Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, amesema Tanzania imejipanga kuwa kitovu cha soko la kaboni barani Afrika na kwamba Serikali inaimarisha mifumo ya usimamizi, uwazi na uwekezaji ili kuhakikisha biashara hiyo inachangia kuboresha maisha ya wananchi na ukuaji uchumi wa taifa. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Yussuf Masauni, akifungua Jukwaa la Soko la Kaboni na Uwekezaji Tanzania 2026, jijini Dar es Salaam Oktoba 22, 2026.
Masauni amesema hayo, Oktoba 22, 2026, alipokuwa akifungua Jukwaa la Soko la Kaboni na Uwekezaji Tanzania 2026, Jijini Dar es Salaam, lililobebwa na kaulimbiu isemayo; “Siku Moja. Soko Moja. Maono ya Pamoja.”
"Serikali inalenga kuhakikisha biashara ya kaboni inakuwa nyenzo muhimu ya maendeleo ya Taifa kwa kuzalisha ajira, kuongeza mapato ya jamii, kuvutia uwekezaji, kuhifadhi misitu na kuendeleza matumizi ya nishati safi, pamoja na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050,"amesema Masauni na kuongeza;
“Tanzania imeamua kuwa kitovu cha soko la kaboni lenye uadilifu barani Afrika, ambapo kila tani ya kaboni inayothibitishwa, inatafsirika kuwa ajira kwa vijana wetu, mapato kwa vijiji vyetu, misitu iliyohifadhiwa, nishati safi majumbani mwetu na mtaji wa kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.”
Ameeleza kwamba Tanzania chini ya uongozi wa Rais,Dk. Samia Suluhu Hassan, ajenda ya nishati safi ya kupikia ni moja ya maeneo yenye fursa kubwa ya biashara ya kaboni, kutokana na uwezo wake wa kufikia mamilioni ya kaya na kuchangia kupunguza gesijoto.
Awali, Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais Dk. Richard Muyungi alisema kwamba jamii zinazohusika na usimamizi wa misitu, ardhioevu, mikoko na maeneo mengine yenye uwezo mkubwa wa kuhifadhi kaboni zinapaswa kushirikishwa kikamilifu katika kubuni na kutekeleza miradi pamoja na kupanga namna ya kugawana manufaa.
Amesema wanawake, vijana, wajasiriamali wa ndani na waendelezaji wa miradi midogo ya kaboni wanapaswa kupata nafasi katika uchumi unaochochewa na soko la bidhaa hiyo.Katika hafla hiyo, Mtendaji Mkuu wa Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC), Kathryn Kigaraba amesema kuwa kituo hicho kina jukumu muhimu la kusaidia maendeleo ya soko la kaboni nchini kwa kuzingatia utaalamu wa kisayansi, mbinu sahihi za kitaalamu, uwazi wa taarifa na mifumo ya ufuatiliaji na uthibitishaji.
"Lengo ni kujenga soko ambalo miradi yake inatambuliwa na kuendelezwa kwa utaratibu unaofaa, inafanyika kwa uwazi na manufaa yanayopatikana yanachangia maendeleo endelevu ya Tanzania," amesema.
Amebainisha kwamba utekelezaji wa azma hiyo unahitaji ushirikiano wa karibu kati ya taasisi za Serikali, wawekezaji, taasisi za fedha, waendelezaji wa miradi ya kaboni,jamii za wenyeji, washirika wa maendeleo na taasisi za utafiti.
Kigaraba amesema kwamba mifumo ya kitaasisi inayohusu tathmini ya miradi, usajili wa miradi, ubadilishanaji wa taarifa na ulinzi wa haki na maslahi ya wadau ni muhimu katika kujenga imani ya soko.



Chapisha Maoni