Alhamisi, 28 Machi 2024

'Hatutawavumilia wanaokwamisha wawekezaji'

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

MAKAMU wa Rais Dk. Philip Mpango amesema Serikali haitasita kuchukua hatua kwa watumishi wataobainika kushiriki kukwamisha wawekezaji wanaotaka kuwekeza nchini, huku akitaja hatua nne walizochukua ili kuvutia wawekezaji.

Dk. Mpango amesema hayo mkoani Dar es Salaam Machi 27, 2024 wakati akifunga la Kongamano la Uwekezaji kati ya China na Tanzania, lililokutanisha zaidi ya kampuni 300 za mataifa hayo, kujadili fursa mbalimbali za uwekezaji.

Makamu wa Rais Dk. Phillip Mpango akifunga la Kongamano la Uwekezaji kati ya China na Tanzania, lililokutanisha zaidi ya kampuni 300 za mataifa hayo, kujadili fursa mbalimbali za uwekezaji.

Makamu wa Rais amesema, kumekuwa na kasumba kwa baadhi ya watumishi wa umma kukwamisha wawekezaji kwa kuendekeza urasimu na rushwa, jambo ambalo hawapo tayari kuvumilia.

“Napenda kuchukua nafasi hii, kuwaagiza watumishi wa umma ambao mnashiriki mchakato wa uwekezaji na nitumie nafasi hii kuwaomba wawekezaji ambao watakutana na vikwazo, wawasiliane na mimi,” amesema.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, imedhamiria kukuza uchumi kupitia sekta ya uwekezaji, hivyo atashangaa kuona mtumishi anashiriki kukwamisha hilo.

Ametaja maeneo hayo kuwa ni kuondoa vikwazo kama urasimu, kupambana na rushwa, kuweka mazingira wezeshi na kuboresha sera na sheria.

“Ili uwekezaji uweze kufanikiwa, tumechukua hatua za kuboresha mazingira kwa kuondoa vikwazo vya urasimu, kupambana na rushwa, kuweka mazingira wezeshi na kuboresha sera na sheria,”amesema Dk. Mpango

Makamu wa Rais amesema iwapo watendaji wote ambao wanasimamia sekta ya uwekezaji wataepuka maeneo hayo manne ambayo ameanisha ni wazi kuwa sekta hiyo itakuwa na mchango mkubwa.

Amesema ni wakati wa kila Mtanzania kutamani maendeleo ya nchi yake na kuachana na urasimu unaokwamisha wawekezaji wa ndani na nje.

Dk. Mpango amesema wawekezaji wanaokuja kuwekeza Tanzania wasisite kutoa taarifa kwa viongozi akiwemo yeye, pale watakapokutana na vikwazo kwa watendaji wa Serikali.

Amesema Tanzania ina fursa nyingi za uwekezaji katika sekta ya kilimo, viwanda, afya na nyingine nyingi, hivyo Serikali inataka zitumike kuchochea maendeleo ya taifa.

Ameitaka China kuleta wawekezaji wengi zaidi nchini, akieleza hali hiyo itaendelea kudumisha uhusiano kati ya mataifa hayo uliodumu kwa zaidi ya miaka 60 sasa.

Washiriki wa Kongamano la Uwekezaji kati ya China na Tanzania, lililokutanisha zaidi ya kampuni 300 za mataifa hayo, kujadili fursa mbalimbali za uwekezaji lililofanyika Dar es Salaam Machi 27, 2024.

Amesema  urafiki na uhusiano wa Tanzania na China umechangia ukuaji wa Pato la Taifa kutoka asilimia 4.8 mwaka 2020 hadi kufika asilimia 5.5 mwaka 2023 na inakadiriwa kuanzia mwaka 2024-2027 pato litafikia asilimia 6.0.

Dk. Mpango amesema taarifa za ukuaji wa pato la taifa zimethibitishwa na Taasisi ya Moody’s na Fisch, hivyo kuwataka wawekezaji kuja kuwekeza kwa kuwa taifa hilo fursa nyingi.

“Novemba mwaka 2022, Taasisi ya Moody’s iliizawadia Tanzania alama ya B2 kwa mtazamo chanya na Desemba mwaka 2023, Fisch iliipa Tanzania Tuzo ya alama B+. Machi 22, Moody’s ilipandisha Tanzania daraja B1 kwa mtazamo thabiti, kwa vigezo hivyo ni wazi kuwa Tanzania inaenda kwenye mafanikio,” amesema.

Abainisha kuwa ukadiriaji huo ni kielelezo cha ukuaji uchumi wa taifa ambao umeweza kuhimili changamoto za mtikisiko wa uchumi duniani, baada ya janga la virusi vya corona.

Kwa mujibu wa Dk. Mpango Tanzania iko kwenye eneo la kimkakati kijiografia linaloifanya kuwa kitovu cha biashara cha kikanda, soko kubwa la ndani lenye watu milioni 64.

“Soko la kikanda la watu takribani bilioni 1.4 chini ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) na Eneo Huru la Biashara la Bara la Afrika (AfCFTA) ni sababu nyingine ya kuwaomba wawekezaji kuja kuwekeza,” amesema.

Dk. Mpango amesema mageuzi ya uwekezaji na biashara ambayo yanaonekana kwa asilimia kubwa yamechangiwa na falsafa ya 4R ya Rais Samia.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema wawekezaji kutoka China wamekuwa wakizingatia muda mfupi wa majadiliano na ni wavumilivu.

“China inakwenda mahali ambapo mataifa mengine yenye nguvu yanashindwa kwenda. Miaka 50 iliyopita tulikuwa na tatizo la reli, na karibu mataifa yote yenye nguvu yalikuwepo lakini hayakuwa tayari kutusaidia kujenga reli, na wakati huo China haikuwa nchi tajiri kama ilivyo sasa, lakini ilikubali kutujengea reli yetu ambayo ni reli ya kukumbukwa, imani yetu watakuja wengi kuja kuwekeza Tanzania,” amesema.

Makamu wa Rais Dk. Phillip Mpango akiteta jambo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo baada ya ufunguzi wa Kongamano la Uwekezaji kati ya China na Tanzania, lililokutanisha zaidi ya kampuni 300 za mataifa hayo, kujadili fursa mbalimbali za uwekezaji.

Prof. Kitila amesema Tanzania ina soko kubwa la ndani, hivyo kuwataka wawekezaji na wafanyabiashara kuja kuwekeza nchi kwa kuwa mazingira ni mazuri.

“Tuna bidhaa nyingi ambazo tunaagiza kutoka nje, ambazo tulipaswa kuzalisha hapa ikiwemo mafuta ya kupikia, sukari ba nguo, hivyo ujio wa kampuni hizi 60 kutoka china ni ishara nzuri kwa siku zijazo,” amesema.

Kitila amesema Tanzania ina vigezo vyote 10 vya kuvutia uwekezaji duniani, ambapo mojawapo ya vigezo ni utulivu wa kisiasa na amani uliopo nchini.

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Dk. Tausi Kida amesema kuanzia mwaka 2021 hadi Desemba 2023 jumla ya miradi 256 kutoka China ilisajiliwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ambayo ina thamani ya Dola za Marekani bilioni 2.4 huku ikitoa ajira zaidi ya 29,122.

“Hawa ni wadau wetu na washirika wa maendeleo na uchumi katika kongamano hilo kampuni 60 kutoka Jimbo la Jinhua,China zimekuja  nchini na zimetembelea eneo la uwekezaji la Sino-Tanzania mkoani Pwani na kuona fursa na miradi ya uwekezaji inayoendelea,”amesema Dk. Kida.

Aidha, Dk. Kida amesema uwekezaji wa moja kwa moja kutoka taifa hilo nchini unaongezeka kutoka Dola za Marekani milioni  92 mwaka 2019 hadi Dola za Marekani milioni 221 mwaka 2021.

Ametaja miradi ambayo watu kutoka China wamewekeza ni viwanda, ujenzi wa biashara, kilimo, uchukuzi na huduma.

Balozi wa China nchini,  Chen Mingjian, amesema Tanzania ina nafasi maalum na muhimu katika urafiki kutoka na uimara wa misingi waliyoiweka waasisi wetu Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Hayati Mao Zedon.

