 100 huku asilimia 95 ya Ofisi zikipangishwa pia. 

Kwenye jengo lenye nyumba za makazi 100, eneo hilo tayari nyumba 85 zimeuzwa, huku mauzo ya nyumba zilizobakia yakiendelea na upangishaji wa hoteli yenye vyumba 81 umefanyika kwa asilimia 100 na hoteli hiyo ikiwa tayari imeanza kutoa huduma.

Kimsingi miradi ya Kawe 711 na Morocco Square inaenda kuboresha mandhari ya Jiji la Dar es Salaam, kuboresha na kukuza uchumi wa Tanzania.

Majengo ya kimkakati, ofisi na biashara 

2H Commercial Building – Morogoro – Ujenzi wa jengo hili la biashara umefikia asilimia 40.

Masasi Plaza - Masasi Mtwara - Ujenzi wa jengo la biashara katika mji wa Masasi upo asilimia 40. 

Kahama - Utekelezaji wa mradi huu umefikia asilimia 70 na unatarajiwa kukamilika Januari 2025. 

Mradi wa ujenzi unaoendelea Kahama

Mtanda Lindi- Ujenzi wa jengo la biashara Mtanda Commercial Building-Lindi umefikia asilimia 30.

Mradi  unaoendelea Lindi

Usimamizi miradi na usanifu

Mhandisi Mary Kaaya wa NHC, ambaye ni Msimamizi wa ujenzi wa Ofisi ya Wizara ya Nishati, (Mbele), akiwaonyesha Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa NHC, waliomzunguka ramani na hatua za ujenzi wa jengo hilo wakati bodi hiyo ilipotembelea na kukagua mradi huo Desemba 11,2024 Mtumba, Dodoma

Miaka minne ya utawala wa Awamu ya Sita, chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, inashuhudia NHC likiwa msimamizi na mshauri elekezi wa miradi mbalimbali nchini.

Miradi hiyo ni pamoja na usimamizi wa ujenzi Soko Kuu la Kariakoo ulio na thamani ya Shilingi bilioni 28 na ambao umeshakamilika kwa wastani wa asilimia 97. Mradi huu ulitarajiwa kukamilika Januari 2025.

Mradi wa pili unaosimamiwa na NHC ni usanifu na usimamizi wa jengo la Ofisi ya Wizara ya Fedha na Mipango eneo la Mtumba umekamilika na ujenzi umefikia asilimia 85, mjenzi akiwa ni Kampuni ya Estim Construction. 

NHC pia inasimamia wa ujenzi wa jengo la Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, awamu ya pili ujenzi umefikia asilimia 88, huku mjenzi akiwa ni Suma JKT;

Mradi wa nne ambao pia unasimamiwa na NHC ni usanifu na ujenzi wa jengo la Soko la Madini (Tanzanite) eneo la Mirerani Manyara.Tayari usanifu umekamilika na ujenzi umefikia asilimia 86. 

Sera ya Ubia

Baada ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kuingia madarakani, alifungua milango ya uwekezaji nchini na kuhimiza ushirikiano wa sekta binafsi na sekta ya umma lengo likiwa kuharakisha ujenzi wa uchumi wa Tanzania. 

Katika kuenda sanjari na maono ya Rais, NHC liliboresha sera yake ya ubia, ambayo ilizinduliwa Waziri Mkuu Novemba 16, 2022. 

Mwaka 2024, NHC liliidhinisha na kusaini mikataba ya miradi 21 ya ubia iliyo na thamani ya Shilingi 179 bilioni. 

Mojawapo ya miradi ya ubia unaoendelea kujengwa eneo la Kariakoo

Tayari NHC imepata vibali kwa miradi 18 vya ujenzi na umeanza kutekelezwa ukifikia hatua mbalimbali, huku miradi mingine mitatu ikiwa imeshapata vibali hivi karibuni na itaanza kutekelezwa. 

NHC inaendelea kusimamia miradi ya ubia mipya na ile ya zamani, ambayo awali ilisimama ikiwa maeneo mbalimbali nchini na tayari miradi minne iliyosimama awali imesharejeshwa NHC ili ikamilishwe. Shirika la Nyumba la Taifa linalenga kuhakikisha miradi yote ya ubia isiyokamilika inarejeshwa na mazungumzo na wabia wenye miradi hiyo yanaendelea. 

NHC inaendelea na upembuzi, pia tathimini ya kina kwa waombaji wapya kwa miradi katika maeneo kadhaa yanayohitaji kuendelezwa, ambapo sasa ipo kwenye hatua ya kupata idhini ya kuendeleza viwanja takriban 80 nchi nzima.

Shirika la Nyumba la Taifa limefanya mageuzi makubwa katika kushirikiana na sekta binafsi kujenga majengo ya kisasa ya makazi na biashara likipendezesha mandhari ya miji yetu. Mfano, eneo la Kariakoo lililokuwa na wapangaji 172, ambao nyumba zao zimevunjwa na kuendelezwa, sasa lina zaidi ya nyumba 2,100 za makazi na biashara. 

Miradi ya ukandarasi

Kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, kimeshuhudia NHC ikipewa miradi mbalimbali ya kimkakati ya ukandarasi, iliyo na thamani ya Shilingi 186 bilioni iliyokamilika au ipo hatua za mwisho za utekelezaji, eneo la Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma ikiwamo ujenzi wa majengo ya Ofisi Nane za Wizara uliofikia asilimia 90.

