Ni mapema mno kusahau mbunge wako aliyebwagwa CCM
-CCM yawaambia wasikate tamaa, nafasi bado zipo nyingi
Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
Baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), kutangaza majina ya wanachama wake waliopita katika mchujo, hatua za awali kwenda kwenye kura za maoni majimboni, ukiacha tabasamu kwa waliopitishwa na kilio kwa ambao hawakuteuliwa, sasa ni wazi chama hicho tawala kimewabwaga baadhi ya wanachama wake waliokuwa wabunge kwenye Bunge linalomaliza muda wake, wakiwamo wabunge maarufu.
Hakika ni mapema mno kusahau mbunge wako aliyetia nia kuwania tena ubunge jina lake likakatwa, lakini ndivyo ilivyo kwani Julai 29,2025 Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, CPA Amos Makalla ametangaza majina ya watakaopigiwa kura ili kupata wagombea ubunge wa majimbo 272,bil kuwepo majina ya wabunge takriban 27 wanaomaliza kipindi cha kuwa madarakani.
Makalla ametaja wateule hao kutoka watia nia takriban 5,000 waliotia nia kuwania kuteuliwa na chama hicho tawala kuwania ubunge katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29 mwaka huu 2025, bila kuwemo majina 27 ya wabunge wake wanaomaliza muda wa ubunge, licha ya kuomba kuteuliwa kuwania tena ubunge.
Makalla amesema: "Uteuzi umefanywa kwa kuzingatia sifa, uwezo wa mgombea na mahitaji ya kisiasa ya majimbo husika."
Hata hivyo, chama hicho kimewasihi wanaCCM ambao majina yao hayakupitishwa kutokata tamaa bali waendelee kuiunga mkono CCM, kikieleza kuwa nafasi za kukitumikia bado ni nyingi.
Lakini, miongoni wa watia nia zaidi ya 5,000 CCM imepitisha jina moja hadi wanane katika kila jimbo kati ya majimbo 272 ambapo kwa hesabu ya haraka ya kila jimbo wamepitishwa wagombea wanane, waliopitishwa ni takriban watia nia 2176 huku wengine 2,824 wakiachwa, miongoni mwao ni wagombea 27 ambao ni wabunge maarufu wa Bunge linalomaliza muda wake.
Wabunge hao 27 walioachwa ni pamoja na Mrisho Mashaka Gambo wa Jimbo la Arusha Mjini, Emanuel Ole Shangai (Ngorongoro), Mohamed Lujuo Moni (Chemba), Nicodemus Maganga (Mbogwe) na Justine Nyamoga wa Kilolo.
Yumo pia January Makamba wa Jimbo la Bumbuli mkoani Tanga, Stephen Byabato(Bukoba Mjini), George Ndaisaba Ruhoro (Ngara), Zuberi Mohammed Kuchauka (Liwale) na Pauline Gekul(Babati Mjini).
Wamo pia Christopher Ole Sendeka (Simanjiro), Flatey Maasai (Mbulu Vijijin) na Vedastus Matayo Manyinyi (Musoma Mjini).
CCM pia imemwacha Mbunge wa Kisesa Luhaga Mpina, Godwin Kunambi (Mlimba) Geoffrey Mwambe (Masasi) na Cecil Mwambe (Ndanda)
Waziri wa zamani wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Anjelina Mabula kutoka Jimbo la Ilemela mkoani Mwanza, pia jina lake halikuteuliwa, akiwamo pia Mansour Shanif Hirani : (Kwimba) Hassan Zidadu Kungu (Tunduru Kaskazini) na Iddi Mpakate wa unduru Kusini.
Katika orodha ya wabunge ambao majina yao hayakuteuliwa kupigiwa kura za maoni yumo pia Iddi Kassim Iddi wa Jimbo la Msalala, George Mwenisongole (Mbozi) na Seif Hamisi Gulamali(Manonga).
Imewajumuisha pia Omar Shekilindi wa Jimbo la Lushoto, Alfred Kimea (Korogwe Mjini), Twaha Mpembenwe (Kibiti) na Turky wa Jimbo la Mpendae Zanzibar.
Mbali na hatua hiyo ya CCM kuwaacha wabunge wake hao, swali linabaki kuwa hatua hiyo ambayo bila shaka inaumiza wagombea hao na wengine waliokatwa, nini kitafuata baada ya kutafakari uamuzi huo wa chama chao.
Hata hivyo, uzoefu unaonyesha kwamba baada ya tukio hilo, baadhi ya wanasiasa hukimbilia vyama vingine kutafuta nafasi ya kuteuliwa na kuwania viti vya ubunge kupitia vyama vya upinzani na kugeuza kipindi hiki kuwa cha mavuno kwa vyama vya siasa vya upinzani.



Maoni
Chapisha Maoni