“Tunafurahi kuona uwekezaji wa China hapa Tanzania ukitoa mchango mkubwa wa uchumi wa nchi na jamii kwa ujumla, na hii inatupa faraja kwetu kuona kwamba tuna na safari inayofanana. Hadi sasa ajira zaidi ya 150,000 zimezalishwa kutokana na miradi ya uwekezaji kutoka china,” amesema.
Amesema wawekezaji kutoka China wanaiona Tanzania kama ni nchi ya ahadi na kutumia rasilimali zilizopo kuleta tija kwa malengo ya kunufaisha nchi zote mbili, lakini pia kuifanyaTanzania kuwa ni kituo cha uzalishaji.

Amesema kuwa maendeleo makubwa ya utulivu pamoja na uongozi madhubuti wa Serikali, wafanyabiashara wengi wa China wamevutiwa kuja kuwekeza Tanzania, na zaidi mapokezi wanayopata yanawafanya waendelee kushiriki

Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Angelina Ngalula amesema chini ya uongozi wa Rais Samia, Tanzania imeweka alama katika kuboresha mazingira ya uwekezaji, hali ambayo inavutia wawekezaji.

“Urari wa biashara kati ya Tanzania na China umezidi kuongezeka, na kufikia mwaka 2022 urari wa biashara katika nchi hizi ulifikia zaidi ya dola bilioni 8, na kupelekea China kuwa ni mbia mkubwa wa biashara kwa nchi ya Tanzania, kwa kipindi cha zaidi ya miaka 8 mfululizo,” amesema.

Katibu wa  Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) wa serikali ya Jinhua nchini China Zhu Chonglie amesema wao kama Mkoa wa Zhejiang, na Serikali yao ya Jiji la Jinhua watahakikisha wawekezaji wanakuja kuwekeza nchini.

Amesema wamekuwa na ushirikiano kwa muda mrefu akitolea mfano kongamano la elimu liliratibiwa na Chuo cha Zhejiang Normal University Tanzania China Education Forum.

Amesema, Tanzania imekuwa nchi ya kwanza Afrika kupokea vikundi mbalimbali vya maonyesho ya utamaduni lakini pia vikundi vya Tanzania vimefika Zhejiang kubadilishana uzoefu.

“Ujio wetu hapa kwa ajili ya Kongamano hili la Uwekezaji ni matokeo ya ushirikiano wa kihistoria uliopo lakini na ukuaji unaoendelea, tunapaswa kuutunza kupitia mabadilishano kama haya ya kiuchumi,” amesema.


Jumatano, 27 Machi 2024

Wachambua miaka 3 ya Dk. Samia, waishauri

 Hellen Ngoromera, daimatznews@gmail.com

Miaka mitatu ya Rais Samia Suluhu Hassan madakani imetajwa kuimarisha na kukuza demokrasia nchini, huku wasomi wakiishauri Serikali kuboresha maisha ya wananchi kiuchumi.

Rais Samia ametimiza miaka mitatu madarakani tangu alipotwaa madaraka ya kuiongoza Tanzania Machi 19, 2021, kufuatia kifo cha mtangulizi wake, Rais John Magufuli Machi 17,2021.

Rais Dk. Samia Suluhu Hassan

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana Machi  26 katika mjadala wa uchambuzi wa miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia madarakani ulioandaliwa na Kampuni ya Mchambuzi Media, Mchambuzi wa masuala ya kisiasa Dk. Denis Muchunguzi na Profesa Samuel Wangwe wameeleza hayo.

"Napongeza miaka mitatu ya  Dk. Samia kwani amefanya makubwa... tumeshuhudia mikutano ya kisiasa ikiruhusiwa, maandamano ya Chadema kwenda Umoja wa Ulaya yalifanyika bila bugudha," amesema Dk. Muchunguzi.

Ameongeza kuwa katika miaka mitatu hiyo hata baadhi ya watu wakiwemo wanasiasa waliohama nchini kutokana  na  sababu mbalimbali walirejea nchini.

Dk. Muchunguzi ametaja jambo jingine kuwa ni pamoja na  kuruhusiwa kwa mitandao ya kijamii ambayo ilipigwa marufuku, huku akishauri vyama vya siasa kuwa imara na madhubuti kifedha viweze kujiendesha vyema.

"Vyama vya siasa viwe imara kifedha, hatuhitaji kuona vyama vinakufa," amesema Dk. Muchunguzi.

 Kwa upande wake, Profesa Samuel Wangwe aliyechangia mada ya Uchumi na Miradi ya Maendeleo, ameshauri Serikali kuboresha maisha ya wananchi ili kuwakwamua kiuchumi.

Profesa Wangwe amesema katika kipindi cha miaka mitatu ya Rais Samia madarakani, ameweze kuinua uchumi na kufikia asilimia 5.2 na kwamba ana imani  kiwango cha ukuaji wake kitaongezeka kwa mwaka huu.

Jumatano, 20 Machi 2024

Wanaumee, hii hatari

-Takwimu zawataja kujamiiana zaidi

Exuperius Kachenje, daimatznews@gmail.com

Karibu nusu ya wanaume Tanzania, wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 49, walifanya mapenzi na mwanamke zaidi ya mmoja ndani ya miezi 12, wakati asilimia nne pekee ya wanawake wenye umri kama huo, walifanya mapenzi na wanaume tofauti kwa kipindi hicho.

Matokeo ya Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria wa Mwaka 2022 inayopatikana Ofisi ya Taifa ya Takwimu, yamebainisha hayo yakieleza kwamba, asilimia 21 ya wanawake walijamiiana na watu ambao ama walikuwa w waume zao au waliishi nao.

 “Kati ya wanawake hao, asilimia 22 walitumia kondom mara ya mwisho walipojamiiana na wenza wao hao,” ripoti hiyo inaweka wazi.

 Kwa mujibu wa ripoti hiyi ya utafiti, asilimia 38 ya wanaume walijamiiana na watu ambao ama ni wake zao au waliowahi kuishi nao, huku asilimia 43 ya wanaume hao wakitumia kondom mara ya mwisho walipojamiiana na wenza wao.

 Kuhusu kupima Virusi vya Ukimwi (HIV), matokeo ya utafiti huo yamebainisha kwama wanawake wanane kati ya kumi wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 49 hawajawahi  kupima wala kupokea matokeo ya vipimo hivyo. 

“Kwa upande wa wanaume asilimia 64 hawajawahi kupima wala kupokea matokeo ya vipimo hivyo katika miezi 12 iliyopita,” inawka wazi ripoti hiyo. 

Matokeo hayo yanaonyesha katika kipindi hicho asilimia 37 ya wanawake na asilimia 31 ya wanaume walipima HIV na kupokea matokeo yao mara ya mwisho walipopima. 

Hata hivyo, ni wanawake wachache sawa na asilimia 18 ndio wamesikia kuhusu uwepo wa vifaa vya upimaji binafsi HIV, huku asilimia 31 ya wakiwa wanaume, ambapo asilimia tatu ya wanawake na tano ya wanaume wametumia vipimo hivyo.

 

Jumatano, 13 Machi 2024

Anne Makinda: Sensa ni kiboko kwa wanasiasa

Exuperius Kachenje, daimatznews@gmail.com
Spika wa Bunge Mstaafu, Anne Makinda amewataka wanasiasa kutofurahia tu matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, badala yake watambue kuwa inaweza kuwa kiboko kwao.

Makinda ambaye pia ni Kamisaa wa Sensa nxhini, ametoa kauli hiyo leo Machi13,2024 jijini Dar es Salaam alipokuwa mgeni rasmi katika mafunzo ya waandishi wa habari, kuhusu matumizi ya takwimu za sensa ikiwa ni sehemu ya awamu ya tatu ya utekelezaji Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.

"Tumewaambia wanasiasa wenzagu, sensa hii imefanikiwa. Lakini, kwenu ni kiboko, shangilieni lakini watu watakuwa wanauliza maswali kutokana na takwimu na maelezo yaliyomo kwenye matokeo ya sensa. Sisi tunafundisha mpaka chini kwa wananchi," amesema Makinda.
Spika mstaafu huyo, ametoa onyo hilo kwa wanasiasa wakati ambapo taifa linatarajia kufanya uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu 2024 na Uchaguzi Mkuu mwakani 2025.

Amebainisha kuwa kutokana na wananchi kupata uelewa kuhusu matumizi ya takwimu ikitokea kiongozi wa siasa anataka kusema vitu vyake visivyo na uhalisia, mtu wa kawaida atanyoosha mkono kumuumbua kufuatana na sensa.