Sehemu ya majengo ya Mradi wa Ofisi Nane za Serikali unaotekelezwa na NHC, Mji wa Serikali, Mtumba Dodoma.
NHC imetekeleza miradi mingine katika Awamu ya Sita ikiwemo ujenzi wa Jengo la Shule ya Uchumi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, uliofikia asilimia 80 kwa gharama ya Shilingi 9.7 bilioni.
Ujenzi wa jengo la ofisi pamoja na uzio wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Temeke Dar es Salaam ambao sasa umefikia asilimia 40 na ujenzi wa ghala la chakula la Halmashauri ya Masasi Vijijiniambao umemilika.

Ujenzi wa Hospitali za Kanda ya Kusini (Mitengo) na Hospitali ya Kanda ya Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Musoma, Mara uliokwishakamilika pamoja na ukamilishaji wa Jengo la Kitengo cha Moyo cha Jakaya Kikwete ambayo nayo imekamilika kwa asilimia 100. 

Shirika pia limejenga majengo mawili ikiwemo ofisi na miundombinu kwa ajili ya tanuru (incinerator) la Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) imekamilika jijini Dodoma, pia linajenga jengo la Tanzanite Mererani, Mkoa wa Manyara ambao upo asilimia 86.

Katika kipindi hicho, NHC inakamilisha pia ujenzi wa miradi 17 yenye majengo 44 ya Wakala wa Misitu Tanzania-TFS kwa thamani ya Shilingi 12.96 bilioni huku pia likitekeleza ujenzi wa jengo la Ofisi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) jijini Dodoma uliofikia asilimia 34.

Matengenezo 

NHC inakamilisha ukarabati wa majengo katika mikoa mbalimbali ya shirika, unaojumuisha ujenzi wa mifumo ya maji takana kupaka rangi.  Tangu mwaka 2023 bajeti ya Shilingi 7 bilioni imekuwa ikitengwa kila mwaka kwa ajili ya ukarabati wa nyumba zake pote nchini, hali inayoelezwa kuwezekana kwa kilichotajwa ni kuimarika kwa uwekezaji na mapato ya Shirikala Nyumba la Taifa.

Miradi inayoanza  

Miradi mbalimbali inaendelea kutekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa kwa mafanikio makubwa. Ndani ya NHC kwa sasa kuna miradi inayokaribia kuanza, ukiwamo wa Samia Housing Scheme Kawe Awamu ya 2 na Kijichi Jijini Dar es Salaam, Singida 2F mkoani Singida, Kashozi Business Center, Bukoba Mjini huku miradi mingine ikiwa ni Mt. Meru Plaza eneo la Kibla jijini Arusha, Mkwakwani Plaza Tanga, Juwata Plaza Morogoro, Medeli Awamu ya 3 Dodoma na Tabora Commercial complex. 

Miradi mingine ni Mpwapwa Flats Dodoma, Ilala Breweries Retail Shops, Iringa ICC na Mtwara Warehouse. 

Mustakabali wa NHC

Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Ahmad Abdallah akionyesha mkono, ishara inayoweza kutafsiriwa ni uelekeo wa uhakika wa shirika hilo kutekeleza majukumu yake. 

NHC linaendelea kupanua wigo wa shughuli zake kwa kutumia teknolojia za kisasa na utaalamu wa ndani huku miaka ijayolikitarajia kuendelea kuanzisha miradi mipya ya makazi, kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, bila kuliacha kando Shirika la Nyumba Zanzibar (ZHC), ujenzi wa vitega Uchumi, kutekeleza miradi ya ukandarasi na kutoa ushauri wa kitaalamu kwa miradi mbalimbali nchini pamoja na kutekeleza sera ya ubia.

Tunaweza kusema kwamba miaka minne ya uongozi wa Dk. Samia Suluhu Hassan, Shirika la Nyumba la Taifa, limepiga hatua kubwa katika kuboresha makazi na sekta ya nyumba nchini. Hatua hiyo inadhihirisha dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuimarisha maisha ya Watanzania kwa kuhakikisha kila mmoja anapata haki ya makazi bora. Kwa mipango madhubuti, NHC itaendelea kuwa mwanga wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini Tanzania.


'Fuatilieni vitambulisho vyenu vya taifa'

 Hussein Ndubikile,daimatznews@gmail.com 

Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo amewahimiza wananchi  kufuatilia vitambulisho vyao vya Taifa mara baada ya kujisajili ili kuepuka changamoto zinazojitokeza wanapohitaji huduma muhimu za kijamii.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), James Kaji ,akizungumza mbele ya wanahabari.

Sillo amezungumza hayo baada ya kutembelea Ofisi za Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na kuzungumza na watumishi wa taasisi hiyo jijini Dar es Salaam,Januari 13,2025.

Naibu Waziri Sillo, ameeleza kuwa vitambulisho zaidi ya milioni 20 tayari vimetengenezwa na kupelekwa Ofisi husika lakini bado kuna changamoto ya baadhi ya watu kushindwa kufuatilia vitambulisho hivyo kwa wakati

Kadhalika Naibu Waziri alimpongeza Mkurugenzi wa NIDA na watumishi hao kwa kazi kubwa wanayoifanya  kuhakikisha huduma ya vitambulisho inawafikia wananchi pamoja na ongezeko la uzalishaji wa vitambulisho hivyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) James Kaji amesema kuwa mamlaka hiyo imeanzisha mfumo wa kutuma jumbe za simu kwa wananchi ili kurahisisha upatikanaji wa vitambulisho ambapo tangu walipoanza tuma ujumbe wa simu ndani ya saa 24 pekee  vitambulisho zaidi ya 400,000 tayari vimechukuliwa.

