Hot Posts

6/recent/ticker-posts

Mbowe kusuka au kunyoa kortini kesho

 Mwandishi Wetu,  daimatznews@gmail.com

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kesho Machi 13,2024 'atasuka au kunyoa'. Ndivyo unavyoweza kusema, wakati Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi itakapotoa uamuzi wa shauri alilofungua Mbowe kuwadai gharama waandishi wa habari 10, wanaomdai mtoto wake Dudley.

Leo waandishi wa habari 10 wanaomdai Dudley ambaye ni Mkurugenzi wa Tanzania Daima, Sh milioni 62.7 wameachia nyumba ya Freeman Mbowe waliyoikamata ili kuipiga mnada kufidia deni lao.

Hata hivyo, wamegoma kulipa gharama za kesi zilizoombwa na Mbowe wakieleza sababu hata wao wameingia gharama katika kudai haki yao.

Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi ilisikikiza shauli hilo mbele ya Naibu Msajili, Mary Mrio leo Machi 12,2024 ikieleza itatoa uamuzi kuhusu gharama kesho saa 8 mchana.

Mbowe kupitia Wakili wake John Mallya aliwasilisha maombi chini ya kiapo kilichoapwa na Freeman Mbowe Februari 26 mwaka huu, akitaka wajibu maombi kuondoa nyumba hiyo kwa sababu si mali ya Dudley na Mahakama iwaamuru wajibu maombi hao kumlipa gharama za kesi mteja wake.

Akizungumza kwa niaba ya wajibu maombi wenzake, Kulwa Mzee aliiambia mahakama kwamba walipitia nyaraka zote na viambatanisho husika, wamejiridhisha na kukubaliana kwa pamoja kwamba nyumba waliyoikamata ni ya familia, lakini inamilikiwa na Freeman Mbowe.

"...Tumepitia nyaraka pamoja na viambatanisho ikiwemo hati ya nyumba. Tumejiridhisha kwamba mkurugenzi tunayemdai, Dudley Mbowe si mmiliki. Hivyo, tunaiomba Mahakama tuiondoe nyumba hiyo kwenye maombi yetu," alisema Kulwa na kuongeza:

"Mheshimiwa, kuhusu gharama, kwa uelewa wetu, katika mashauri ya migogoro ya kikazi, hakuna gharama. Hiyo inatokana na uwezo na kipato kidogo cha wafanyakazi;

"Wakati sisi tunafanya jambo hili, tulikuwa tukiamini kabisa kuwa ni nyumba ya mkurugenzi wetu kwa sababu katika hatua ya makubaliano, alikuwa anatuambia kuwa tutafanya vikao nyumbani kwake na tumefanya hapo vikao  kwenye hiyo nyumba," amesema Kulwa.

Ameongeza: "Mheshimiwa katika hatua za mwisho, baba yake ambaye ndiye mwombaji katika shauri hili alitualika tukutane hapo hapo tulipokuwa tukikutana. Tulikutana hapo, akakubali kubeba dhamana ya mtoto wake akakubali kutulipa mwezi Desemba."

Kulwa alidai kutokana na mazingira hayo waliamini kuwa hapo ndipo nyumbani kwake mkurugenzi na baada ya kushindwa kuwalipa katika kutekeleza namna ya kupata haki yao ndio maana waliamua kukamata hiyo nyumba.

"...Mheshimiwa tunaomba tusilipe gharama, kwanza huyu mwombaji hakuingia gharama kwani katika  hatua zote za majadiliano tulikuwa tunakwenda kwake kwa gharama zetu wenyewe na ahadi zake za kutulipa Desemba 2023 ambazo alishindwa kutekeleza hilo lilituathiri, maana tulikuwa katika maandalizi ya siku kuu na  ada za watoto shuleni,"amedai Kulwa.

Aliomba Mahakama katika uamuzi kuhusu gharama ikiwezekana kila upande ubebe gharama zake.

Kwa upande wake, dalali wa Mahakama Jesca Massawe ambaye ni mjibu maombi wa 11, alidai alipokea amri ya Mahakama kwa ajili ya kukamata hiyo nyumba.