"Kila mtu anafundishwa ili kila mmoja awe na uelewa kuhusiana na sensa, pia matokeo na takwimu zake," amesema.

Amebainisha kuwa NBS imeona umuhimuwa kuwapa mafunzo pia waandishi wa habari ili taaluma hiyo iwe ya kuaminika zaidi kwa takwimu.

 "Waandishi wa habari mna nafasi kubwa katika suala hili na sisi tunawategemea. Tunategemea nchi yetu ifike mahali inazungumza habari za takwimu, sio tunazungumza maneno ya majungu majungu tu vitu vitu visivyoeleweka, hapana, tuzungumze maendeleo," amesema Makinda.


Amesema baada ya Rais kutangaza matokeo ya mwanzo mwaka 2022, kulitokewa mwongozo ambao lengo lake kuu ni kutumia matokeo ya sensa ya mwaka 2022 ili kuongeza uelewa, kufanya uwazi na kupanua wigo wa matumizi ya matokeo ya sensa kwa serikali zetu.

"Hili ni kwa wananchi pia  na wadau wote ili waweze kupanga mipango yao jumuishi kwa maendeleo endelevu ya kiuchumi, kijamii na kimazingira," amesema Kamisaa huyo wa Sensa.

Waandishi wa habari wambwaga Mbowe kortini

 Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe, amebwagwa kortini na waandishi wa habari 10, wanaomdai mtoto wake katika kesi aliyofungua kutaka wamlipe gharama kwa kukamata nyumba yake.

Uamuzi huo umetolewa na Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Kazi leo Machi 13 2024 mbele ya Naibu Msajili Mary Mrio kufuatia  maombi ya Mbowe, yaliyowasilishwa kwa hati ya dharura chini ya kiapo cha Mbowe, aliyewakilishwa na Wakili John Mallya.

Uamuzi huo wa Mahakama umetolewa baada ya kupitiwa hoja zote za mleta maombi.

Hoja hizo za Mbowe ziliwasilishwa na Mbowe kupitia Wakili wake John Mallya, ambapo Mrio amesema mahakama iliona hakuna ubishi katika maombi ya kuiachia nyumba na kwamba kinachobishaniwa ni mleta maombi (Mbowe), kulipwa gharama za kesi na wajibu maombi, ambao ni waandishi wa habari 10 na dalali wa mahakama.

Mrio amesema: "Mahakama iliangalia katika kesi hii kama gharama zilipwe au zisilipwe. Nimepitia Gazeti la Serikali (GN) namba 106 la mwaka 2007, lilielekeza kwamba kesi za aina hii hakuna sehemu inayoelekeza kulipa gharama."

Kuhusu shauri hilo, Mrio amesema: "Mahakama inaona hakuna haja ya kutoa gharama, kila upande ubebe gharama zake na inatamka kwamba nyumba iliyokamatwa iko huru."

Jana, waandishi wa habari 10 wanaomdai Dudley ambaye ni Mkurugenzi wa Tanzania Daima, Sh milioni 62.7, waliachia nyumba ya Freeman Mbowe waliyoikamata ili kuipiga mnada kufidia deni lao.

Hata hivyo, waligomea kulipa gharama za kesi zilizoombwa na Mbowe wakieleza sababu hata wao wameingia gharama katika kudai haki yao.

Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi ilisikikiza shauli hilo mbele ya Naibu Msajili, Mary Mrio leo Machi 12,2024 ikieleza itatoa uamuzi kuhusu gharama kesho saa 8 mchana.

Mbowe kupitia Wakili wake John Mallya aliwasilisha maombi chini ya kiapo kilichoapwa na Freeman Mbowe Februari 26 mwaka huu, akitaka wajibu maombi kuondoa nyumba hiyo kwa sababu si mali ya Dudley na Mahakama iwaamuru wajibu maombi hao kumlipa gharama za kesi mteja wake.

Akizungumza kwa niaba ya wajibu maombi wenzake, Kulwa Mzee aliiambia mahakama kwamba walipitia nyaraka zote na viambatanisho husika, wamejiridhisha na kukubaliana kwa pamoja kwamba nyumba waliyoikamata ni ya familia, lakini inamilikiwa na Freeman Mbowe.

"...Tumepitia nyaraka pamoja na viambatanisho ikiwemo hati ya nyumba. Tumejiridhisha kwamba mkurugenzi tunayemdai, Dudley Mbowe si mmiliki. Hivyo, tunaiomba Mahakama tuiondoe nyumba hiyo kwenye maombi yetu," alisema Kulwa na kuongeza:

"Mheshimiwa, kuhusu gharama, kwa uelewa wetu, katika mashauri ya migogoro ya kikazi, hakuna gharama. Hiyo inatokana na uwezo na kipato kidogo cha wafanyakazi;

"Wakati sisi tunafanya jambo hili, tulikuwa tukiamini kabisa kuwa ni nyumba ya mkurugenzi wetu kwa sababu katika hatua ya makubaliano, alikuwa anatuambia kuwa tutafanya vikao nyumbani kwake na tumefanya hapo vikao  kwenye hiyo nyumba," amesema Kulwa.

Ameongeza: "Mheshimiwa katika hatua za mwisho, baba yake ambaye ndiye mwombaji katika shauri hili alitualika tukutane hapo hapo tulipokuwa tukikutana. Tulikutana hapo, akakubali kubeba dhamana ya mtoto wake akakubali kutulipa mwezi Desemba."

Kulwa alidai kutokana na mazingira hayo waliamini kuwa hapo ndipo nyumbani kwake mkurugenzi na baada ya kushindwa kuwalipa katika kutekeleza namna ya kupata haki yao ndio maana waliamua kukamata hiyo nyumba.

"...Mheshimiwa tunaomba tusilipe gharama, kwanza huyu mwombaji hakuingia gharama kwani katika  hatua zote za majadiliano tulikuwa tunakwenda kwake kwa gharama zetu wenyewe na ahadi zake za kutulipa Desemba 2023 ambazo alishindwa kutekeleza hilo lilituathiri, maana tulikuwa katika maandalizi ya siku kuu na  ada za watoto shuleni,"amedai Kulwa.

Aliomba Mahakama katika uamuzi kuhusu gharama ikiwezekana kila upande ubebe gharama zake.

Kwa upande wake, dalali wa Mahakama Jesca Massawe ambaye ni mjibu maombi wa 11, alidai alipokea amri ya Mahakama kwa ajili ya kukamata hiyo nyumba.

"Sisi madalali wa Mahakama katika kutekeleza majukumu yetu, tulikaa na Mahakama hii chini ya Jaji Mfawidhi  akatuelekeza kuwa katika mashauri haya ya kukamata mali tusijihusishe na utambuzi wa mali bali tukamate na kama kuna changamoto basi italetwa mahakamani, " amesema.

Ameongeza kwamba alitekeleza amri ya Mahakama kama ilivyoelekezwa.

Wakili Mallya alijibu hoja hiyo akieleza kwamba anakubaliana na mjibu maombi Kulwa kwa aliyoyasema ya kuachia nyumba hiyo.

Hata hivyo akasema: "Kuhusu suala la gharama, mteja mwombaji anastahili kulipwa gharama na mambo mengine aliyoyasema mjibu maombi alipaswa kuyaleta kwa njia ya kiapo."

Amedai kuhusu hoja za mjibu maombi wa 11 ambaye ni dalali, kweli ni afisa wa Mahakama, lakini maelezo yake hayakuja kwenye kiapo. 

"Kwa kuwa anamtaja na Jaji Mfawidhi, haya yalipaswa kuja kwa njia ya kiapo na si maneno matupu mahakamani. Kwa hiyo naiomba Mahakama yako isiyazingatie  na tunaomba mahakama izingatie suala la gharama,"alidai Mallya.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, Naibu Msajili Mrio aliahirisha shauri hadi leo saa nane mchana kwa ajili ya uamuzi.

Katika shauri la msingi,  mjibu maombi mwingine Maregesi Paul, aliomba kuyaondoa maombi ya kukamata nyumba hiyo na kuieleza Mahakama kwamba wanatarajia kuwasilisha maombi mengine upya ya kumkamata Dudley.

"Maombi haya yameondolewa kwa kibali cha kuyaleta tena, "alisema Msajili.

