- DC aipongeza NHC
- Ni baada ya kutembelaea Samia Housing Scheme
Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule, amefanya ziara katika mradi wa kihistoria wa Samia Housing Scheme, unaotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Kawe, jijini Dar es Salaam na kupongeza jitihada za shirika hilo kuendeleza makazi bora nchini.
Akizungumza katika ziara hiyo, Mtambule amesema kuwa iwapo mradi huo ungejengwa na mkandarasi wa nje, gharama zingefikia shilingi bilioni 72, hivyo ufanisi wa NHC ni jambo la kujivunia.
“Hivyo tunaweza kueleza kuwa, hapa NHC imeokoa takriban Shilingi bilioni 24, ambazo sasa zinatumika kwa shughuli nyingine za kuendele za makazi nchini,” amesema Mtambule na kuongeza:
“Nimevutiwa sana na mradi huu. Nyumba hizi nzuri na za kisasa zitadumu kwa muda mrefu na zimeongeza thamani ya Kinondoni. Tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha miradi kama hii iliyokuwa imekwama sasa imekamilika.”
Ziara hiyo ya Januari 8,2025 ililenga kukagua maendeleo ya mradi huo mkubwa, wenye lengo la kuboresha makazi nchini na kuimarisha ustawi wa wakazi wa Kinondoni na Tanzania.Mkuu huyo wa wilaya amepongeza juhudi za NHC kuboresha mazingira ya kibiashara na huduma za jamii akisema:
“Tunajivunia ushirikiano mzuri uliopo. Ninaomba ubunifu huu usiishie Kawe pekee, bali ufike maeneo mengine kama Bunju, Madale, na Mabwepande, ambapo pia kuna fursa za uwekezaji.”
Amesema ubunifu na juhudi za NHC kuhakikisha nyumba zinajengwa kwa viwango bora na gharama nafuu ni za kupigiwa mfano na zinastahili kuungwa mkono.
Awali, Mtambule alipokea taarifa kutoka kwa Mhandisi Grace Msita wa NHC aliyeeleza kuwa mradi huo wa Samia Housing Scheme umelenga kujenga nyumba 5,000 kwa awamu.
“Mradi unakadiriwa kugharimu shilingi bilioni 48 hadi ukapokamilika na tayari shilingi bilioni 30 zimetumika kufanikisha hatua zilizofikiwa sasa,” amesema Mhandisi Msita.
Ameongeza kuwa hatua za ujenzi zinaendelea kwa kasi kukamilisha mradi huo, huku kazi za sasa zikiwa ni kufunga milango, kuimarisha mifumo ya lifti na kupanga njia za watembea kwa miguu (pavement).
Shirika la Nyumba la Taifa limemshukuru Mkuu huyo wa Wilaya kwa ushauri na ushirikiano anaotoa mara kwa mara, likisisitiza dhamira yake ya kuendelea kuboresha makazi na huduma kwa Watanzania.
![]() |
Sehemu ya Mradi wa Samia Housing Scheme unavyoonekana pichani. |
Mradi wa Samia Housing Scheme unaakisi dhamira ya Rais Samia na NHC ya kuhakikisha Watanzania wanapata makazi bora ya kisasa kwa gharama nafuu, huku ukichangia kukuza uchumi na kuboresha mazingira ya maisha.
Mkuu wa Wilaya amepongeza juhudi za NHC kwa kujenga nyumba zenye viwango vya juu kwa bei nafuu, huku akitoa wito wa kuendelea na kasi hiyo ili kuhakikisha azma ya kutoa makazi bora kwa Watanzania inatimia.
Mradi huo ni sehemu ya jitihada za kuimarisha makazi bora ya kisasa kwa ajili ya Watanzania, ukiashiria pia ukuaji wa sekta ya nyumba na ujenzi nchini.
0 Maoni