Hot Posts

6/recent/ticker-posts

Mahakama yamwonya mtoto wa Mbowe kwa kutofika kortini

-Yamtaka kulipa madai ya wanahabari

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

MAHAKAMA Kuu Divisheni ya Kazi imemuonya Mkurugenzi wa Gazeti la Tanzania Daima, Dudley Mbowe kwa kutofika mahakamani tangu shauri la madai ya malimbikizo ya misharaha ya waandishi wa habari 10 lilipofunguliwa mwanzoni mwa mwaka jana na kumuamuru kulipa fedha hizo.

Dudley Mbowe, Mkurugenzi wa Tanzania Daima

Dudley ambaye ni mtoto wa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amepewa amri hiyo leo Januari 14,2025 mbele ya Naibu Msajili wa Mahakama hiyo, Mary Mrio wakati shauri hilo la madai lilipokuwa likitajwa,ambapo ametakiwa kulipa kabla ya Januari 31,2025.

Msajili Mrio amesema shauri hilo limwtajwa leo kwa ajili ya kuangalia maombi ya waandishi wa habari ya kumkamata Dudley na kumtupa gerezani kama mfungwa wa kiraia kwa kushindwa kulipa malimbikizo ya mishahara yao baada ya kushinda tuzo mahakamani.

Hata hivyo, Mrio amesema maombi hayo hayajawasilishwa ambapo amemuru yawasilishwe mahakamani ndani ya siku saba kwa ajili ya kupangiwa Jaji wa kuyasikiliza.

Katika majibu yake mbele ya Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Wakili Samadani Mngumi anayemwakilisha Dudley, amedai kuwa hajazumza

na mteja wake zaidi ya kupokea maelekezo ya kufika mahakamani kuomba udhuru hadi Januari 28 ili aweze kufika.

Msajili Mrio alihoji kama Dudley atafika mahakamani hapo siku hiyo kulipa deni au kwa ajili mazungumzo huku akieleza kwamba licha ya kuitwa mahakamani tangu kesi hiyo ilipofunguliwa mwanzoni mwa mwaka 2024, Mkurugenzi huyo wa Tanzania Daima hajawahi kufika.

"Mteja wako ameitwa mara kadhaa namahakama hii, lakini hajawahi kufika. Simjui, hata sijawahi kumuona. Sasa, afike mahakamani akiwa amelipa,"amesema Mrio kwa msisitizo.

Shauri hilo limeahirishwa hadi Januari 31 mwaka huu kwa ajili ya kusikilizwa maombi ya kumkamata Mkurugenzi huyo, ambayo yanatakiwa kuwa yamewasilishwa ndani ya siku saba kuanzia leo.

Awali, Mahakama ilitoa amri ya waandishi hao kulipwa baada ya kupitia hoja za washinda tuzo katika Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) Julai 2023.

Shauri hilo namba 28461 la mwaka 2023, wadai Maregesi Paul na wenzake tisa dhidi ya Mkurugenzi wa Gazeti la Tanzania Daima, Dudley Mbowe.

Walalamikaji hao walipata tuzo Julai 17 mwaka 2023 mbele ya Msuluhidhi wa CMA Ilala,  Bonasia Mollel.

Madai ya awali yalikuwa jumla ya Sh milioni 114.lakini baada ya kukaa mezani kwa majadiliano kwa Pamoja, kiwango hicho cha fedha kilishuka na kufikia Sh milioni 62.7.

Dudley alikubali kulipa fedha hizo kwa awamu tatu, Oktoba 30, Desemba 30 mwaka 2023 na awamu ya mwisho ilikuwa mwishoni Februari mwaka jana, lakini hakulipa.

Hata hivyo Dudley aliingia makubaliano ya kulipa malimbikizo hayo nje ya Mahakama Aprili hadi Mei mwaka jana, lakini pia hajafanya hivyo.



Chapisha Maoni

0 Maoni