Mbowe alifungua shauri dhidi ya Maregesi Paul, Fidelis Felix, Christina Mwakangale, Janeth Josiah, Exuperius Kachenje, Hellen Sisya, Kulwa Mzee, Nora Damian, Makuburi Ally, Mkurugenzi wa Gazeti la Tanzania na Kampuni ya Udalali ya JJ Auctioneers& Debt Collectors.

Februari 13 mwaka huu, Mahakama ilikubali maombi ya wadai na kumteua dalali wa Mahakama kukamata nyumba kwa ajili ya kuipiga mnada.

Februari 28 mwaka huu, dalali wa Mahakama, Jesca Massawe alifanikiwa kubandika matangazo ya kukamata nyumba ya Mkurugenzi tayari kupigwa mnada kufidia deni la malimbikizo ya mishahara wafanyakazi.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Mary Mrio alitoa amri hiyo baada ya kupitia hoja za washinda tuzo katika Tume ya Usuluhishi na Uamuzi(CMA) Julai 2023.

Shauri hilo namba 28461 la mwaka 2023, wadai Maregesi Paul na wenzake tisa dhidi ya Mkurugenzi wa Gazeti la Tanzania Daima, Dudley Mbowe.

Baada ya mdaiwa kukaidi kulipa, wadai  walikubaliana njia sahihi kukamata nyumba yake namba 9 iliyopo Mtaa wa Feza , Mikocheni B barabara ya Chipaka na Mahakama ilikubali.

Walalamikaji hao walipata tuzo Julai 17 mwaka 2023 mbele ya Msuluhidhi wa CMA Ilala,  Bonasia Mollel.

Madai ya awali yalikuwa jumla ya Sh milioni 114 baada ya kukaa mezani kwenye majadiliano kwa pamoja kiwango hicho cha fedha kilishuka na kufikia Sh milioni 62.7.

Dudley alikubali kulipa fedha hizo kwa awamu tatu, Oktoba 30, Desemba 30 mwaka 2023 na awamu ya mwisho ilikuwa mwishoni Februari mwaka huu, lakini hakulipa.

Jumanne, 12 Machi 2024

Jafo: Miradi huchochea uwezo wa wananchi

 Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Dk. Selemani Jafo amesema miradi mbalimbali ya mazingira imechangia kuwajengea wananchi uwezo katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Waziri wa nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Selemani Jafo 
akiwasilisha taarifa za utekelezaji wa miradi ya Urejeshwaji wa Mazingira, Bayoanuai Tanzania na Hifadhi Endelevu ya Ardhi katika Bonde la Ziwa Nyasa mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira, Machi 12, 2024 jijini Dodoma.


Ametoa kauli hiyo wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mradi wa Urejeshwaji wa Mazingira na Hifadhi ya Bayoanuai Tanzania (SLR) unaotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa.

Pia aliwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mradi wa Hifadhi Endelevu ya Ardhi katika Bonde la Ziwa Nyasa (SLM-Nyasa) kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira katika kikao kilichofanyika Machi 12, 2024 jijini Dodoma.

Dk. Jafo amesema kuwa kutokana na wananchi kuendelea kupata elimu ya mazingira, wameendelea kushiriki kikamilifu katika shughuli za upandaji wa miti hatua iliyochangia kupatikana kwa mvua katika maeneo mbalimbali nchini.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia kamati yako mmefanya kazi kubwa kwani mmetupa maelekezo ambayo tumeyafanyia kazi, hasa katika eneo la kuwaelimisha wananchi kuhusu kuhifadhi mazingira na matunda yake tunayaona. Wananchi wengi wameendelea kupanda miti kwa wingi,” amesema.

Dk. Jafo amesema kuwa kutokana na uharibifu wa mazingira katika bonde la Ziwa Nyasa unaotokana na shughuli za kibinadamu zisizo endelevu, Ofisi ya Makamu wa Rais inatekeleza Mradi wa SLM-Nyasa kuwajengea uwezo wananchi hao kutumia mbinu bora za kuhifadhi ardhi.

Ameongeza kuwa, kupitia mradi huo wananchi wanaojengewa uwezo wanaweza kuboresha maisha yao kwa kuwa na njia mbadala ya kujipatia kipato na kuachana na vitendo vya ukataji wa miti ovyo au uvuvi usio endelevu. 

 Jafo amesema Ofisi ya Makamu wa Rais inatekeleza Mradi wa SLR ili kuimarisha usimamizi jumuishi wa mazingira na urejeshwaji wa mazingira yaliyoharibiwa ili kujenga uhimilivu wa mifumo ikolojia.

Mfuko wa Self wakopesha bil 324 wananchi 300,000

Selemani Msuya, daimatznews@gmail.com

MFUKO wa Self umetoa mikopo ya zaidi ya Sh bilioni 324 kwa wananchi 314,055 wa mikoa 30 nchini huku ukijipanga kupanua wigo siku zijazo.

Mfuko pia umesema katika mikopo iliyotoa kiwango cha mikopo chechefu ni chini ya asilimia 10, huku wakijipanga kukabiliana na changamoto ya mikopo kaushadamu.

Hayo yamesemwa Machi 12,2024 na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Self, Mudith Cheyo alipozungumza kwenye mkutano wa 53 wa ya taasisi hiyo na wahariri wa vyombo vya habari Dar es Salaam, kupitia uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Cheyo amebainisha kwamba, hadi Desemba 31 mwaka jana, mfuko huo unaotarajia kuwezesha wananchi wengi kwa mikopo, ulifikia zaidi ya wananchi 300,000; wanawake 166,449 sawa na asilimia 53 na wanaume 147,606 sawa na asilimia 47.

Ameongeza kuwa Self pia umekopesha na kuzijengea uwezo taasisi ndogo 200 za fedha na kutengeneza ajira 37,024 kwa mwaka jana na kutoa elimu kwa wakopaji 1,519.

Ofisa Mtendaji huyo amesema katika kipindi cha miaka mitatu ya Rais Samia Suluhu Hassan, Mfuko wa Self umepata faida ya Sh bilioni 2 huku ikitoa gawio kwa serikali zaisdi ya shilingi milioni 240

“Tumekuwa tukikua mwaka hadi mwaka, na tumepata faida ya Sh bilioni mbili, tukatoa gawio la zaidi ya Sh milioni 240, huku mtaji ukiongezeka kutoka Sh bilioni 56 hadi 62,” amesema Cheyo.

Amebainisha kuwa mikakati yao ni kuhakikisha mfuko huo unakuwa na matawi 20 kutoka 12 ya sasa ifikapo mwaka 2026, huku akisisitiza kuwa wamejipanga kuondoa mikopo kaushadamu.

Amesema kupitia mkakati wa kuongeza matawi, wanatarajia kulifikia kundi kubwa la Watanzania, hasa kwenye SMEs ambao wanakadiriwa kufikia milioni nne.

Mkurugenzi wa Biashara wa Self, Petro Mataba amesema Mfuko huo unafanya kazi kwa kuzingatia uadilifu, ushirikiano, ubunifu, mteja na uwajibikaji, hali ambayo imewawezesha kukua kwa kasi.

Amesema Mfuko umetoa mikopo kwa wananchi na taasisi kama Kampuni ya Star Natural Product iliyokopeshwa Sh milioni 100 na Shule ya Bright Future Academy, Sh milioni 400.

Ametaja changamoto zilizopo kuwa ni wananchi wengi kukosa elimu ya fedha, kujishughulisha na biashara zisizo rasmi na kukosa utamaduni wa kukopa na kurejesha, ingawa wanaendelea kutoa elimu ili wabadilike.

Mkurugenzi wa Masoko, Santiel Yona amesema mpango mkakati wao ni kufikia wateja wengi hasa wa kipato cha chini, kuongeza ufanisi na kuhakikisha taasisi inakuwa endelevu

Rais Samia aigusa CCM

 Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Rais Samia Suluhu Hassan, amefanya uteuzi akikigusa Chama Cha Mapinduzi(CCM), kwa kumteua Naibu Katibu Mkuu wake, Anamringi Macha, kuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga.

Kwa hatua hiyo, kuna uwezekano kwa CCM kumteua na kumpitisha mtu mwingine kushika nafasi ya unaibu katibu mkuu, badala ya Anamringi.

Anamringi anachukua nafasi ya Christina Mndema, ambaye ameteuliwa na Rais kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira).

