Mwandishi Wetu, daimanewstz@gmail.com
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Ashatu Kijaji amewataka wajasiriamali wanawake wanaoendesha biashara zao sokoni kurasimisha biashara zao na kuzisajili kwa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA).
Amesema hilo litaziongezea thamani na kulinda bunifu zao na kuwawezesha kunufaika nazo kiuchumi.
Dk. Kijaji ametoa rai hiyo katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Godfrey Nyaisa, leo Machi 7, 2024 ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani Machi 8 kila mwaka.
Hafla hiyo iliandaliwa na Wanawake wa Masokoni wa Mkoa wa Dar es Salaam (WOMEN TAPO) katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam.
Afisa Mtendaji Mkuu huyo wa BRELA amewataka wanawake wajasiriamali hao kuacha kuendesha biashara kienyeji, huku akiwaeleza faida watakazopata kwa kusajili biashara na vumbuzi zao.
“Niwahakikishie kuwa BRELA inazipa ulinzi wa kisheria biashara na bunifu iwapo mtu yeyote ataiga kazi yako, kwa wewe mwanamke mjasiriamali uliye na usajili wa BRELA una haki ya kushtaki mahakamani na Wakala itasimama kukutetea kuwa hiyo ni mali yako” ameeleza Nyaisa.
Amewasisitizia umuhimu wa kuongeza thamani bidhaa wanazozalisha kwa kuweka alama ya biashara ili kutambulika kwa haraka katika masoko na kuzitofautisha na bidhaa zingine.
Ameongeza kuwa mbali ya kupata ulinzi wa kisheria pia watapata fursa ya kukopesheka katika Taasisi rasmi za Kifedha ambako moja ya masharti lazima uwe umesajili biashara yako BRELA badala ya kuchukua mikopo umiza.
0 Maoni