![]() |
Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Ahmad Abdallah |
- Aipongeza NHC kwa ubunifu Morocco Square
- Atamani ‘Morocco Square’ nyingine Mabwepande
Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule, amefanya ziara katika Mradi wa Morocco Square, unaotekelezwa na NHC 'akimteta’ Rais Samia Suluhu Hassan kwa kumpongeza kutokana na kuongoza juhudi za kukwamua miradi mikubwa ya Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), iliyokuwa imekwama.
Mtambule pia amelipongeza shirika hilo kwa ubunifu
ujenzi wa Morocco Square akisema anatamani ubunifu aliouona kwenye ujenzi wa
jengo hilo upelekwe pia kwenye maeneo mengine ya wilaya hiyo yenye nafasi ya kujenga
majengo ya uwekezaji ikiwamo Mabwepande.
Mtambule ameyasema hayo alipofanya ziara katika Mradi wa Morocco Square, unaotekelezwa na NHC katika eneo la Morocco, jijini Dar es Salaam Januari 8,2025 ili kukagua maendeleo ya mradi huo mkubwa unaolenga kuboresha makazi na kukuza mazingira ya kibiashara katika Wilaya ya Kinondoni.
“Namshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuongoza juhudi za kukwamua miradi mikubwa iliyokuwa imekwama, ikiwemo Samia Housing Scheme na Kawe 711, ambayo sasa inaendelea kwa kasi na kufikia viwango vya juu,” amesema Mtambule.
![]() |
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan akisisitiza jambo katika moja ya hotuba zake. |
Ameeleza kuwa Mradi wa Morocco Square umekaribia kukamilika kwa asilimia kubwa, huku akielekeza hatua zilizobaki, ambazo ni asilimia 2 pekee, zikamilishwe haraka ili biashara zianze.
Mtambule amesifu na kupongeza ubunifi wa NHC waliouonyesha kwenye mradi huo na mingine wanayoitekeleza akishauri maeneo mengine pia yanufaike.
“Napongeza
ubunifu wa NHC, nashauri ubunifu huu usiishie hapa Morocco pekee. Shirika
liangalie pia maeneo mengine kama Bunju, Madale na Mabwepande, ambako kuna
fursa nyingi za uwekezaji, ikiwemo uuzaji wa viwanja,” ameongeza.
Amepongeza pia juhudi za NHC kwa kuwekeza miradi mikubwa inayoongeza thamani ya maeneo na kuboresha maisha ya wakazi wa Kinondoni.
“Tunawashukuru kwa ubunifu katika ujenzi, hasa kwa miradi hii ambayo imeongeza thamani kubwa kwa maeneo yetu. Tuna kila sababu ya kuhakikisha kwamba biashara zinafanyika vizuri na huduma zinaendelea kusogezwa karibu na wananchi,” amehitimisha Mtambule.
Kwa upande wake, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), limemshukuru Mkuu huyo wa Wilaya kwa ushauri wake na ushirikiano anaouonyesha mara kwa mara.
NHC imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kuleta maendeleo kupitia miradi ya makazi bora na huduma zinazokidhi mahitaji ya Watanzania.
Mradi wa Morocco Square uliopo katika makutano ya Barabara za Mwai Kibaki, Ali Hassan Mwinyi na Ursino eneo la Regent Estate, wilayani Kinondoni, unaendelea kuwa sehemu muhimu ya juhudi za NHC za kukuza uchumi wa maeneo ya mijini, kuboresha maisha ya wakazi na kuimarisha sekta ya ujenzi nchini.
Kupitia mradi huo wa kipekee, NHC imejenga majengo manne kwenye msingi mmoja, jengo moja likiwa ni hoteli, la pili ofisi mbalimbali, jengo la tatu ni la biashara na la nne ni makaziya watu.
Mradi huo uliozinduliwa Novemba 23 mwaka 2024, umejengwa kwa gharama ya Shilingi bilioni 137 ni alama mpya ya kazi nzuri zilizofanywa na NHC nchini likiwa na nyumba za makazi, ofisi, maeneo ya biashara na burudani yakiwa kwenye msingi wa jengo moja.
![]() |
Sehemu ya jengo la Morocco Square inavyoonekana kwa nje. |
0 Maoni