Taarifa iliyotolewa leo na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Zuhura Yunus leo Machi 12,2024, imeeleza kuwa mbali na uteuzi wa wawili hao, Rais Samia pia amefanya uteuzi na uhamisho wa watendaji mbalimbali, wakiwamo wakuu wa wilaya, wakurugenzi watendaji wa halmashauri na makatibu tawala wa wilaya.

Taarifa hiyo ya Ikulu, imeeleza kuwa uapisho wa wakuu wa mikoa na naibu katibu mkuu, utafanyika kesho saa 4 asubuhi Ikulu Dar es Salaam.

Habari zaidi soma orodha ya watbyeule na nafasi zao katika kiambatanisho



Kesi ya Jalakhan yapigwa kalenda Nzega

 Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

MAHAKAMA ya Mwanzo Nzega imeendelea kulipiga kalenda shauri la  Mirathi ya Zena Jalakhan lenye mvutano wa ndugu katika kusimamia mirathi hiyo.

Shauri hilo lipo mbele ya Hakimu Mfawidhi, Abunas Sonyo, ambapo jana liliahirishwa kwa mara nyingine hadi Aprili 23 kwa ajili ya kusikiliza pingamizi.

Mmoja wa wanafamilia, Salma Mohammed katika shauri hilo anayewakilishwa na Wakili Kaumuliza David awali aliomba apewe muda wa kupitia jalada la shauri hilo la mirathi na mahakama ilikubali maombi hayo.

Lakini jana, shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kusikiliza mapingamizi, lakini upande wa Karim Samji ambaye awali aliyekuwa msimamizi wa mirathi, aliomba shauri lisiendelee kwa sababu wakili wao hakuwepo mahakamani.

Karim alidai Wakili wao hakuwepo kwa sababu hakujua mahakamani shauri linaloendelea ni lipi na baada ya Mahakama kuwafahamisha kwamba kinachoendelea ni usikilizwaji wa mapingamizi, waliomba kuahirisha.

Wakili Kaumuliza aliomba Mahakama iahirishe shauri hilo hadi April 23 mwaka huu na hata upande wa pili walipohoji muda ni mrefu, bado wakili aliomba iwe tarehe hiyo kwani ndio atakuwa na nafasi.

Shauri hilo lenye mvutano, upande wa pili wa Salma wanapinga  Karim Samji aliyeteuliwa na Mahakama kusimamia mirathi ya Zena  kutekeleza amri ya Mahakama ya kukusanya mali za marehemu.

Salma Mohammed alifungua shauri la mirathi ya Zainabu Jalakhan kwa mali ambayo ni nyumba iliyopo pia katika mirathi ya Zena Jalakhan, huku mahakama ikiwa ilishamteua Karim kuwa msimamizi.

Mwombaji Salma aliwasilisha hoja tatu, akidai kwamba shauri linalomuhusu marehemu lilikwisha sikilizwa na kutolewa uamuzi katika shauri la mirathi namba 24/2023.

Hoja ya pili mali iliyotajwa katika maombi hayo ilikwishaorodheshwa katika mirathi namba 24/2023 mbele ya Hakimu Hilda Kibona.

Katika hoja ya mwisho ni  kwamba shauri hilo lenye viini hivyo lilishasikilizwa na kuamuliwa na mahakama hiyo hivyo aliomba maombi ya mirathi namba 35 ya mwaka jana ya mali ya Zena Jalakhan, ambayo mahakama ilimteua Karim kuwa msimamizi yatupiliwe mbali.

Awali Mahakama hiyo mbele ya Hakimu Sonyo ilimteua Karim kuwa msimamizi wa mirathi ya mali ya marehemu Zena ambayo ni nyumba iliyopo Mtaa wa Ntinginya wilayani Nzega mkoani Tabora yenye namba NTC/NMSH/NTI/81.

Mahakama hiyo pia mbele ya Hakimu Hilda Kibona ilimteua Salma Mohammed kuwa msimamizi wa mirathi ya Zainabu Jalakhan ambayo nyumba iliyopo kwenye mirathi ni hiyo hiyo iliyopo mtaa wa Ntinginya wilayani Nzega yenye namba NTC/NMSH/NTI/81.

Hivi karibuni baada ya Mahakama kufanya usuluhishi kwa familia hiyo, iliamuru  aliyeteuliwa kusimamia mirathi, Karim akusanye mali za marehemu.

Hata hivyo, katika nyaraka mbalimbali za nyumba hizo ikiwemo risiti za kodi ya pango iliyowasilishwa mahakamani zinasomeka kwa jina la Zena Jalakhan na si Zainabu Jalakhan.

Karim katika kiapo chake mahakamani alidai marehemu hakuacha wosia na maelezo hayo yaliungwa mkono na wajukuu, Gullam Siager na Haji Seager hivyo mahakama ikamteua kusimamia mirathi hiyo.

Marehemu aliacha nyumba moja iliyopo Mtaa wa Ntinginya, wilayani Nzega yenye namba NTC/NMSH/NTI/81.

Wanafamilia wanufaika katika mirathi hiyo ni wajukuu, Araf Seager, Azaz Seager, Haji Seager, Asha Seager, Gullam Seager, Fatuma Seager, Kasu Seager na Karim Samji ambaye ni mtoto.

Mbowe kusuka au kunyoa kortini kesho

 Mwandishi Wetu,  daimatznews@gmail.com

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kesho Machi 13,2024 'atasuka au kunyoa'. Ndivyo unavyoweza kusema, wakati Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi itakapotoa uamuzi wa shauri alilofungua Mbowe kuwadai gharama waandishi wa habari 10, wanaomdai mtoto wake Dudley.

Leo waandishi wa habari 10 wanaomdai Dudley ambaye ni Mkurugenzi wa Tanzania Daima, Sh milioni 62.7 wameachia nyumba ya Freeman Mbowe waliyoikamata ili kuipiga mnada kufidia deni lao.

Hata hivyo, wamegoma kulipa gharama za kesi zilizoombwa na Mbowe wakieleza sababu hata wao wameingia gharama katika kudai haki yao.

Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi ilisikikiza shauli hilo mbele ya Naibu Msajili, Mary Mrio leo Machi 12,2024 ikieleza itatoa uamuzi kuhusu gharama kesho saa 8 mchana.

Mbowe kupitia Wakili wake John Mallya aliwasilisha maombi chini ya kiapo kilichoapwa na Freeman Mbowe Februari 26 mwaka huu, akitaka wajibu maombi kuondoa nyumba hiyo kwa sababu si mali ya Dudley na Mahakama iwaamuru wajibu maombi hao kumlipa gharama za kesi mteja wake.

Akizungumza kwa niaba ya wajibu maombi wenzake, Kulwa Mzee aliiambia mahakama kwamba walipitia nyaraka zote na viambatanisho husika, wamejiridhisha na kukubaliana kwa pamoja kwamba nyumba waliyoikamata ni ya familia, lakini inamilikiwa na Freeman Mbowe.

"...Tumepitia nyaraka pamoja na viambatanisho ikiwemo hati ya nyumba. Tumejiridhisha kwamba mkurugenzi tunayemdai, Dudley Mbowe si mmiliki. Hivyo, tunaiomba Mahakama tuiondoe nyumba hiyo kwenye maombi yetu," alisema Kulwa na kuongeza:

"Mheshimiwa, kuhusu gharama, kwa uelewa wetu, katika mashauri ya migogoro ya kikazi, hakuna gharama. Hiyo inatokana na uwezo na kipato kidogo cha wafanyakazi;

"Wakati sisi tunafanya jambo hili, tulikuwa tukiamini kabisa kuwa ni nyumba ya mkurugenzi wetu kwa sababu katika hatua ya makubaliano, alikuwa anatuambia kuwa tutafanya vikao nyumbani kwake na tumefanya hapo vikao  kwenye hiyo nyumba," amesema Kulwa.

Ameongeza: "Mheshimiwa katika hatua za mwisho, baba yake ambaye ndiye mwombaji katika shauri hili alitualika tukutane hapo hapo tulipokuwa tukikutana. Tulikutana hapo, akakubali kubeba dhamana ya mtoto wake akakubali kutulipa mwezi Desemba."

Kulwa alidai kutokana na mazingira hayo waliamini kuwa hapo ndipo nyumbani kwake mkurugenzi na baada ya kushindwa kuwalipa katika kutekeleza namna ya kupata haki yao ndio maana waliamua kukamata hiyo nyumba.

