Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
Uongozi wa Taasisi ya Uhasibu Arusha (IAA), umekutana na Mkurugenzi Mkuu Msaidizi wa UNESCO anayeshughulikia Elimu, Profesa Qun Chen, jijini Paris Ufaransa, ambapo wamejadiliana kuhusu kuanzisha ushirikiano wa kimkakati baina ya taasisi hizo.
Katika mkutano huo, IAA iliongozwa na Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini, Dk. Mwamini Tulli, na Mkuu wa Chuo, Profesa Eliamani Sedoyeka, ambaye amemweleza Prof Qun Chen nafasi ya IAA katika kuandaa wataalamu wa uhasibu, fedha, biashara na TEHAMA.Prof Sedoyeka pia alielezea dhamira ya chuo hicho kupanua ushirikiano wa kimataifa katika mafunzo na utafiti.
Kwa upande wake, Prof. Chen ameonesha utayari wa UNESCO kushirikiana na IAA katika kuwaendeleza walimu, utafiti pamoja na kuanzisha UNESCO Chairs kama kiungo cha ushirikiano wa kitaaluma na taasisi za nchi nyingine.
Katika mkutano huo Prof. Chen aliambatana na Carlos Vargas-Tamez, Mkuu wa Sehemu ya Maendeleo ya Walimu wa UNESCO, na Maya Prince, Meneja wa Programu ya UNITWIN/UNESCO Chairs.Ziara na mazungumzo hayo vimeratibiwa na Ubalozi wa Tanzania nchini Ufaransa, kwa ushiriki wa Balozi Mhe. Saidi Yakubu.




Chapisha Maoni