Habemus Papam; Moshi mweupe watokea Vatican tumepata Papa
-Ni Kardinali Robert Prevost wa Chicago Marekani
-Sasa ni Papa Leo wa XIV
Mwandishi Wetu,daimatznews@gmail.com
Habemus Papam;Ndiyo maneno yanayotamkwa kwa kilatini, kutangazia ulimwengu kwamba Papa amepatikana.
![]() |
Papa Leo wa XIV, akisalimia umati wa waamini waliofirika viwanja vya St.Peters Vatican, mara baada ya kutangazwa kuwa kiongozi mpya wa Kanisa Katoliki duniani. |
Ndivyo ilivyotokea leo, historia mpya imeandikwa kwa Kanisa Katoliki,ambapo kwa mara ya kwanza Mmarekani amechaguliwa kuwa Papa.
Leo Alhamisi Mei 08, Baraza la Makardinali lililokuwa likikutana ndani ya Kanisa la Sistine kwa katika mkutano wa siri wa uchaguzi wa Papa limemchagua Kardinali Robert Prevost, mzaliwa wa Chicago, kuliongoza Kanisa Katoliki.duniani.
Kardinali Robert Prevost amekubali wadhifa wake mpya kuwa Askofu wa Roma na kiongozi wa kiroho wa Wakatoliki zaidi ya bilioni 1.4 duniani, huku akichagua jina la Papa Leo wa XIV.
Kwa siku ya pili leo kuanzia jana Mei 7,2025, makardinali 133 wa Kanisa Katoliki duniani walikuwa kwenye mchakato wa kupiga kura kumtafuta Papa mpya kupitia mkutano wao maalum unaojulikana kama Conclave.
Papa Leo wa XIV sasa ndiye mrithi wa nafasi hiyo ya kuliongoza Kanisa Katoliki, baada ya kifo cha mtangulizi wake, Papa Francis kilichotokea mjini Vatican Aprili 21,2025.
Uchaguzi huo ni hatua muhimu kwa Kanisa Katoliki,lakini pia kwa Marekani, taifa ambalo ushawishi wake wa kimataifa mara nyingi umeibua maswali kuhusu uwezekano wa kutoa kiongozi wa Kanisa Katolikiduniani.
Kati ya mapapa 266 waliotangulia katika historia, hakuna hata mmoja aliyechaguliwa kutoka Marekani, huku pia chini ya ishirini pekee wamewahi kushika wadhifa huo tangu Marekani ilipotangaza uhuru mwaka 1776.
Usiku wa mkesha wa mkutano huo, Askofu Robert Barron kutoka Minnesota alitafakari juu ya ukosefu huu wa kihistoria, akimnukuu marehemu mlezi wake, Kardinali Francis George, aliyekuwa na maoni kwamba Papa kutoka Marekani hangetokea hadi pale ushawishi wa kimataifa wa taifa hilo utakapopungua.
![]() |
Moshi mweupe ukitoka katika dohani ya Kanisa la Sistine, kuashiria kupatikana kwa Papa mpya. |
“Kama Marekani inaongoza dunia kisiasa, kiutamaduni na kiuchumi, hawataki Marekani pia iiongoze dunia kidini,” Barron alieleza.
Askofu Barron, ambaye hivi karibuni aliteuliwa na Rais Trump kuwa mwanachama wa Tume ya Ikulu kuhusu Uhuru wa Kidini, alikuwa miongoni mwa viongozi wengi wa Kanisa waliokuwepo Roma wiki hii.
Ingawa hakuwa miongoni mwa makardinali wapiga kura, Barron alitumia muda mwingi kujadiliana nao walipokuwa wakitafakari ni nani anayefaa zaidi kuiongoza Kanisa katika hatua yake ijayo.
Kwa uchaguzi wa Papa Leo wa XIV, enzi mpya inaanza, enzi inayovunja karne nyingi za jadi na kumweka Mmarekani katika kiini cha Ukatoliki duniani.
Maoni
Chapisha Maoni