"...Mheshimiwa tunaomba tusilipe gharama, kwanza huyu mwombaji hakuingia gharama kwani katika  hatua zote za majadiliano tulikuwa tunakwenda kwake kwa gharama zetu wenyewe na ahadi zake za kutulipa Desemba 2023 ambazo alishindwa kutekeleza hilo lilituathiri, maana tulikuwa katika maandalizi ya siku kuu na  ada za watoto shuleni,"amedai Kulwa.

Aliomba Mahakama katika uamuzi kuhusu gharama ikiwezekana kila upande ubebe gharama zake.

Kwa upande wake, dalali wa Mahakama Jesca Massawe ambaye ni mjibu maombi wa 11, alidai alipokea amri ya Mahakama kwa ajili ya kukamata hiyo nyumba.

"Sisi madalali wa Mahakama katika kutekeleza majukumu yetu, tulikaa na Mahakama hii chini ya Jaji Mfawidhi  akatuelekeza kuwa katika mashauri haya ya kukamata mali tusijihusishe na utambuzi wa mali bali tukamate na kama kuna changamoto basi italetwa mahakamani, " amesema.

Ameongeza kwamba alitekeleza amri ya Mahakama kama ilivyoelekezwa.

Wakili Mallya alijibu hoja hiyo akieleza kwamba anakubaliana na mjibu maombi Kulwa kwa aliyoyasema ya kuachia nyumba hiyo.

Hata hivyo akasema: "Kuhusu suala la gharama, mteja mwombaji anastahili kulipwa gharama na mambo mengine aliyoyasema mjibu maombi alipaswa kuyaleta kwa njia ya kiapo."

Amedai kuhusu hoja za mjibu maombi wa 11 ambaye ni dalali, kweli ni afisa wa Mahakama lakini maelezo yake hayakuja kwenye kiapo. 

"Kwa kuwa anamtaja na Jaji Mfawidhi, haya yalipaswa kuja kwa njia ya kiapo na si maneno matupu mahakamani. Kwa hiyo naiomba Mahakama yako isiyazingatie  na tunaomba mahakama izingatie suala la gharama,"alidai Mallya.

Naibu Msajili Mrio baada ya kusikiliza hoja za pande zote aliahirisha shauri hadi leo saa nane mchana kwa ajili ya uamuzi.

Katika shauri la msingi,  mjibu maombi mwingine Maregesi Paul, aliomba kuyaondoa maombi ya kukamata nyumba hiyo na kuieleza Mahakama kwamba wanatarajia kuwasilisha maombi mengine upya ya kumkamata Dudley.

"Maombi haya yameondolewa kwa kibali cha kuyaleta tena, "alisema Msajili.

Mbowe kafungua shauri dhidi ya Maregesi Paul, Fidelis Felix, Christina Mwakangale, Janeth Josiah, Exuperius Kachenje, Hellen Sisya, Kulwa Mzee, Nora Damian, Makuburi Ally, Mkurugenzi wa Gazeti la Tanzania na Kampuni ya Udalali ya JJ Auctioneers& Debt Collectors.

Februari 13 mwaka huu, Mahakama ilikubali maombi ya wadai na kumteua dalali wa Mahakama kukamata nyumba kwa ajili ya kuipiga mnada.

Februari 28 mwaka huu, dalali wa Mahakama, Jesca Massawe alifanikiwa kubandika matangazo ya kukamata nyumba ya Mkurugenzi tayari kupigwa mnada kufidia deni la malimbikizo ya mishahara wafanyakazi.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Mary Mrio alitoa amri hiyo baada ya kupitia hoja za washinda tuzo katika Tume ya Usuluhishi na Uamuzi(CMA) Julai 2023.

Shauri hilo namba 28461 la mwaka 2023, wadai Maregesi Paul na wenzake tisa dhidi ya Mkurugenzi wa Gazeti la Tanzania Daima, Dudley Mbowe.

Baada ya mdaiwa kukaidi kulipa, wadai  walikubaliana njia sahihi kukamata nyumba yake namba 9 iliyopo Mtaa wa Feza , Mikocheni B barabara ya Chipaka na Mahakama ilikubali.

Walalamikaji hao walipata tuzo Julai 17 mwaka 2023 mbele ya Msuluhidhi wa CMA Ilala,  Bonasia Mollel.

Madai ya awali yalikuwa jumla ya Sh milioni 114 baada ya kukaa mezani kwenye majadiliano kwa pamoja kiwango hicho cha fedha kilishuka na kufikia Sh milioni 62.7.

Dudley alikubali kulipa fedha hizo kwa awamu tatu, Oktoba 30, Desemba 30 mwaka 2023 na awamu ya mwisho ilikuwa mwishoni Februari mwaka huu lakini hakulipa.

Jumapili, 10 Machi 2024

NEEC, wanawake 5000 kumpongeza Rais Samia Dar

Mwandishi Wetu daimanewstz@gmail.com

Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za wanawake nchini wameandaa hafla maalumu ya kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan na kutambua umahiri wake wa kuwa mwanamke kinara kwa masuala ya nishati safi ya kupikia na utunzaji wa mazingira.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam  Machi 9, 2024, Katibu Mtendaji wa  NEEC, BengI Issa hafla hiyo ambayo itahudhuriwa  pia na  Rais Samia itafanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee sambamba na kumpongeza kwa ujasiri na uthubutu wake.

“Hii ni fursa ya kipekee kwa wanawake wa Mkoa wa Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi kwenye  hafla hiyo maalumu ya kutambua kuwa Rais Samia Suluhu ni mwanamke kinara wa masuala ya nishati safi ya kupikia na utunzaji wa mazingira,” amesema.

Issa amesema Rais Samia kwa ujasiri wake, mbali ya kuwa mwanamke kinara kwenye masuala nishati safi ya kupikia na utunzaji wa mazingira nchini, amefanikiwa kuifungua nchi katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa pia.

“NEEC inatambua na kuheshimu mchango wa Rais Samia katika kuwawezesha wanawake kutoka kwenye mazingira magumu ya nishati ya kupikia, ikiwemo mkaa na kuni ambavyo  vimekuwa vikileta  madhara kwa afya ya binadamu na  mazingira. Tunaamini mpango huo utaleta  matokeo chanya kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla wake,” amesema Bi. Issa.

Amefafanua kwamba kupitia mpango huo, Rais Samia anatarajiwa kwenda Ufarasa kuongoza kikao kitakachowakutanisha marais wa dunia, wakilenga  kumuunga mkono na kuja na mikakati itakayowezesha kukamilisha mpango utakaokuwa mwarobaini wa nishati safi ya kupikia na rafiki kwa mazingira nchini.

Amebainisha kuwa Baraza hilo lina jumla ya  majukwaa  ya uwezeshaji  3,500 katika ngazi ya mtaa, vijiji, kata, wilaya, mikoa mpaka  ngazi ya kitaifa,  lengo likiwa kuwaleta wanawake  wote pamoja  na kujadili na kuibua fursa  mbalimbali za kiuchumi na kutoa mchango kwa  maendeleo ya taifa.

“Majukwaa yote hapa  nchini yaende na kasi  ya Mheshimimiwa Rais Samia ya kujielekeza  kwenye matumizi ya nishati safi.  Tuone kwamba hii ni fursa ambayo kila mwanamke wa kitanzania anatakiwa kuichangamkia sanjari na kuandaa miradi pia kubuni rasilimali  zitakazoendana na utunzaji wa mazingira,” amesema.  

Hafla hiyo  inatarajiwa kuwakutanisha wanawake  zaidi ya  5,000 kutoka  makundi mbalimbali  ya wanawake nchini  yakiwamo  majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi,  wanawake kutoka vyama vya utafiti na wanawake kutoka vyama vya makandarasi Tanzania.

 Mengine ni waandishi wa habari wanawake, wanawake kutoka kwenye vikoba, wanawake kutoka vyama vya kilimo na vyama vya utafiti.

Jumamosi, 9 Machi 2024

Chongolo arejea kivingine

 -Aendelea kuaminiwa kuitumikia CCM

Exuperius Kachenje, daimanewstz@gmail.com

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo, amerejea madarakani kwa namna nyingine, safari hii akiteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe. 

Uteuzi wa Chongolo umefanywa na Rais Dk.Samia Suluhu Hassan leo na kutangazwa na Katibu Mkuu Kiongozi,Balozi Dk. Moses Kusiluka.