Jamii ishirikiane kukomesha haya-ACT

 Hussein Ndubikile, daimatznews@gmail.com

Mwenyekiti  wa Ngome ya Vijana ya Chama cha ACT Wazalendo, Abdul Nondo amesema ni muhimu jamii kushirikiana bila kujali itikadi zao  ili kukomesha vitendo vya utekaji vilivyoshamiri nchini.
Abdul Nondo


Nondo amesema ili kukomesha vitendo vya utekaji ni vyema pia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, likafanya mabadiliko ya sheria kwa Askari wa Jeshi la Polisi, kuvaa sare anapokwenda kumkamata mtuhumiwa ili kuondoa taharuki.

"Tofauti na hilo ni vema sheria nayo ikasema kwamba sheria ikasema askari anatakiwa ajitambulishe na kueleza kosa la mtuhumiwa kabla ya kumkamata na aeleze anampeleka kituo gani cha Polisi ili kuwapa urahisi ndugu, jamaa kuweza kumfuatilia.

Ameyasema hayo Jijini Dar es Salaam Januari 13,2025 wakati akizungumza na wanahabari kuhusu mazingira ya kutekwa kwake na hofu aliyonayo baada ya kuvunja masharti aliyopewa  na waliomteka wakati wakimwachia, akiamini kwamba wanaweza kumteka tena na pengine kumuua.

“Mwaka 2023, Bunge lilifanya mabadiliko na kupitisha sheria kwa mtuhumiwa kuweza kukamatwa na askari asiyevaa sare, jambo ambalo kwa sasa inaonekana kutumika vibaya, hivyo nadhani huu ndio muda wa kuifanyia mabadiliko tena ili iseme askari anapokwenda kumkamata mtu ni lazima avae sare na ajitambulishe na aseme anampeleka kituo gani,” amesema.

Nondo amesema kwamba vitendo vya utekaji vinavyoonekana kuanza kushika kasi visifumbiwe macho, kwani vinachafua sura ya nchi na kusisitiza uchunguzi ufanyike kwa matukio ambayo yameripotiwa na taarifa za uchunguzi zitolewe na isifanywe dhiaka.

Ameongeza kuwa kama havitadhibitiwa mapema vinaweza kuonekana siku zijazo kama utamaduni na inaweza kusababisha makundi ya kiharifu kuchukua mwanya huo kutimiza malengo yao na kuja kuyadhibiti inaweza kuwa ni kazi kubwa na kusisitiza muda bado hupo ya kufanyia kazi kwani amani ikivurugika haitoangalia chama ama mtu.

HOFU TENA

Amesema kuwa ni jukumu la kila mwananchi kupaza sauti ya kulinda amani, akieleza kwamba kwa sasa anaishi kwa hofu ya kutekwa tena, baada ya kuvunja masharti yote ambayo amepewa na watu waliomteka Desemba Mosi, mwaka jana katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli, Mbezi jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Nondo, alitekwa na watu hao wasiojulikana muda mfupi baada ya kushuka kwenye basi akitokea mkoani Kigoma na kutelekezwa kwenye ufukwe wa Coco akiwa na hali mbaya na akasaidiwa na waendesha bodaboda kufikishwa katika ofisi za chama hicho Magomeni, Dar es Salaam.

Nondo ameeleza kwamba wakati anaachiwa na watekaji hao, walimtaka atekeleze masharti kadhaa yatakayomfanya kuwa huru na hasitekwe tena siku sijazo, ambayo anadai tayari ameshayavunja yote hali inayosababisha kuwa na hofu ya kutekwa kwa mara nyingine na pengine kuuawa.

“Wakati wananiachia waliambia nisiongee na vyombo vya habari jambo ambalo tayari nimelivunja, pili waliniambia baada ya pale niende nyumbani jambo ambalo nimefanya kinyume nao, tatu waliniambia nifunge mdomo nalo sijatekeleza, naaminmi wanaweza kufanya chochote hivyo suala la ulinzi wangu liko juu yangu na siwezi kutembea na walinzi ila chama kinanilinda, Mungu ananilinda,” amesema

Kwa mujibu wa Nondo, hawezi kukaa kimya kwa kuwa yeye ni kiongozi wa Ngome ya Vijana, hivyo anawajibika kusema na hatojificha, ikitokea ametekwa tena ama kuuawa itakuwa wamemtanguliza tu kwa maana kila mwanadamu atapitia kifo.

Amesisitiza kwamba hao watekaji wanaweza kumteka yeyote, hivyo wasipodhibitiwa siku za usoni yanaweza kuonekana ya kawaida hali itakayoweza kusababisha amani ambayo ni tunu ya taifa ikatoweka na kuirejesha ikawa ni kazi ngumu.

Pia ametolea mfano taifa la Mali, akidai kwamba kwa sasa liko katika wakati mgumu kudhibiti vitendo vya utekaji ambavyo vilianza kama mchezo na kusababisha makundi ya kigaidi kuingia na sasa teka wageni na kuomba fedha ili wawaachie.

“Kwanza Tanzania, sipendi nchi yangu ifikie huko, kazi kubwa imefanyika kuifanya nchi kuwa tulivu na kusababisha watalii kumiminika kwa wingi na pato la taifa kuongezeka, hivyo wananchi tupaze sauti kudhibiti hali hii kwa maslahi ya taifa,” amesema.


