Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
MAHAKAMA ya Mwanzo Nzega imeendelea kulipiga kalenda shauri la Mirathi ya Zena Jalakhan lenye mvutano wa ndugu katika kusimamia mirathi hiyo.
Shauri hilo lipo mbele ya Hakimu Mfawidhi, Abunas Sonyo, ambapo jana liliahirishwa kwa mara nyingine hadi Aprili 23 kwa ajili ya kusikiliza pingamizi.
Mmoja wa wanafamilia, Salma Mohammed katika shauri hilo anayewakilishwa na Wakili Kaumuliza David awali aliomba apewe muda wa kupitia jalada la shauri hilo la mirathi na mahakama ilikubali maombi hayo.
Lakini jana, shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kusikiliza mapingamizi, lakini upande wa Karim Samji ambaye awali aliyekuwa msimamizi wa mirathi, aliomba shauri lisiendelee kwa sababu wakili wao hakuwepo mahakamani.
Karim alidai Wakili wao hakuwepo kwa sababu hakujua mahakamani shauri linaloendelea ni lipi na baada ya Mahakama kuwafahamisha kwamba kinachoendelea ni usikilizwaji wa mapingamizi, waliomba kuahirisha.
Wakili Kaumuliza aliomba Mahakama iahirishe shauri hilo hadi April 23 mwaka huu na hata upande wa pili walipohoji muda ni mrefu, bado wakili aliomba iwe tarehe hiyo kwani ndio atakuwa na nafasi.
Shauri hilo lenye mvutano, upande wa pili wa Salma wanapinga Karim Samji aliyeteuliwa na Mahakama kusimamia mirathi ya Zena kutekeleza amri ya Mahakama ya kukusanya mali za marehemu.
Salma Mohammed alifungua shauri la mirathi ya Zainabu Jalakhan kwa mali ambayo ni nyumba iliyopo pia katika mirathi ya Zena Jalakhan, huku mahakama ikiwa ilishamteua Karim kuwa msimamizi.
Mwombaji Salma aliwasilisha hoja tatu, akidai kwamba shauri linalomuhusu marehemu lilikwisha sikilizwa na kutolewa uamuzi katika shauri la mirathi namba 24/2023.
Hoja ya pili mali iliyotajwa katika maombi hayo ilikwishaorodheshwa katika mirathi namba 24/2023 mbele ya Hakimu Hilda Kibona.
Katika hoja ya mwisho ni kwamba shauri hilo lenye viini hivyo lilishasikilizwa na kuamuliwa na mahakama hiyo hivyo aliomba maombi ya mirathi namba 35 ya mwaka jana ya mali ya Zena Jalakhan, ambayo mahakama ilimteua Karim kuwa msimamizi yatupiliwe mbali.
Awali Mahakama hiyo mbele ya Hakimu Sonyo ilimteua Karim kuwa msimamizi wa mirathi ya mali ya marehemu Zena ambayo ni nyumba iliyopo Mtaa wa Ntinginya wilayani Nzega mkoani Tabora yenye namba NTC/NMSH/NTI/81.
Mahakama hiyo pia mbele ya Hakimu Hilda Kibona ilimteua Salma Mohammed kuwa msimamizi wa mirathi ya Zainabu Jalakhan ambayo nyumba iliyopo kwenye mirathi ni hiyo hiyo iliyopo mtaa wa Ntinginya wilayani Nzega yenye namba NTC/NMSH/NTI/81.
Hivi karibuni baada ya Mahakama kufanya usuluhishi kwa familia hiyo, iliamuru aliyeteuliwa kusimamia mirathi, Karim akusanye mali za marehemu.
Hata hivyo, katika nyaraka mbalimbali za nyumba hizo ikiwemo risiti za kodi ya pango iliyowasilishwa mahakamani zinasomeka kwa jina la Zena Jalakhan na si Zainabu Jalakhan.
Karim katika kiapo chake mahakamani alidai marehemu hakuacha wosia na maelezo hayo yaliungwa mkono na wajukuu, Gullam Siager na Haji Seager hivyo mahakama ikamteua kusimamia mirathi hiyo.
Marehemu aliacha nyumba moja iliyopo Mtaa wa Ntinginya, wilayani Nzega yenye namba NTC/NMSH/NTI/81.
Wanafamilia wanufaika katika mirathi hiyo ni wajukuu, Araf Seager, Azaz Seager, Haji Seager, Asha Seager, Gullam Seager, Fatuma Seager, Kasu Seager na Karim Samji ambaye ni mtoto.
0 Maoni