Taarifa hiyo ya Katibu Mkuu Kiongozi, umetaja pia wateule wengine na ukuu wa mkoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri, sanjari na uhamisho wa watendaji wa nafasi hizo.

Chongolo anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe kutoka nafasi ya ukatibu mkuu wa CCM, aliyojiuzulu Novemb mwaka 2023 kwa kilichoelezwa ni kutokana na kuchafuliwa mtandaoni, jambo ambalo Rais Samia alisema linachunguzwa.

Hata hivyo, uteuzi huo unaweza kuelezwa kwamba Rais amejiridhisha na usafi wa Chongolo, ambaye alibeba jukumu la kuwajibika baada ya kuchafuliwa. 

Unaweza kuelezwa pia ni wa kimkakati, utakaomfanya Chongolo aendelee kuitumikia CCM, akiwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe akimwakilisha Rais na Mwenyekiti wa CCM Taifa, ambaye ni Rais Samia Suluhu Hassan.

Ikumbukwe kuwa nafasi ya ukatibu mkuu wa CCM imechukuliwa na Balozi Emanuel  Nchimbi, huku Chongolo akichukua nafasi ya Dk.Francis Michael.

Zaidi, soma orodha ya wateule wapya na wanaohamishwa hapa chini.









Ijumaa, 8 Machi 2024

ACT yataka kuwakutanisha Rais Samia, Dk.Mwinyi Z'bar

 Makuburi Ally

CHAMA cha ACT Wazalendo kinatarajia kuwakutanisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali ikiwamo nia ya chama hicho kujitoa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (GNU).

Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu  amesema hayo leo Machi 8,2024 mbele ya waandishi wa habari akieleza kwamba hatua hiyo ni zao la kikao cha Halmashauri Kuu Taifa ya ACT Wazalendo iliyokutana Machi 4 mwaka huu, makao makuu ya chama hicho, Magomeni jijini Dar es Salaam.

Amesema uwepo wa GNU ni utulivu wa kiuchumi, utalii, mikopo, biashara na kwamba roho ya uchumi wa Zanzibar inategemea utulivu.

"Kikao cha Halmashauri Kuu Taifa kilifanya tafakuri ya kina juu ya mwenendo na mwelekeo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar," amesema Shaibu.

Amebainisha kuwa Serikali hiyo ni matakwa kisheria kwa hoja tatu ambazo ni kuachiwa huru kwa viongozi wote wa ACT walioshikiliwa, watuhumiwa hao ni lazima wafidiwe sambamba na mageuzi ya kimfumo na usimamizi wa uchaguzi.

Mwisho

Diamond ajipeleka BRELA

-Aelimishwa kuhusu ulinzi wa kazi zake

 Mwandishi Wetu, daimanewstz@gmail.com

Mwanamuziki wa kizazi kipya, Naseeb Abdul maarufu Diamond Platnumz ametembelea Ofisi za BRELA jijini Dar es Salaam Machi 7, 2024, ambapo amekutana na kuzungumza na  Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Godfrey Nyaisa ambapo alipata elimu kuhusu ulinzi wa kazi na chapa zake . 

Akizunguza baada ya mkutano wake na Nyaisa, Diamond amesema mbali na kuwa mwanamuziki yeye ni mfanyabiashara na mwekezaji ambaye hutengeneza na kuanzisha chapa na kuwainua vijana ili kujipatia kipato hivyo BRELA hawezi kupakwepa kwa kuwa yeye ni mfanyabiashara.

Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa (Kulia), akimkabishi nyaraka nyota wa muziki nchini na mkurugenzi wa Wasafi Media, Diamond Platnums, wakati alipotembelea ofisi za BRELA makao makuu Machi 7, 2024.

 “Nilipokutana  na Nyaisa naye kujitambulisha kwangu alinieleza kwamba BRELA panafaa kuwa  nyumbani kwangu kwa sababu nina chapa tofauti, hivyo patanisaidia katika kusajili kazi zangu ili nisipoteze haki,"amesema Diamond na kufafanua:

"Maneno hayo yalikuwa na maana kubwa katika maisha yangu na hapo ndipo nilipobadilisha mtazamo na kugundua vijana wengi wanapoteza haki zao.” 

Diamond ameonya kuwa wasanii, wanamichezo, vijana na yeyote mwenye lengo la kufika mbali kimaendeleo, hawezi kufanikiwa iwapo hajarasimisha biashara yake BRELA na ili kuwa rasmi unahitaji kusajili jina la biashara, kusajili kampuni na kufuata taratibu mbalimbali zilizowekwa na serikali kama njia nzuri  zitakazolinda na kuwezesha vijana kufika mbali. 

Amesisitiza kuwa ni vyema kwa wasanii na vijana kujitahidi kurasimisha na kulinda alama za biashara,huduma na vumbuzi zao BRELA ili kulinda ndoto zao kwa sababu mtu akianzisha jambo na likawa kubwa, ukigundua kuna mtu mwingine anatumia alama hiyo, kama yeye amewahi kuisajili kisheria, anaweza kukupeleka katika vyombo vya sheria.  

“Kwa watu wanaotumia brand zetu pasipokuwa na haki halali, naelewa kibinadamu atakuwa anatafuta riziki, lakini nawashauri waache ili baadae wasinilaumu  kwa sababu sheria itafuata mkondo wake. Lakini kwa kipindi hiki tumeamua kuwa makini zaidi katika biashara," amesisitiza Diamond.

Amehitimisha kwa kusema kuwa sasa amegundua umuhimu wa sajili na amefanikiwa kuchukua hatua ya kulinda haki zake BRELA, baada ya kufahamu kwa kina faida zake hivyo kuepuka hasara kubwa ambayo angeipata na kupelekea kupoteza Pato la Taifa.

Alhamisi, 7 Machi 2024

Dk.Kijaji awaita BRELA wanawake wajasiriamali

Mwandishi Wetu, daimanewstz@gmail.com

Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Ashatu Kijaji amewataka wajasiriamali wanawake wanaoendesha biashara zao sokoni kurasimisha biashara zao na kuzisajili kwa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA).

Amesema hilo litaziongezea thamani na kulinda bunifu zao na kuwawezesha kunufaika nazo kiuchumi.


Dk. Kijaji ametoa rai hiyo katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa, leo Machi 7, 2024 ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Machi 8 kila mwaka.

Hafla hiyo iliandaliwa na Wanawake wa Masokoni wa Mkoa wa Dar es Salaam (WOMEN TAPO) katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam.

Afisa Mtendaji Mkuu huyo wa BRELA amewataka wanawake wajasiriamali hao kuacha kuendesha biashara  kienyeji, huku akiwaeleza faida watakazopata kwa kusajili biashara na vumbuzi zao.

“Niwahakikishie kuwa BRELA inazipa ulinzi wa kisheria biashara na bunifu iwapo mtu yeyote ataiga kazi yako, kwa wewe mwanamke mjasiriamali uliye na usajili wa BRELA una haki ya kushtaki mahakamani na Wakala itasimama kukutetea kuwa hiyo ni mali yako” ameeleza Nyaisa.

Amewasisitizia umuhimu wa kuongeza thamani bidhaa wanazozalisha kwa kuweka alama ya biashara ili kutambulika kwa haraka katika masoko na kuzitofautisha na bidhaa zingine. 


Ameongeza kuwa mbali ya kupata ulinzi wa kisheria pia watapata fursa ya kukopesheka katika Taasisi rasmi za Kifedha ambako moja ya masharti lazima uwe umesajili biashara yako BRELA badala ya kuchukua mikopo umiza.

Jumatano, 6 Machi 2024

Utafiti: Akili bandia hubashiri kifo kwa usahihi

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Utafiti mpya wa kisayansi ubebaini kuwa mfumo wa akili bandia (AI), una uwezo mkubwa wa kubashiri kifo cha binadamu kwa usahihi pamoja na kubainisha hatari za kutokea vifo vya mapema.

Mfumo huo wa akili bandia uliowezeshwa na historia za mamilioni ya watu na takwimu, una kiwango kikubwa cha usahihi katika kutabiri maisha na uwezekano wa vifo kutokea kuliko mifumo yote iliyopo sasa. Wanasayansi kutoka Technical University of Denmark (DTU), wamebainisha.

Jarida la Computational Science

Katika utafiti wao, wanasayansi hao walitumia takwimu za soko la ajira na afya zaidi ya milioni sita zilizokusanywa kati ya mwaka 2008 na 2020, zilizojumuisha taarifa za mtu mmoja mmoja, elimu, alivyokwenda kutibiwa hospitali na matokeo ya vipimo, kipato na shughuli wanazofanya.