Mahakama yamwonya mtoto wa Mbowe kwa kutofika kortini

-Yamtaka kulipa madai ya wanahabari

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

MAHAKAMA Kuu Divisheni ya Kazi imemuonya Mkurugenzi wa Gazeti la Tanzania Daima, Dudley Mbowe kwa kutofika mahakamani tangu shauri la madai ya malimbikizo ya misharaha ya waandishi wa habari 10 lilipofunguliwa mwanzoni mwa mwaka jana na kumuamuru kulipa fedha hizo.

Dudley Mbowe, Mkurugenzi wa Tanzania Daima

Dudley ambaye ni mtoto wa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amepewa amri hiyo leo Januari 14,2025 mbele ya Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Mary Mrio wakati shauri hilo la madai lilipokuwa likitajwa,ambapo ametakiwa kulipa kabla ya Januari 31,2025.

Msajili Mrio amesema shauri hilo limwtajwa leo kwa ajili ya kuangalia maombi ya waandishi wa habari ya kumkamata Dudley na kumtupa gerezani kama mfungwa wa kiraia kwa kushindwa kulipa malimbikizo ya mishahara yao baada ya kushinda tuzo mahakamani.

Hata hivyo, Mrio amesema maombi hayo hayajawasilishwa ambapo amemuru yawasilishwe mahakamani ndani ya siku saba kwa ajili ya kupangiwa Jaji wa kuyasikiliza.

Katika majibu yake mbele ya Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Wakili Samadani Mngumi anayemwakilisha Dudley, amedai kuwa hajazumza

na mteja wake zaidi ya kupokea maelekezo ya kufika mahakamani kuomba udhuru hadi Januari 28 ili aweze kufika.

Msajili Mrio alihoji kama Dudley atafika mahakamani hapo siku hiyo kulipa deni au kwa ajili mazungumzo huku akieleza kwamba licha ya kuitwa mahakamani tangu kesi hiyo ilipofunguliwa mwanzoni mwa mwaka 2024, Mkurugenzi huyo wa Tanzania Daima hajawahi kufika.

"Mteja wako ameitwa mara kadhaa namahakama hii, lakini hajawahi kufika. Simjui, hata sijawahi kumuona. Sasa, afike mahakamani akiwa amelipa,"amesema Mrio kwa msisitizo.

Shauri hilo limeahirishwa hadi Januari 31 mwaka huu kwa ajili ya kusikilizwa maombi ya kumkamata Mkurugenzi huyo, ambayo yanatakiwa kuwa yamewasilishwa ndani ya siku saba kuanzia leo.

Awali, Mahakama ilitoa amri ya waandishi hao kulipwa baada ya kupitia hoja za washinda tuzo katika Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) Julai 2023.

Shauri hilo namba 28461 la mwaka 2023, wadai Maregesi Paul na wenzake tisa dhidi ya Mkurugenzi wa Gazeti la Tanzania Daima, Dudley Mbowe.

Walalamikaji hao walipata tuzo Julai 17 mwaka 2023 mbele ya Msuluhidhi wa CMA Ilala,  Bonasia Mollel.

Madai ya awali yalikuwa jumla ya Sh milioni 114.lakini baada ya kukaa mezani kwa majadiliano kwa Pamoja, kiwango hicho cha fedha kilishuka na kufikia Sh milioni 62.7.

Dudley alikubali kulipa fedha hizo kwa awamu tatu, Oktoba 30, Desemba 30 mwaka 2023 na awamu ya mwisho ilikuwa mwishoni Februari mwaka jana, lakini hakulipa.

Hata hivyo Dudley aliingia makubaliano ya kulipa malimbikizo hayo nje ya Mahakama Aprili hadi Mei mwaka jana, lakini pia hajafanya hivyo.



Ijumaa, 10 Januari 2025

'NHC yaokoa bilioni 24'

 

- DC aipongeza NHC 

- Ni baada ya kutembelaea Samia Housing Scheme

 Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

 Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule, amefanya ziara katika mradi wa kihistoria wa Samia Housing Scheme, unaotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Kawe, jijini Dar es Salaam na kupongeza jitihada za shirika hilo kuendeleza makazi bora nchini. 

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni,Saad Mtambule, Wa pili  kushoto, akiwa katika ziara kwenye mradi wa kihistoria wa Samia Housing Scheme, unaotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Kawe, jijini Dar es Salaam, Januari 8, 2025. Wengine pichani ni watendaji wa NHC na kutoka ofisi ya Mkuu huyo wa Wilaya.

Akizungumza katika ziara hiyo, Mtambule amesema kuwa iwapo mradi huo ungejengwa na mkandarasi wa nje, gharama zingefikia shilingi bilioni 72, hivyo ufanisi wa NHC ni jambo la kujivunia.

“Hivyo tunaweza kueleza kuwa, hapa NHC imeokoa takriban Shilingi bilioni 24, ambazo sasa zinatumika kwa shughuli nyingine za kuendele za makazi nchini,” amesema Mtambule na kuongeza:

“Nimevutiwa sana na mradi huu. Nyumba hizi nzuri na za kisasa zitadumu kwa muda mrefu na zimeongeza thamani ya Kinondoni. Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha miradi kama hii iliyokuwa imekwama sasa imekamilika.”

Meneja Habari na Uhusiano wa NHC, Muungano Saguya (Wa kwanza kulia),akitoa maelezo mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Saad Mtambule, (Wa pili kulia), alipofanya ziara katika mradi wa Samia Housing Scheme wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Kawe, jijini Dar es Salaam. 

