-Aelimishwa kuhusu ulinzi wa kazi zake
Mwandishi Wetu, daimanewstz@gmail.com
Mwanamuziki wa kizazi kipya, Naseeb Abdul maarufu Diamond Platnumz ametembelea Ofisi za BRELA jijini Dar es Salaam Machi 7, 2024, ambapo amekutana na kuzungumza na Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), Godfrey Nyaisa ambapo alipata elimu kuhusu ulinzi wa kazi na chapa zake .
Akizunguza baada ya mkutano wake na Nyaisa, Diamond amesema mbali na kuwa mwanamuziki yeye ni mfanyabiashara na mwekezaji ambaye hutengeneza na kuanzisha chapa na kuwainua vijana ili kujipatia kipato hivyo BRELA hawezi kupakwepa kwa kuwa yeye ni mfanyabiashara.
“Nilipokutana na Nyaisa naye kujitambulisha kwangu alinieleza kwamba BRELA panafaa kuwa nyumbani kwangu kwa sababu nina chapa tofauti, hivyo patanisaidia katika kusajili kazi zangu ili nisipoteze haki,"amesema Diamond na kufafanua:
"Maneno hayo yalikuwa na maana kubwa katika maisha yangu na hapo ndipo nilipobadilisha mtazamo na kugundua vijana wengi wanapoteza haki zao.”
Diamond ameonya kuwa wasanii, wanamichezo, vijana na yeyote mwenye lengo la kufika mbali kimaendeleo, hawezi kufanikiwa iwapo hajarasimisha biashara yake BRELA na ili kuwa rasmi unahitaji kusajili jina la biashara, kusajili kampuni na kufuata taratibu mbalimbali zilizowekwa na serikali kama njia nzuri zitakazolinda na kuwezesha vijana kufika mbali.
Amesisitiza kuwa ni vyema kwa wasanii na vijana kujitahidi kurasimisha na kulinda alama za biashara,huduma na vumbuzi zao BRELA ili kulinda ndoto zao kwa sababu mtu akianzisha jambo na likawa kubwa, ukigundua kuna mtu mwingine anatumia alama hiyo, kama yeye amewahi kuisajili kisheria, anaweza kukupeleka katika vyombo vya sheria.
“Kwa watu wanaotumia brand zetu pasipokuwa na haki halali, naelewa kibinadamu atakuwa anatafuta riziki, lakini nawashauri waache ili baadae wasinilaumu kwa sababu sheria itafuata mkondo wake. Lakini kwa kipindi hiki tumeamua kuwa makini zaidi katika biashara," amesisitiza Diamond.
Amehitimisha kwa kusema kuwa sasa amegundua umuhimu wa sajili na amefanikiwa kuchukua hatua ya kulinda haki zake BRELA, baada ya kufahamu kwa kina faida zake hivyo kuepuka hasara kubwa ambayo angeipata na kupelekea kupoteza Pato la Taifa.
0 Maoni