Wanasayansi hao walibadili takwimu hizo kuwa katika maneno ili kufundisha lugha ya kisayansi iitwayo “life2vec” inayoelezwa ni sawa na mifumo ya teknolojia ya akili bandia  kama ule wa ChatGPT.

Kwa mujibu wa utafiti huo uliochapichwa katika Jarida la Nature Computational Science hivi karibuni,  mara akili bandia inapofundishwa na kuelewa takwimu hizo, huzalisha mfumo bora zaidi unaoweza kuchambua kuhusu mtu binafsi  na kutoa majibu yenye usahihi kwa kiwango kikubwa cha usahihi kuonyesha muda atakaokufa.

Watafiti hao walichukua takwimu kutoka kikundi cha watu weny umri wa miaka 35 hadi 65 na nusu kati ya hao tayari wamefariki kati ya mwaka 2016 na 2020, ambapo akili bandia iliulizwa kati ya hao yupi aliye hai na aliyefariki. 

Majibu ya mfumo huo wa akili bandia ulitoa majibu sahihi kwa asilimia 11 zaidi ya mifumo iliyopo sasa hata mifumo inayotumika  na kampuni za bima kupanga bei na miongozo ya sera. 

“ Jambo muhimu la kushangaza hapa ni maisha ya watu kama mfululizo wa matukio, sawa na sentesi inavyoundwa na maneno yanayofuatana,” amesema mtafiti Sune Lehman wa chuo kikuu DTU na kuongeza:

Mtafiti, Sune Lehmann
“ Kwa kawaida hii ni kazi ambayo mtendaji huitumia katika akili bandia, lakini katika mjaribio yetu, huwatumia kuchambua kitu tunachoita mpangilio wa matukio yanayotokea katika maisha ya watu.”

Hata hivyo, wanasayansi hao wameonya kuwa mfumo huo haufai kutumika katika bima za afya kwa mujibu wa taratibu za kimaadili.

Jumamosi, 2 Machi 2024

BRELA yazipa makali taasisi za kuchunguza uhalifu

-Ni kuhusu kuzuia uhalifu umiliki manufaa

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imetoa mafunzo ya kutambua wamiliki manufaa wa kampuni na Majina ya Biashara kwa taasisi za uchunguzi.

Kwa mujibu wa BRELA lengo la mafunzo hayo yaliyofanyika jijini Arusha Februari 25, 2924 ni kurahisha utekelezaji wa majukumu ya taasisi hizo kuzuia na kupambana na uhalifu wa kifedha. 

Kaimu Mkurugenzi wa Makampuni na Majina ya Biashara wa BRELA, Isdori Nkindi akitoa mafunzo kwa Taasisi za Uchunguzi juu ya namna ya kutambua mmiliki manufaa wa Kampuni na Majina ya Biashara, jijini Arusha Februari 24,2024.

Kaimu Mkurugenzi wa Makampuni na Majina ya Biashara BRELA, Isdor Nkindi ameeleza hayo akibainisha kuwa, Wakala yake imekasimiwa na Serikali pendekezo namba 24 kati ya mapendekezo 40 ya Kikosikazi cha Kushughulika na Makosa ya Uhalifu wa Kifedha Ulimwenguni (FATIF), linalohimiza uwazi katika makampuni, hivyo ni jukumu lao kuzijengea uwezo taasisi hizo za kuzuia na kupambana na uhalifu wa kifedha.

“Kutokana na jukumu hilo, kila nchi mshirika inawajibika kuwajengea uwezo na miundombinu wadau wake kwa ajili ya kukabiliana na makosa kama hayo, hivyo ni muhimu kukutana na taasisi zinazoshughulika na uhalifu, ili tuweze kuzungumza lugha moja, kwenye dalili za uhalifu hata kabla ya kutokea, ili uweze kudhibitiwa,”amesema Nkindi.

Ametoa wito kwa kila taasisi kutimiza wajibu wake na kwamba BRELA ikishakamilisha kufanya sajili, taasisi kama TAKUKURU na Polisi waende kuchukua taarifa hizo pindi viashiria vya uhalifu vinapojitokeza, ili kuzuia uhalifu usitokee. 

Kwa mujibu wa sheria, BRELA ndio yenye jukumu la kufanya sajili za makampuni na majina ya biashara, ikiwa pia wamiliki wa kanzidata za makampuni, hivyo endapo kutakua na kiashiria cha uhalifu kiweze kushughulikiwa.   

Washiriki wa kikao kazi kuhusu Dhana ya Wamiliki Manufaa  iliyotolewa na BRELA kwa wadau, wakiwemo mawakili na wafanya biashara jijini Arusha, wakifuatilia mafunzo hayo mapema Februari 27, 2024.


Katika mafunzo hayo, Nkindi amezitaka  taasisi hizo kufuata utaratibu wa kuomba taarifa kupitia mamlaka zao, badala ya mtumishi mmoja mmoja kuomba pekee yake.

 Mafunzo hayo yaliyofanyika kwa siku moja yamehudhuriwa na taasisi saba zikiwemo, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Polisi, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Uhamiaji, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Mahakama ya Tanzania.

Ijumaa, 1 Machi 2024

Mawakili watakiwa kuwaibua wahalifu wa fedha

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Mawakili na Wafanyabiashara nchini, wametakiwa kuwaibua wote watakaobainika kujihusisha na vitendo vya uhalifu wa kifedha kwa kuwa vinakwamisha maendeleo ya Taifa.

Rai hiyo imetolewa leo Machi mosi mjini Arusha na Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa huo anayesimamia  Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Frank Mmbando aliyezungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, wakati akifungua kikao kazi kati ya BRELA na Wadau Jijini Arusha. 

Washiriki wa kikao kazi kuhusu Dhana ya Wamiliki Manufaa  iliyotolewa na BRELA kwa wadau wakiwemo Mawakili na Wafanyabiashara Jijini Arusha, wakifuatilia mafunzo hayo mapema Februari 27,2024.

“Serikali inatambua kuwepo kwa changamoto za taarifa za baadhi ya wamiliki wa kampuni wanaoweza kutumia kampuni zao kukwepa kodi, kupitisha fedha haramu, kujihusisha na ufadhili wa vitendo vya ugaidi na ndio maana BRELA ilikutana na wawakilishi wa Taasisi za Uchunguzi na Mamlaka za Udhibiti ili kushauriana jinsi ya kukabiliana na changamoto hii, ambayo inaleta taswira isiyo nzuri kwa wafanyabiashara nchini.”amesema Mmbando.

Ameongeza: "Nawapongeza BRELA kwa kuona umuhimu mkubwa wa kutoa elimu baada ya  mabadiliko ya Sheria ya Fedha ya Mwaka 2020, iliyopitisha marekebisho kwenye Sheria ya Kampuni Sura 212 pamoja na Kanuni za Wamiliki Manufaa wa Kampuni na Kanuni za Majina ya Biashara (Umiliki Manufaa) za Mwaka 2023 pia kanuni zake kupitishwa na Waziri mwenye dhamana na biashara nchini."

Amewaomba mawakili na wafanyabiashara hao waendelee kuwa mabalozi wazuri na kuwa jicho la Serikali kwa kusaidia kuwaibua wote watakaobainika kujihusisha na vitendo kama hivyo kwani vitendo hivyo vinakwamisha maendeleo ya Taifa.

Mmbando pia ametoa rai kwa waandishi wa habari waliohudhuria warsha hiyo kutumia vyombo vyao kusaidia kufikisha elimu kuhusu dhana ya Wamiliki Manufaa ili wadau na wananchi wote waielewe na na kuitii.                                                          

Washiriki wa mafunzo kwa Taasisi za Uchunguzi wakiwa katika picha za pamoja wakati wa mafunzo ya namna ya kutambua Mmiliki Manufaa wa Kampuni na Majina ya Biashara, ili kupunguza uhalifu wa kifedha  Jijini Arusha.

Pamoja na warsha hiyo, BRELA imefanya Kliniki ya siku tatu ya wafanyabiashara katika eneo la Stendi Kuu ya mabasi ili kutoa msaada wa usajili na elimu wezeshi kwa watakaokuwa wanahitaji huduma hiyo ambapo amewaomba wananchi kufika ili kupata huduma hizo muhimu.