Hussein Ndubikile, daimatznews@gmail.com
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam wakati akitoa mwelekeo wa mvua hizo, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, (Pichani juu), Dk. Ladislaus Chang’a, amesema mvua hizo zinatarajiwa kuanza katika wiki ya kwanza na ya pili ya Oktoba katika baadhi ya maeneo.
Amebainisha kuwa mikoa ya Arusha na Manyara, mvua zinatarajiwa kuwa za wastani hadi juu ya wastani, huku hali kama hiyo ikitarajiwa pia katika ukanda wa Kaskazini unaojumuisha Tanga, Dar es Salaam, kaskazini mwa Morogoro pamoja na visiwa vya Mafia na Pemba.
TMA imesema uwepo wa El Niño unaweza kuchangia kuongezeka kwa vipindi vya mvua kubwa, hali ambayo inaweza kusababisha mafuriko na athari katika miundombinu, kilimo, usafiri na shughuli nyingine za kijamii na kiuchumi.
El Niño ni hali ya mabadiliko ya mfumo wa joto la bahari katika eneo la Pasifiki ya ikweta, ambayo huathiri mifumo ya hewa duniani na inaweza kusababisha mabadiliko ya mvua na joto katika maeneo mbalimbali. Kwa Tanzania, hali hiyo inaweza kuhusishwa na ongezeko la mvua katika baadhi ya maeneo, ingawa athari zake hutofautiana kulingana na eneo na kipindi.
Kutokana na hali hiyo, TMA imewataka wananchi kufuatilia taarifa rasmi za hali ya hewa na kuchukua tahadhari mapema, hasa katika maeneo yanayoweza kukumbwa na mvua kubwa na mafuriko.
TMA pia imesema hali hiyo inaweza kuchangia kuanza mapema kwa mvua za msimu wa Novemba hadi Aprili katika baadhi ya maeneo yanayopata msimu huo.
Katika sekta ya kilimo, TMA imesema kuongezeka kwa unyevunyevu wa udongo na uwezekano wa mafuriko kunaweza kuathiri ukuaji wa mazao na shughuli za kilimo, huku mazingira yenye unyevunyevu yakitarajiwa pia kuchochea kuibuka kwa baadhi ya magonjwa ya mimea.
Wakulima wametakiwa kuandaa mashamba, kupanda na kupalilia kwa wakati, kutumia pembejeo zinazofaa na kuzingatia ushauri wa wataalamu.
Kwa wafugaji, TMA imeshauri kuandaa malisho na kuhifadhi maji ya kutosha kwa matumizi ya mifugo, huku wakitakiwa kufuatilia taarifa za hali ya hewa na kupata ushauri kutoka kwa maafisa mifugo.
Wavuvi na wakulima wa mwani nao wametakiwa kufuatilia taarifa za hali ya hewa na hali ya bahari kabla ya kufanya shughuli zao.
TMA imeonya kuwa mvua kubwa zinazoweza kuambatana na vipindi vya El Niño zinaweza pia kuathiri barabara, madaraja na miundombinu mingine ya usafiri kutokana na mafuriko na mmomonyoko wa udongo.
Mamlaka za serikali za mitaa zimetakiwa kujiandaa kwa kuboresha mifumo ya mifereji ya maji, kuondoa vizuizi kwenye njia za maji na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu tahadhari za kuchukua wakati wa mvua kubwa.
Katika sekta ya afya, TMA imeonya kuhusu uwezekano wa kuongezeka kwa magonjwa kutokana na maji kutuama, kuathirika kwa mifumo ya maji taka na changamoto katika usafi wa mazingira.
Aidha, TMA imevitaka vyombo vya habari kuendelea kutumia taarifa rasmi za hali ya hewa katika kuhabarisha na kuelimisha jamii kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa na tahadhari zinazopaswa kuchukuliwa.
