-Rais Samia aunga mkono
wanyang'anywe visiwa
Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com Zanzibar; Rais Samia Suluhu Hassan
amezindua hoteli kubwa ya kitalii Bawe Island the Cocoon Collection iliyopo
katika Kisiwa cha Bawe Januari 7,2025, huku Rais wa Zanzibar Dk. Hussein Mwinyi
akitoa siku 90 kwa wawekezaji walioshindwa kuendeleza visiwa walivyovikodi
kuvirejesha serikalini.
Katika tukio hilo la kihistoria, ambalo ni sehemu ya sherehe za maadhimisho ya
miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Januari 12 mwaka 1964, Rais Samia
amezindua hoteli hiyo akiwa na mwenyeji wake Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Uzinduzi wa hoteli hiyo ni sehemu ya mikakati
ya Dk.Mwinyi kuinua Uchumi wa Zanzibar kwa kuvutia wawekezaji, ambapo uwekezaji
wa Bawe Hotel umefanyika chini ya mpango ukodishwaji ardhi ya visiwa vidogo
chini ya Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) na tayari visiwa16 kati ya 50
vimewekezwa.
Akiungumza katika hafla hiyo kwenye kisiwa hicho kilichopo umbali
wa kilometa kumi kutoka Mji Mkongwe, Rais Samia amesema Dk. Mwinyi aliona mbali
kwa kufikiria na kutekeleza ukodishaji wa visiwa vidogo.
“Dk Mwinyi aliona mbali
kukoisha visiwa, waswahili husema,uchumi tuliukalia, leo ajira zaidi ya 400
zimezalishwa. Ujenzi na uwekezaji katika visiwa vidogo utakuza jina la Zanzibar,
kila jambo lina mambo yake,” amesema Dk Samia na kuongeza:
“Uwekezaji huu hapa
Bawe wa zaidi ya Dola za Marekani 42 milioni (Shilingi bilioni 109.2) ni ishara
ya wawekezaji kuridhika na mazingira pia utawala.”
Rais Samia amesema lengo na
dhamira ya mapinduzi ni kuwaletea neema wananchi wa Zanzibar na kwamba hata
Ilani ya Uchaguzi wa CCM imeeleza, yapo mambo mengi ya kufanya, ikiwamo Uchumi
wa Zanibar kuwa endelevu.
“Mawapongeza ZIPA kusimamia uwekezaji, msiingizwe
mtegoni, kazi iendelee, yajayo yanafurahisha. Serikali imedhamiria kuongeza
uwekezaji bandarini katika Bandari ya Malindi, Maruhubi, Fumba, Mkoani, Manga
Pwani na Mpigaduri,pia ujenzi wa Bandari Wete na kubwa zaidi Kizimkazi;
Hapa
Dk.Mwinyi umemaliza, ntakupa kila ushirikiano, Uwanja wa Ndege wa Abeid Amani
Karume unaendelea kuboreshwa, Pemba sasa ndege zinarukahata usiku, ila tutafanya
makubwa zaidi.
Naipongeza ZIPA kwa usimamizi madhubuti, tuendelee kuelimisha
wananchi uwekezaji katika visiwa kwani ni jambo jipya kwao.”
Rais Samia amesema
jeuri ya leo ya Zanzibar katika maeneleo inatokana na mchango wa Serikali ya
Mapinduzi awamu zote,akihimiza wananchi kuendelea kuyaenzi mapinduzi.
Awali,
akimkaribisha Rais Samia, Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi amesema:
“ …Leo
niseme hadharani kwamba Rais Samia amekuwa msaada mkubwa kwa Serikali ya
Mapinduzi Zanzibar katika mambo yetu yote. Namshukuru na kumpongeza kwa dhati na
kwa kweli tupo pamoja naye katika kuijenga nchi yetu kwa pande zote za Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania.
Leo ni historia ya pekee, tumeonyesha faida ya maeneo ya
visiwa, awali yalisemwa mengi.”
Dk. Mwinyi amesema Serikali yake kupitia ZIPA
imeshatoa visiwa 16 kwa wawekezaji ili viwekezwe na kwamba Bawe ndio mradi wa
kwanza kuzinduliwa ikiwa na kiwango cha kimataifa, akiwashukuru wawekezaji kwa
kutimiza waliloahidi ikiwamo kuwasaidia wavuvi waliokuwa wakitumia kisiwa hicho
kwa kuwajengea jiko la kisasa na kununua samaki wote wanaowavua.
Amewaonya
wawekezaji waliokodishwa visiwa bila kuviendeleza kwa muda mrefu kuwa
vitarejeshwa serikalini wsipofanya lolote ndani ya siku 90.
“…Nataka leo nitoe
tamko kwa wale wote ambao tumewakodisha visiwa, muda umekuwa mrefu, hawajaanza
kujenga, Serikali inawapa miezi mitatu kuanzia sasa. Hapo tutakapoona
hawaendelezi tutavirudisha serikalini,” amesema.
Rais Samia Suluhu Hassan katika
hotuba yake ya ufunguzi wa hoteli hiyo ameunga mkono kauli ya Dk,Mwinyi kuhusu
kuwanyang’anya wawekezaji wasiondeleza visiwa hivyo akisema;
“Nami naungana na
Rais wa Zanzibar kwamba wale wote waliopewa visiwa nahawajafanya kazi, basi
miezi mitatu,baada yah apo Mheshimiwa Rais usirudi nyuma.”
Akizungumzia CCM,
Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi amesema Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho ya
mwaka 2020 iliwataka kuongeza vitanda kwenye hoteli za kitalii kutoka 10,000
hadi 15,000, lakini hadi 2024, mwaka mmoja kabla muda wa utekelezaji kuisha
wameshaongeza kufikia 15,132.
Dk. Mwinyi ametaja faida kubwa tatu za uwekeaji
ikiwamo kukukua kwa soko la bidhaa za wazanzibari, kuongezeka watalii na ajira, akiwataka Wazanzibar kuwa na weledi na kusoma ili waweze kufanya kazi kwenye
hoteli hizo za kitalii.
Amedokeza kuwa nchi ya Italia kupitia balozi wake nchini
imeeleza kutenga kiasi cha Euro 5000 kwa ajili ya kuwajengea uwezo Wazanzibar
waweze kuajiriwa kwenye hoteli hizo, akiishukuru Italia kwa msaada huo.
0 Maoni