Hussein Ndubikile, daimatznews@gmail.com
Waziri Mkuu Kivuli wa Chama cha ACT Wazalendo, Isihaki Rashidi Mchinjita, amesema kuwa Baraza la Mawaziri Kivuli la chama hicho litautumia mwaka 2025 kwa kusimamia haki za wananchi, uwajibikaji wa Serikali na kupigania mageuzi ya kweli ya kidemokrasia.
![]() |
Waziri Mkuu Kivuli wa Chama cha ACT Wazalendo, Isihaki Rashidi Mchinjita akizungumza na wanahabari Januari 8,2025 Makao Makuu ya ACT, Magomeni Dar es Salaam, |
Mchinjita amesema mwaka 2024 ulikuwa wa changamoto nyingi ikiwamo migogoro ya ardhi, hali ya kiuchumi isiyorihisha, kuongezeka kwa matukio ya utekaji na mauaji, maafa ya mvua za Elnino na wananchi kukosa huduma bora akieleza kwamba mwaka 2025 haupaswi kuendelea na taswira ya mwaka jana..
Katika kusisitiza msimamo huo, amesema kuwa Watanzania wanapaswa kushirikiana na ACT Wazalendo kufanya maamuzi yatakayoleta mabadiliko katika kuimarisha maisha yao na kujenga taifa la wote.
Kauli hiyo ameitoa Januari 8, 2025 alipozungumza na waandishi wa habari Makao Makuu ya chama hicho, Magomeni, Dar es Salaam wakati akitoa tathmini ya mwaka 2024 na kuelezea mwelekeo wa baraza hilo kwa mwaka 2025.
“Mwaka 2025 ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu ni mwaka wa uamuzi. ACT Wazalendo tumejizatiti kuimarisha haki za kijamii, kupigania mageuzi ya demokrasia na maendeleo ya kiuchumi kwa maslahi ya wote.”
Waziri Mkuu huyo kivuli amesema mwaka 2024 ulikuwa na changamoto ya hali mbaya ya kiuchumi, ambapo deni la serikali lilifikia shilingi trilioni 93.7, hali aliyosema inaathari uwezo wa taifa kutoa huduma bora hata ajira katika sekta muhimu ikiwamo afya na elimu hivyo ugumu wa maisha kuongezeka.
“Ni jambo la aibu kuona wananchi wa kipato cha chini wakinyimwa huduma za afya kwa sababu hawawezi kumudu gharama afya ambazo ni haki, si bidhaa,” aliongeza.
Akizungumzia demokrasia, Mchinjita ameeleza hitaji la Tanzania kuwa na Tume Huru ya Uchaguzi, akibainisha kuwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2024 umeonesha sura isiyofurahisha kuelekea mageuzi ya kweli.
“Ili tuwe na uchaguzi wa haki na uwazi mwaka 2025 ni lazima tuwe na Tume Huru ya Uchaguzi itakayohakikisha kila kura ya Mtanzania inaheshimiwa,” aliongeza.
Amehitimisha kwa kuahidi kuwa Baraza la Mawaziri Kivuli la ACT litaendelea kuwa sauti ya wananchi, huku ikisisitiza mshikamano wa kitaifa kupambana na changamoto zilizopo.
0 Maoni