Hot Posts

6/recent/ticker-posts

Wachambua miaka 3 ya Dk. Samia, waishauri

 Hellen Ngoromera, daimatznews@gmail.com

Miaka mitatu ya Rais Samia Suluhu Hassan madakani imetajwa kuimarisha na kukuza demokrasia nchini, huku wasomi wakiishauri Serikali kuboresha maisha ya wananchi kiuchumi.

Rais Samia ametimiza miaka mitatu madarakani tangu alipotwaa madaraka ya kuiongoza Tanzania Machi 19, 2021, kufuatia kifo cha mtangulizi wake, Rais John Magufuli Machi 17,2021.

Rais Dk. Samia Suluhu Hassan

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana Machi  26 katika mjadala wa uchambuzi wa miaka mitatu ya uongozi wa Rais Samia madarakani ulioandaliwa na Kampuni ya Mchambuzi Media, Mchambuzi wa masuala ya kisiasa Dk. Denis Muchunguzi na Profesa Samuel Wangwe wameeleza hayo.

"Napongeza miaka mitatu ya  Dk. Samia kwani amefanya makubwa... tumeshuhudia mikutano ya kisiasa ikiruhusiwa, maandamano ya Chadema kwenda Umoja wa Ulaya yalifanyika bila bugudha," amesema Dk. Muchunguzi.

Ameongeza kuwa katika miaka mitatu hiyo hata baadhi ya watu wakiwemo wanasiasa waliohama nchini kutokana  na  sababu mbalimbali walirejea nchini.

Dk. Muchunguzi ametaja jambo jingine kuwa ni pamoja na  kuruhusiwa kwa mitandao ya kijamii ambayo ilipigwa marufuku, huku akishauri vyama vya siasa kuwa imara na madhubuti kifedha viweze kujiendesha vyema.

"Vyama vya siasa viwe imara kifedha, hatuhitaji kuona vyama vinakufa," amesema Dk. Muchunguzi.

 Kwa upande wake, Profesa Samuel Wangwe aliyechangia mada ya Uchumi na Miradi ya Maendeleo, ameshauri Serikali kuboresha maisha ya wananchi ili kuwakwamua kiuchumi.

Profesa Wangwe amesema katika kipindi cha miaka mitatu ya Rais Samia madarakani, ameweze kuinua uchumi na kufikia asilimia 5.2 na kwamba ana imani  kiwango cha ukuaji wake kitaongezeka kwa mwaka huu.

Chapisha Maoni

0 Maoni