Hot Posts

6/recent/ticker-posts

Mawakili watakiwa kuwaibua wahalifu wa fedha

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Mawakili na Wafanyabiashara nchini, wametakiwa kuwaibua wote watakaobainika kujihusisha na vitendo vya uhalifu wa kifedha kwa kuwa vinakwamisha maendeleo ya Taifa.

Rai hiyo imetolewa leo Machi mosi mjini Arusha na Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa huo anayesimamia  Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Frank Mmbando aliyezungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha, wakati akifungua kikao kazi kati ya BRELA na Wadau Jijini Arusha. 

Washiriki wa kikao kazi kuhusu Dhana ya Wamiliki Manufaa  iliyotolewa na BRELA kwa wadau wakiwemo Mawakili na Wafanyabiashara Jijini Arusha, wakifuatilia mafunzo hayo mapema Februari 27,2024.

“Serikali inatambua kuwepo kwa changamoto za taarifa za baadhi ya wamiliki wa kampuni wanaoweza kutumia kampuni zao kukwepa kodi, kupitisha fedha haramu, kujihusisha na ufadhili wa vitendo vya ugaidi na ndio maana BRELA ilikutana na wawakilishi wa Taasisi za Uchunguzi na Mamlaka za Udhibiti ili kushauriana jinsi ya kukabiliana na changamoto hii, ambayo inaleta taswira isiyo nzuri kwa wafanyabiashara nchini.”amesema Mmbando.

Ameongeza: "Nawapongeza BRELA kwa kuona umuhimu mkubwa wa kutoa elimu baada ya  mabadiliko ya Sheria ya Fedha ya Mwaka 2020, iliyopitisha marekebisho kwenye Sheria ya Kampuni Sura 212 pamoja na Kanuni za Wamiliki Manufaa wa Kampuni na Kanuni za Majina ya Biashara (Umiliki Manufaa) za Mwaka 2023 pia kanuni zake kupitishwa na Waziri mwenye dhamana na biashara nchini."

Amewaomba mawakili na wafanyabiashara hao waendelee kuwa mabalozi wazuri na kuwa jicho la Serikali kwa kusaidia kuwaibua wote watakaobainika kujihusisha na vitendo kama hivyo kwani vitendo hivyo vinakwamisha maendeleo ya Taifa.

Mmbando pia ametoa rai kwa waandishi wa habari waliohudhuria warsha hiyo kutumia vyombo vyao kusaidia kufikisha elimu kuhusu dhana ya Wamiliki Manufaa ili wadau na wananchi wote waielewe na na kuitii.                                                          

Washiriki wa mafunzo kwa Taasisi za Uchunguzi wakiwa katika picha za pamoja wakati wa mafunzo ya namna ya kutambua Mmiliki Manufaa wa Kampuni na Majina ya Biashara, ili kupunguza uhalifu wa kifedha  Jijini Arusha.

Pamoja na warsha hiyo, BRELA imefanya Kliniki ya siku tatu ya wafanyabiashara katika eneo la Stendi Kuu ya mabasi ili kutoa msaada wa usajili na elimu wezeshi kwa watakaokuwa wanahitaji huduma hiyo ambapo amewaomba wananchi kufika ili kupata huduma hizo muhimu.

Chapisha Maoni

0 Maoni