Hot Posts

6/recent/ticker-posts

BRELA yazipa makali taasisi za kuchunguza uhalifu

-Ni kuhusu kuzuia uhalifu umiliki manufaa

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), imetoa mafunzo ya kutambua wamiliki manufaa wa kampuni na Majina ya Biashara kwa taasisi za uchunguzi.

Kwa mujibu wa BRELA lengo la mafunzo hayo yaliyofanyika jijini Arusha Februari 25, 2924 ni kurahisha utekelezaji wa majukumu ya taasisi hizo kuzuia na kupambana na uhalifu wa kifedha. 

Kaimu Mkurugenzi wa Makampuni na Majina ya Biashara wa BRELA, Isdori Nkindi akitoa mafunzo kwa Taasisi za Uchunguzi juu ya namna ya kutambua mmiliki manufaa wa Kampuni na Majina ya Biashara, jijini Arusha Februari 24,2024.

Kaimu Mkurugenzi wa Makampuni na Majina ya Biashara BRELA, Isdor Nkindi ameeleza hayo akibainisha kuwa, Wakala yake imekasimiwa na Serikali pendekezo namba 24 kati ya mapendekezo 40 ya Kikosikazi cha Kushughulika na Makosa ya Uhalifu wa Kifedha Ulimwenguni (FATIF), linalohimiza uwazi katika makampuni, hivyo ni jukumu lao kuzijengea uwezo taasisi hizo za kuzuia na kupambana na uhalifu wa kifedha.

“Kutokana na jukumu hilo, kila nchi mshirika inawajibika kuwajengea uwezo na miundombinu wadau wake kwa ajili ya kukabiliana na makosa kama hayo, hivyo ni muhimu kukutana na taasisi zinazoshughulika na uhalifu, ili tuweze kuzungumza lugha moja, kwenye dalili za uhalifu hata kabla ya kutokea, ili uweze kudhibitiwa,”amesema Nkindi.

Ametoa wito kwa kila taasisi kutimiza wajibu wake na kwamba BRELA ikishakamilisha kufanya sajili, taasisi kama TAKUKURU na Polisi waende kuchukua taarifa hizo pindi viashiria vya uhalifu vinapojitokeza, ili kuzuia uhalifu usitokee. 

Kwa mujibu wa sheria, BRELA ndio yenye jukumu la kufanya sajili za makampuni na majina ya biashara, ikiwa pia wamiliki wa kanzidata za makampuni, hivyo endapo kutakua na kiashiria cha uhalifu kiweze kushughulikiwa.   

Washiriki wa kikao kazi kuhusu Dhana ya Wamiliki Manufaa  iliyotolewa na BRELA kwa wadau, wakiwemo mawakili na wafanya biashara jijini Arusha, wakifuatilia mafunzo hayo mapema Februari 27, 2024.


Katika mafunzo hayo, Nkindi amezitaka  taasisi hizo kufuata utaratibu wa kuomba taarifa kupitia mamlaka zao, badala ya mtumishi mmoja mmoja kuomba pekee yake.

 Mafunzo hayo yaliyofanyika kwa siku moja yamehudhuriwa na taasisi saba zikiwemo, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Polisi, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Uhamiaji, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka na Mahakama ya Tanzania.

Chapisha Maoni

0 Maoni