Spika wa Bunge Mstaafu, Anne Makinda amewataka wanasiasa kutofurahia tu matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, badala yake watambue kuwa inaweza kuwa kiboko kwao.
Makinda ambaye pia ni Kamisaa wa Sensa nxhini, ametoa kauli hiyo leo Machi13,2024 jijini Dar es Salaam alipokuwa mgeni rasmi katika mafunzo ya waandishi wa habari, kuhusu matumizi ya takwimu za sensa ikiwa ni sehemu ya awamu ya tatu ya utekelezaji Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.
"Tumewaambia wanasiasa wenzagu, sensa hii imefanikiwa. Lakini, kwenu ni kiboko, shangilieni lakini watu watakuwa wanauliza maswali kutokana na takwimu na maelezo yaliyomo kwenye matokeo ya sensa. Sisi tunafundisha mpaka chini kwa wananchi," amesema Makinda.
Spika mstaafu huyo, ametoa onyo hilo kwa wanasiasa wakati ambapo taifa linatarajia kufanya uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu 2024 na Uchaguzi Mkuu mwakani 2025.
Amebainisha kuwa kutokana na wananchi kupata uelewa kuhusu matumizi ya takwimu ikitokea kiongozi wa siasa anataka kusema vitu vyake visivyo na uhalisia, mtu wa kawaida atanyoosha mkono kumuumbua kufuatana na sensa.
"Kila mtu anafundishwa ili kila mmoja awe na uelewa kuhusiana na sensa, pia matokeo na takwimu zake," amesema.
Amebainisha kuwa NBS imeona umuhimuwa kuwapa mafunzo pia waandishi wa habari ili taaluma hiyo iwe ya kuaminika zaidi kwa takwimu.
"Waandishi wa habari mna nafasi kubwa katika suala hili na sisi tunawategemea. Tunategemea nchi yetu ifike mahali inazungumza habari za takwimu, sio tunazungumza maneno ya majungu majungu tu vitu vitu visivyoeleweka, hapana, tuzungumze maendeleo," amesema Makinda.
Amesema baada ya Rais kutangaza matokeo ya mwanzo mwaka 2022, kulitokewa mwongozo ambao lengo lake kuu ni kutumia matokeo ya sensa ya mwaka 2022 ili kuongeza uelewa, kufanya uwazi na kupanua wigo wa matumizi ya matokeo ya sensa kwa serikali zetu.
"Hili ni kwa wananchi pia na wadau wote ili waweze kupanga mipango yao jumuishi kwa maendeleo endelevu ya kiuchumi, kijamii na kimazingira," amesema Kamisaa huyo wa Sensa.
0 Maoni