"Sisi madalali wa Mahakama katika kutekeleza majukumu yetu, tulikaa na Mahakama hii chini ya Jaji Mfawidhi  akatuelekeza kuwa katika mashauri haya ya kukamata mali tusijihusishe na utambuzi wa mali bali tukamate na kama kuna changamoto basi italetwa mahakamani, " amesema.

Ameongeza kwamba alitekeleza amri ya Mahakama kama ilivyoelekezwa.

Wakili Mallya alijibu hoja hiyo akieleza kwamba anakubaliana na mjibu maombi Kulwa kwa aliyoyasema ya kuachia nyumba hiyo.

Hata hivyo akasema: "Kuhusu suala la gharama, mteja mwombaji anastahili kulipwa gharama na mambo mengine aliyoyasema mjibu maombi alipaswa kuyaleta kwa njia ya kiapo."

Amedai kuhusu hoja za mjibu maombi wa 11 ambaye ni dalali, kweli ni afisa wa Mahakama lakini maelezo yake hayakuja kwenye kiapo. 

"Kwa kuwa anamtaja na Jaji Mfawidhi, haya yalipaswa kuja kwa njia ya kiapo na si maneno matupu mahakamani. Kwa hiyo naiomba Mahakama yako isiyazingatie  na tunaomba mahakama izingatie suala la gharama,"alidai Mallya.

Naibu Msajili Mrio baada ya kusikiliza hoja za pande zote aliahirisha shauri hadi leo saa nane mchana kwa ajili ya uamuzi.

Katika shauri la msingi,  mjibu maombi mwingine Maregesi Paul, aliomba kuyaondoa maombi ya kukamata nyumba hiyo na kuieleza Mahakama kwamba wanatarajia kuwasilisha maombi mengine upya ya kumkamata Dudley.

"Maombi haya yameondolewa kwa kibali cha kuyaleta tena, "alisema Msajili.

Mbowe kafungua shauri dhidi ya Maregesi Paul, Fidelis Felix, Christina Mwakangale, Janeth Josiah, Exuperius Kachenje, Hellen Sisya, Kulwa Mzee, Nora Damian, Makuburi Ally, Mkurugenzi wa Gazeti la Tanzania na Kampuni ya Udalali ya JJ Auctioneers& Debt Collectors.

Februari 13 mwaka huu, Mahakama ilikubali maombi ya wadai na kumteua dalali wa Mahakama kukamata nyumba kwa ajili ya kuipiga mnada.

Februari 28 mwaka huu, dalali wa Mahakama, Jesca Massawe alifanikiwa kubandika matangazo ya kukamata nyumba ya Mkurugenzi tayari kupigwa mnada kufidia deni la malimbikizo ya mishahara wafanyakazi.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Mary Mrio alitoa amri hiyo baada ya kupitia hoja za washinda tuzo katika Tume ya Usuluhishi na Uamuzi(CMA) Julai 2023.

Shauri hilo namba 28461 la mwaka 2023, wadai Maregesi Paul na wenzake tisa dhidi ya Mkurugenzi wa Gazeti la Tanzania Daima, Dudley Mbowe.

Baada ya mdaiwa kukaidi kulipa, wadai  walikubaliana njia sahihi kukamata nyumba yake namba 9 iliyopo Mtaa wa Feza , Mikocheni B barabara ya Chipaka na Mahakama ilikubali.

Walalamikaji hao walipata tuzo Julai 17 mwaka 2023 mbele ya Msuluhidhi wa CMA Ilala,  Bonasia Mollel.

Madai ya awali yalikuwa jumla ya Sh milioni 114 baada ya kukaa mezani kwenye majadiliano kwa pamoja kiwango hicho cha fedha kilishuka na kufikia Sh milioni 62.7.

Dudley alikubali kulipa fedha hizo kwa awamu tatu, Oktoba 30, Desemba 30 mwaka 2023 na awamu ya mwisho ilikuwa mwishoni Februari mwaka huu lakini hakulipa.

Chapisha Maoni

0 Maoni