Ziara hiyo  ya Januari 8,2025 ililenga kukagua maendeleo ya mradi huo mkubwa, wenye lengo la kuboresha makazi nchini na kuimarisha ustawi wa wakazi wa Kinondoni na Tanzania.

Mkuu huyo  wa wilaya amepongeza juhudi za NHC kuboresha mazingira ya kibiashara na huduma za jamii akisema: 

“Tunajivunia ushirikiano mzuri uliopo. Ninaomba ubunifu huu usiishie Kawe pekee, bali ufike maeneo mengine kama Bunju, Madale, na Mabwepande, ambapo pia kuna fursa za uwekezaji.” 

Amesema ubunifu na juhudi za NHC kuhakikisha nyumba zinajengwa kwa viwango bora na gharama nafuu ni za kupigiwa mfano na zinastahili kuungwa mkono.

Awali, Mtambule alipokea taarifa kutoka kwa Mhandisi Grace Msita wa NHC aliyeeleza kuwa mradi huo wa Samia Housing Scheme umelenga kujenga nyumba 5,000 kwa awamu. 

“Mradi unakadiriwa kugharimu shilingi bilioni 48 hadi ukapokamilika na tayari shilingi bilioni 30 zimetumika kufanikisha hatua zilizofikiwa sasa,” amesema Mhandisi Msita.

Ameongeza kuwa hatua za ujenzi zinaendelea kwa kasi kukamilisha mradi huo, huku kazi za sasa zikiwa ni kufunga milango, kuimarisha mifumo ya lifti na kupanga njia za watembea kwa miguu (pavement). 

Shirika la Nyumba la Taifa limemshukuru Mkuu huyo wa Wilaya kwa ushauri na ushirikiano anaotoa mara kwa mara, likisisitiza dhamira yake ya kuendelea kuboresha makazi na huduma kwa Watanzania.

Sehemu ya Mradi wa Samia Housing Scheme unavyoonekana pichani.

Mradi wa Samia Housing Scheme unaakisi dhamira ya Rais Samia na NHC ya kuhakikisha Watanzania wanapata makazi bora ya kisasa kwa gharama nafuu, huku ukichangia kukuza uchumi na kuboresha mazingira ya maisha.

Mkuu wa Wilaya amepongeza juhudi za NHC kwa kujenga nyumba zenye viwango vya juu kwa bei nafuu, huku akitoa wito wa kuendelea na kasi hiyo ili kuhakikisha azma ya kutoa makazi bora kwa Watanzania inatimia.

Mradi huo ni sehemu ya jitihada za kuimarisha makazi bora ya kisasa kwa ajili ya Watanzania, ukiashiria pia ukuaji wa sekta ya nyumba na ujenzi nchini.


'NHC yaokoa bilioni 24'

- DC aipongeza NHC 

- Ni baada ya kutembelaea Samia Housing Scheme

 Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

 Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule, amefanya ziara katika mradi wa kihistoria wa Samia Housing Scheme, unaotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Kawe, jijini Dar es Salaam na kupongeza jitihada za shirika hilo kuendeleza makazi bora nchini. 

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni,Saad Mtambule, Wa pili  kushoto, akiwa katika ziara kwenye mradi wa kihistoria wa Samia Housing Scheme, unaotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Kawe, jijini Dar es Salaam, Januari 8, 2025. Wengine pichani ni watendaji wa NHC na kutoka ofisi ya Mkuu huyo wa Wilaya.

Akizungumza katika ziara hiyo, Mtambule amesema kuwa iwapo mradi huo ungejengwa na mkandarasi wa nje, gharama zingefikia shilingi bilioni 72, hivyo ufanisi wa NHC ni jambo la kujivunia.

“Hivyo tunaweza kueleza kuwa, hapa NHC imeokoa takriban Shilingi bilioni 24, ambazo sasa zinatumika kwa shughuli nyingine za kuendele za makazi nchini,” amesema Mtambule na kuongeza:

“Nimevutiwa sana na mradi huu. Nyumba hizi nzuri na za kisasa zitadumu kwa muda mrefu na zimeongeza thamani ya Kinondoni. Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha miradi kama hii iliyokuwa imekwama sasa imekamilika.”

Meneja Habari na Uhusiano wa NHC, Muungano Saguya (Wa kwanza kulia),akitoa maelezo mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Saad Mtambule, (Wa pili kulia), alipofanya ziara katika mradi wa Samia Housing Scheme wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Kawe, jijini Dar es Salaam. 
Ziara hiyo  ya Januari 8,2025 ililenga kukagua maendeleo ya mradi huo mkubwa, wenye lengo la kuboresha makazi nchini na kuimarisha ustawi wa wakazi wa Kinondoni na Tanzania.

Mkuu huyo  wa wilaya amepongeza juhudi za NHC kuboresha mazingira ya kibiashara na huduma za jamii akisema: 

“Tunajivunia ushirikiano mzuri uliopo. Ninaomba ubunifu huu usiishie Kawe pekee, bali ufike maeneo mengine kama Bunju, Madale, na Mabwepande, ambapo pia kuna fursa za uwekezaji.” 

Amesema ubunifu na juhudi za NHC kuhakikisha nyumba zinajengwa kwa viwango bora na gharama nafuu ni za kupigiwa mfano na zinastahili kuungwa mkono.

Awali, Mtambule alipokea taarifa kutoka kwa Mhandisi Grace Msita wa NHC aliyeeleza kuwa mradi huo wa Samia Housing Scheme umelenga kujenga nyumba 5,000 kwa awamu. 

