Mwandishi Wetu daimanewstz@gmail.com
Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali za wanawake nchini wameandaa hafla maalumu ya kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan na kutambua umahiri wake wa kuwa mwanamke kinara kwa masuala ya nishati safi ya kupikia na utunzaji wa mazingira.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Machi 9, 2024, Katibu Mtendaji wa NEEC, BengI Issa hafla hiyo ambayo itahudhuriwa pia na Rais Samia itafanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee sambamba na kumpongeza kwa ujasiri na uthubutu wake.
“Hii ni fursa ya kipekee kwa wanawake wa Mkoa wa Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi kwenye hafla hiyo maalumu ya kutambua kuwa Rais Samia Suluhu ni mwanamke kinara wa masuala ya nishati safi ya kupikia na utunzaji wa mazingira,” amesema.
Issa amesema Rais Samia kwa ujasiri wake, mbali ya kuwa mwanamke kinara kwenye masuala nishati safi ya kupikia na utunzaji wa mazingira nchini, amefanikiwa kuifungua nchi katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa pia.
“NEEC inatambua na kuheshimu mchango wa Rais Samia katika kuwawezesha wanawake kutoka kwenye mazingira magumu ya nishati ya kupikia, ikiwemo mkaa na kuni ambavyo vimekuwa vikileta madhara kwa afya ya binadamu na mazingira. Tunaamini mpango huo utaleta matokeo chanya kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla wake,” amesema Bi. Issa.
Amefafanua kwamba kupitia mpango huo, Rais Samia anatarajiwa kwenda Ufarasa kuongoza kikao kitakachowakutanisha marais wa dunia, wakilenga kumuunga mkono na kuja na mikakati itakayowezesha kukamilisha mpango utakaokuwa mwarobaini wa nishati safi ya kupikia na rafiki kwa mazingira nchini.
Amebainisha kuwa Baraza hilo lina jumla ya majukwaa ya uwezeshaji 3,500 katika ngazi ya mtaa, vijiji, kata, wilaya, mikoa mpaka ngazi ya kitaifa, lengo likiwa kuwaleta wanawake wote pamoja na kujadili na kuibua fursa mbalimbali za kiuchumi na kutoa mchango kwa maendeleo ya taifa.
“Majukwaa yote hapa nchini yaende na kasi ya Mheshimimiwa Rais Samia ya kujielekeza kwenye matumizi ya nishati safi. Tuone kwamba hii ni fursa ambayo kila mwanamke wa kitanzania anatakiwa kuichangamkia sanjari na kuandaa miradi pia kubuni rasilimali zitakazoendana na utunzaji wa mazingira,” amesema.
Hafla hiyo inatarajiwa kuwakutanisha wanawake zaidi ya 5,000 kutoka makundi mbalimbali ya wanawake nchini yakiwamo majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi, wanawake kutoka vyama vya utafiti na wanawake kutoka vyama vya makandarasi Tanzania.
Mengine ni waandishi wa habari wanawake, wanawake kutoka kwenye vikoba, wanawake kutoka vyama vya kilimo na vyama vya utafiti.
0 Maoni