Mamlaka hiyo imesema imeendelea kujenga uwezo wa kutoa utabiri wa hali ya hewa hadi ngazi ya wilaya, hatua inayolenga kuwawezesha wananchi, wakulima, wafugaji, wafanyabiashara na serikali za mitaa kupanga shughuli zao kwa kuzingatia taarifa za hali ya hewa.
TMA imewataka wananchi kuendelea kufuatilia taarifa za kila siku, angalizo na tahadhari zitakazotolewa, ikisisitiza kuwa kuchukua hatua mapema ni muhimu katika kupunguza madhara yanayoweza kusababishwa na mvua kubwa.
MAFURIKO NA KILIMO
TMA imeonya kuwa mvua nyingi zinaweza kuongeza unyevunyevu wa udongo na kusababisha mafuriko, hali inayoweza kuathiri shughuli za kilimo na uzalishaji wa chakula.
Pamoja na changamoto hizo, mvua zinaweza kuongeza uzalishaji katika maeneo yatakayotumia vizuri fursa hiyo. Wakulima wametakiwa kuandaa mashamba, kupanda kwa wakati, kutumia pembejeo sahihi na kuboresha usimamizi wa maji.
“Wakulima wanashauriwa kutumia mbinu bora za kilimo, kuvuna maji ya mvua na kuchukua hatua za kudhibiti visumbufu vya mimea ili kupunguza athari na kuongeza uzalishaji,” imesema TMA.
BARABARA, MADARAJA NA USAFIRI
Mamlaka hiyo imeonya kuwa mvua kubwa zinaweza kusababisha mafuriko, mmomonyoko wa udongo, kuharibika kwa barabara na madaraja, hali inayoweza kuvuruga usafiri na kuongeza hatari ya ajali.
Bandari nazo zinaweza kukumbwa na mawimbi makubwa na hali mbaya ya bahari, huku usafiri wa anga ukiathiriwa na mwonekano hafifu na kuchelewa kwa safari.
TMA imewataka wadau wa usafiri kukagua miundombinu mara kwa mara na kufuatilia taarifa za hali ya hewa ili kuchukua hatua kwa wakati.
AFYA NA MAZINGIRA
TMA pia imeonya kuhusu uwezekano wa kuongezeka kwa magonjwa kutokana na maji kutuama, kuathirika kwa mifumo ya maji taka na uchafuzi wa vyanzo vya maji.
Mamlaka za afya zimetakiwa kujiandaa kwa changamoto hizo, huku wananchi wakihimizwa kuchukua hatua za usafi na kuzuia maji kutuama katika maeneo ya makazi.
WAFUGAJI NA WAVUVI
Wafugaji wametakiwa kupanga matumizi ya maji na malisho pamoja na kufuatilia ushauri wa wataalamu wa mifugo.
Wavuvi na wakulima wa mwani nao wametakiwa kufuatilia taarifa za hali ya hewa na bahari kabla ya kuanza shughuli zao ili kupunguza hatari zinazoweza kujitokeza.
SERIKALI ZA MITAA ZATAKIWA KUJIANDAA
TMA imezitaka serikali za mitaa kuimarisha mifumo ya mifereji, kuondoa vizuizi kwenye njia za maji na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kujikinga na mafuriko.
“Maandalizi ya mapema ni muhimu katika kupunguza madhara ya matukio ya hali mbaya ya hewa,” TMA imesisitiza.
TMA imesema pia imeendelea kuboresha utabiri wa hali ya hewa hadi ngazi ya wilaya, hatua inayolenga kuwasaidia wananchi, wakulima, wafugaji, wafanyabiashara na serikali kupanga shughuli zao kwa kuzingatia mwenendo wa hali ya hewa.
Mamlaka hiyo imewataka wananchi kuendelea kufuatilia taarifa za kila siku, angalizo na tahadhari rasmi zitakazotolewa kadiri hali ya hewa itakavyobadilika.
“Taarifa rasmi za hali ya hewa zinapaswa kuwa chanzo cha msingi katika kuhabarisha na kuelimisha jamii kuhusu matukio yanayoweza kujitokeza,” TMA imesema.



Chapisha Maoni