“Mradi unakadiriwa kugharimu shilingi bilioni 48 hadi ukapokamilika na tayari shilingi bilioni 30 zimetumika kufanikisha hatua zilizofikiwa sasa,” amesema Mhandisi Msita.

Ameongeza kuwa hatua za ujenzi zinaendelea kwa kasi kukamilisha mradi huo, huku kazi za sasa zikiwa ni kufunga milango, kuimarisha mifumo ya lifti na kupanga njia za watembea kwa miguu (pavement). 

Shirika la Nyumba la Taifa limemshukuru Mkuu huyo wa Wilaya kwa ushauri na ushirikiano anaotoa mara kwa mara, likisisitiza dhamira yake ya kuendelea kuboresha makazi na huduma kwa Watanzania.

Sehemu ya Mradi wa Samia Housing Scheme unavyoonekana pichani.

Mradi wa Samia Housing Scheme unaakisi dhamira ya Rais Samia na NHC ya kuhakikisha Watanzania wanapata makazi bora ya kisasa kwa gharama nafuu, huku ukichangia kukuza uchumi na kuboresha mazingira ya maisha.

Mkuu wa Wilaya amepongeza juhudi za NHC kwa kujenga nyumba zenye viwango vya juu kwa bei nafuu, huku akitoa wito wa kuendelea na kasi hiyo ili kuhakikisha azma ya kutoa makazi bora kwa Watanzania inatimia.

Mradi huo ni sehemu ya jitihada za kuimarisha makazi bora ya kisasa kwa ajili ya Watanzania, ukiashiria pia ukuaji wa sekta ya nyumba na ujenzi nchini.


Alhamisi, 9 Januari 2025

Baraza Kivuli ACT, lajipanga kusimamia uwajibikaji wa Serikali

Hussein  Ndubikile, daimatznews@gmail.com

Waziri Mkuu Kivuli wa Chama cha ACT Wazalendo, Isihaki Rashidi Mchinjita, amesema kuwa Baraza la Mawaziri Kivuli la chama hicho litautumia mwaka 2025 kwa kusimamia haki za wananchi, uwajibikaji wa Serikali na kupigania mageuzi ya kweli ya kidemokrasia.

Waziri Mkuu Kivuli wa Chama cha ACT Wazalendo,  Isihaki Rashidi Mchinjita akizungumza na wanahabari Januari 8,2025 Makao Makuu ya ACT, Magomeni Dar es Salaam,

Mchinjita amesema mwaka 2024 ulikuwa wa changamoto nyingi ikiwamo migogoro ya ardhi,  hali ya kiuchumi isiyorihisha, kuongezeka kwa matukio ya utekaji na mauaji, maafa ya mvua za Elnino na wananchi kukosa huduma bora akieleza kwamba mwaka 2025 haupaswi kuendelea na taswira ya mwaka jana..

Katika kusisitiza msimamo huo, amesema kuwa Watanzania wanapaswa kushirikiana na ACT Wazalendo kufanya maamuzi yatakayoleta mabadiliko katika kuimarisha maisha yao na kujenga taifa la wote.

Kauli hiyo ameitoa Januari 8, 2025 alipozungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya chama hicho, Magomeni, Dar es Salaam wakati akitoa tathmini ya mwaka 2024 na kuelezea mwelekeo wa baraza hilo kwa mwaka 2025.

“Mwaka 2025 ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu ni mwaka wa uamuzi. ACT Wazalendo tumejizatiti kuimarisha haki za kijamii, kupigania mageuzi ya demokrasia na maendeleo ya kiuchumi kwa maslahi ya wote.”

Waziri Mkuu huyo kivuli amesema mwaka 2024 ulikuwa na changamoto ya hali mbaya ya kiuchumi, ambapo deni la serikali lilifikia shilingi trilioni 93.7, hali aliyosema inaathari uwezo wa taifa kutoa huduma bora hata ajira  katika sekta muhimu ikiwamo afya na elimu  hivyo ugumu wa maisha kuongezeka.

“Ni jambo la aibu kuona wananchi wa kipato cha chini wakinyimwa huduma za afya kwa sababu hawawezi kumudu gharama afya ambazo ni haki, si bidhaa,” aliongeza.

Akizungumzia demokrasia, Mchinjita ameeleza hitaji la Tanzania kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi, akibainisha kuwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 umeonesha sura isiyofurahisha kuelekea mageuzi ya kweli.

“Ili tuwe na uchaguzi wa haki na uwazi mwaka 2025 ni lazima tuwe na Tume Huru ya Uchaguzi itakayohakikisha kila kura ya Mtanzania inaheshimiwa,” aliongeza.

Amehitimisha kwa kuahidi kuwa Baraza la Mawaziri Kivuli la ACT litaendelea kuwa sauti ya wananchi, huku ikisisitiza mshikamano wa kitaifa kupambana na changamoto zilizopo. 

DC Kinondoni ‘amteta’ Rais Samia NHC



    
   

Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Ahmad Abdallah


- Aipongeza NHC kwa ubunifu Morocco Square

- Atamani ‘Morocco Square’ nyingine Mabwepande

 Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule, amefanya ziara katika Mradi wa Morocco Square, unaotekelezwa na NHC 'akimteta’ Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumpongeza kutokana na kuongoza juhudi za kukwamua miradi mikubwa ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), iliyokuwa imekwama. 


Msimamizi wa Mradi wa Morocco Square kutoka NHC, Stanley Msofe akimuonesha Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni. Saad Mtambulike(aliyevaa suti), sehemu ya jengo hilo, wakati kiongozi huyo alipotembelea na kukagua jengo hilo. Wengine pichani ni Meneja Habari na Uhusiano waNHC, Muungano Saguya (wa pilikulia) na mtumishi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Wilaya  Kinondoni.

Mtambule pia amelipongeza shirika hilo kwa ubunifu ujenzi wa Morocco Square akisema anatamani ubunifu aliouona kwenye ujenzi wa jengo hilo upelekwe pia kwenye maeneo mengine ya wilaya hiyo yenye nafasi ya kujenga majengo ya uwekezaji ikiwamo Mabwepande.

Mtambule ameyasema hayo alipofanya ziara katika Mradi wa Morocco Square, unaotekelezwa na NHC katika eneo la Morocco, jijini Dar es Salaam Januari 8,2025 ili kukagua maendeleo ya mradi huo mkubwa unaolenga kuboresha makazi na kukuza mazingira ya kibiashara katika Wilaya ya Kinondoni. 

“Namshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuongoza juhudi za kukwamua miradi mikubwa iliyokuwa imekwama, ikiwemo Samia Housing Scheme na Kawe 711, ambayo sasa inaendelea kwa kasi na kufikia viwango vya juu,” amesema  Mtambule.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan akisisitiza jambo katika moja ya hotuba zake.

Ameeleza kuwa Mradi wa Morocco Square umekaribia kukamilika kwa asilimia kubwa, huku akielekeza hatua zilizobaki, ambazo ni asilimia 2 pekee, zikamilishwe haraka ili biashara zianze.

Mtambule amesifu na kupongeza ubunifi wa NHC waliouonyesha kwenye mradi huo na mingine wanayoitekeleza akishauri maeneo mengine pia yanufaike. 

 “Napongeza ubunifu wa NHC, nashauri ubunifu huu usiishie hapa Morocco pekee. Shirika liangalie pia maeneo mengine kama Bunju, Madale na Mabwepande, ambako kuna fursa nyingi za uwekezaji, ikiwemo uuzaji wa viwanja,” ameongeza.

Amepongeza pia juhudi za NHC kwa kuwekeza miradi mikubwa inayoongeza thamani ya maeneo na kuboresha maisha ya wakazi wa Kinondoni.

“Tunawashukuru kwa ubunifu katika ujenzi, hasa kwa miradi hii ambayo imeongeza thamani kubwa kwa maeneo yetu. Tuna kila sababu ya kuhakikisha kwamba biashara zinafanyika vizuri na huduma zinaendelea kusogezwa karibu na wananchi,” amehitimisha Mtambule.

Meneja Habari na Uhusiano wa NHC, Muungano Saguya (Aliyesimama), akitoa maelezo kwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule(Wa kwanza kushoto) kuhusu mradi wa Morocco Square. Wengine pichani ni watendaji wa NHC na wa ofisi ya Mkuu wa Wilaya huyo. 

Kwa upande wake, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), limemshukuru Mkuu huyo wa Wilaya kwa ushauri wake na ushirikiano anaouonyesha mara kwa mara.

NHC imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kuleta maendeleo kupitia miradi ya makazi bora na huduma zinazokidhi mahitaji ya Watanzania.

Mradi wa Morocco Square uliopo katika makutano ya Barabara za Mwai Kibaki, Ali Hassan Mwinyi na Ursino eneo la Regent Estate, wilayani  Kinondoni, unaendelea kuwa sehemu muhimu ya juhudi za NHC za kukuza uchumi wa maeneo ya mijini, kuboresha maisha ya wakazi na kuimarisha sekta ya ujenzi nchini.

Kupitia mradi huo wa kipekee, NHC imejenga majengo manne kwenye msingi mmoja,  jengo moja likiwa ni hoteli, la pili ofisi mbalimbali, jengo la tatu ni la biashara na la nne ni makaziya watu. 

Mradi  huo uliozinduliwa Novemba 23 mwaka 2024,  umejengwa kwa gharama ya Shilingi bilioni 137 ni alama mpya ya kazi nzuri zilizofanywa na NHC nchini likiwa na nyumba za makazi, ofisi, maeneo ya biashara na burudani yakiwa kwenye msingi wa jengo moja.

Sehemu ya jengo la Morocco Square inavyoonekana kwa nje.

 

 

Jumanne, 7 Januari 2025

Rais Samia azindua hoteli ya bil 109 Kisiwa cha Bawe

-Dk. Mwinyi akunjua makucha wawekezaji ‘uchwara’
 -Rais Samia aunga mkono wanyang'anywe visiwa
Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com Zanzibar; Rais Samia Suluhu Hassan amezindua hoteli kubwa ya kitalii Bawe Island the Cocoon Collection iliyopo katika Kisiwa cha Bawe Januari 7,2025, huku Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Mwinyi akitoa siku 90 kwa wawekezaji walioshindwa kuendeleza visiwa walivyovikodi kuvirejesha serikalini.
Rais Samia Suluhu Hassan (Wa pili kulia), akisisitiza jambo, wakati alipotembelea kujionea vyumba vya kulala wageni katika Hoteli ya Bawe, kisiwani Bawe aliyoizindua Januari 7,2024 mjini Zanzibar.Wa nne kulia ni Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, aliyesimama mbele ni mwekezaji wa mradi huo.

Katika tukio hilo la kihistoria, ambalo ni sehemu ya sherehe za maadhimisho ya miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Januari 12 mwaka 1964, Rais Samia amezindua hoteli hiyo akiwa na mwenyeji wake Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Uzinduzi wa hoteli hiyo ni sehemu ya mikakati ya Dk.Mwinyi kuinua Uchumi wa Zanzibar kwa kuvutia wawekezaji, ambapo uwekezaji wa Bawe Hotel umefanyika chini ya mpango ukodishwaji ardhi ya visiwa vidogo chini ya Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) na tayari visiwa16 kati ya 50 vimewekezwa.

Akiungumza katika hafla hiyo kwenye kisiwa hicho kilichopo umbali wa kilometa kumi kutoka Mji Mkongwe, Rais Samia amesema Dk. Mwinyi aliona mbali kwa kufikiria na kutekeleza ukodishaji wa visiwa vidogo.

“Dk Mwinyi aliona mbali kukoisha visiwa, waswahili husema,uchumi tuliukalia, leo ajira zaidi ya 400 zimezalishwa. Ujenzi na uwekezaji katika visiwa vidogo utakuza jina la Zanzibar, kila jambo lina mambo yake,” amesema Dk Samia na kuongeza: 

“Uwekezaji huu hapa Bawe wa zaidi ya Dola za Marekani 42 milioni (Shilingi bilioni 109.2) ni ishara ya wawekezaji kuridhika na mazingira pia utawala.” 

Rais Samia amesema lengo na dhamira ya mapinduzi ni kuwaletea neema wananchi wa Zanzibar na kwamba hata Ilani ya Uchaguzi wa CCM imeeleza, yapo mambo mengi ya kufanya, ikiwamo Uchumi wa Zanibar kuwa endelevu.

“Mawapongeza ZIPA kusimamia uwekezaji, msiingizwe mtegoni, kazi iendelee, yajayo yanafurahisha. Serikali imedhamiria kuongeza uwekezaji bandarini katika Bandari ya Malindi, Maruhubi, Fumba, Mkoani, Manga Pwani na Mpigaduri,pia ujenzi wa Bandari Wete na kubwa zaidi Kizimkazi; 

Hapa Dk.Mwinyi umemaliza, ntakupa kila ushirikiano, Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani Karume unaendelea kuboreshwa, Pemba sasa ndege zinarukahata usiku, ila tutafanya makubwa zaidi. 

Naipongeza ZIPA kwa usimamizi madhubuti, tuendelee kuelimisha wananchi uwekezaji katika visiwa kwani ni jambo jipya kwao.” 

Rais Samia amesema jeuri ya leo ya Zanzibar katika maeneleo inatokana na mchango wa Serikali ya Mapinduzi awamu zote,akihimiza wananchi kuendelea kuyaenzi mapinduzi.

Awali, akimkaribisha Rais Samia, Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi amesema:

“ …Leo niseme hadharani kwamba Rais Samia amekuwa msaada mkubwa kwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika mambo yetu yote. Namshukuru na kumpongeza kwa dhati na kwa kweli tupo pamoja naye katika kuijenga nchi yetu kwa pande zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 
Leo ni historia ya pekee, tumeonyesha faida ya maeneo ya visiwa, awali yalisemwa mengi.” 

Dk. Mwinyi amesema Serikali yake kupitia ZIPA imeshatoa visiwa 16 kwa wawekezaji ili viwekezwe na kwamba Bawe ndio mradi wa kwanza kuzinduliwa ikiwa na kiwango cha kimataifa, akiwashukuru wawekezaji kwa kutimiza waliloahidi ikiwamo kuwasaidia wavuvi waliokuwa wakitumia kisiwa hicho kwa kuwajengea jiko la kisasa na kununua samaki wote wanaowavua. 

Amewaonya wawekezaji waliokodishwa visiwa bila kuviendeleza kwa muda mrefu kuwa vitarejeshwa serikalini wsipofanya lolote ndani ya siku 90. 

“…Nataka leo nitoe tamko kwa wale wote ambao tumewakodisha visiwa, muda umekuwa mrefu, hawajaanza kujenga, Serikali inawapa miezi mitatu kuanzia sasa. Hapo tutakapoona hawaendelezi tutavirudisha serikalini,” amesema.
Rais Samia Suluhu Hassan katika hotuba yake ya ufunguzi wa hoteli hiyo ameunga mkono kauli ya Dk,Mwinyi kuhusu kuwanyang’anya wawekezaji wasiondeleza visiwa hivyo akisema; 
“Nami naungana na Rais wa Zanzibar kwamba wale wote waliopewa visiwa nahawajafanya kazi, basi miezi mitatu,baada yah apo Mheshimiwa Rais usirudi nyuma.”

Akizungumzia CCM, Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi amesema Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho ya mwaka 2020 iliwataka kuongeza vitanda kwenye hoteli za kitalii kutoka 10,000 hadi 15,000, lakini hadi 2024, mwaka mmoja kabla muda wa utekelezaji kuisha wameshaongeza kufikia 15,132. 

Dk. Mwinyi ametaja faida kubwa tatu za uwekeaji ikiwamo kukukua kwa soko la bidhaa za wazanzibari, kuongezeka watalii na ajira, akiwataka Wazanzibar kuwa na weledi na kusoma ili waweze kufanya kazi kwenye hoteli hizo za kitalii. 

Amedokeza kuwa nchi ya Italia kupitia balozi wake nchini imeeleza kutenga kiasi cha Euro 5000 kwa ajili ya kuwajengea uwezo Wazanzibar waweze kuajiriwa kwenye hoteli hizo, akiishukuru Italia kwa msaada huo.