-Yaadhimisha Siku ya Wanyamapori Duniani
-Yaita wananchi kujionea vivutio vya mjini
Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
Mamlaka ya Uhifadhi Wanyamapori nchini (TAWA), Kanda Maalum ya Dar es Salaam, leo Machi 3, 2026, imeungana na wadau wengine wa sekta hiyo katika kuadhimisha Siku ya Wanyamapori Duniani, inayoadhimishwa Machi 3 kila mwaka, ikihimiza jamii kushiriki katika kulinda wanyama walio katika hatari ya kutoweka kwa faida ya taifa leo na vizazi vijavyo.
![]() |
| Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Sylvester Mushy |
Kamanda wa Uhifadhi Kanda Maalum ya Dar es Salaam,
Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Sylvester Mushy ametoa wito huo ofisini kwake
jijini Dar es Salaam leo Machi 3, 2026 alipokuwa akizungumzia maadhimisho hayo
yaliyobeba Kauli mbiu isemayo; ‘Mimea dawa, manukato, uhifadhi urithi na
kuboresha maisha.’
Amesema kauli mbiu hiyo inahamasisha wananchi kutunza
hifadhi wanyama pori na mimea, lakini pia TAWA imetumia siku hiyo kuwapa elimu na kuwahamasisha
wananchi kujifunza kudhibiti wnyama wakali waharibifu wa mimea kama tembo kwa
kutumia mimea ambayo huwafukuza badala ya kuwaua.
“Leo ni Siku Kuu, Dunia inapokumbuka umuhimu wa uhifadhi wanyamapori. Kwa mwaka huu kitaifa siku hii inaadhimishwa mkoani Arusha. Wananchi wanapaswa kupata uelewa wa manufaa ya wanyamapori na mimea na kushiriki kuifadhi,” amesema Mushy na kuongeza:
“Mfano katika kudhibiti Wanyama wakali waharibifu, TAWA
inafundisha wananchi kutumia pilipili kichaa, kwa kupanda kando ya mashamba yao
au kuzisaga na kumwaga maeneo hayo ili kuwafukuza tembo wasiharibu mazao.”
Kamishna Msaidizi Mwandamizi, Mushy amesema wananchi hasa
vijana wana fursa kutembelea maeneo mbalimbali ya vivutio na hifadhi yaliyo
chini ya mamlaka hiyo, ikiwamo hifadhi za mjini kama Msitu wa Pande Dar es
Salaam wenye wanyama mbalimbali ikiwamo simba na duma.
Ametaja vivutio vingine ndani ya kanda hiyo maalum kuwa
ni Magofu ya Kunduchi yaliyobeba historia ya waswahili na Hifadhi ya Wami Mbiki
iliyopo Morogoro nili kujifunza, kuburudika na kujionea shughuli za uhifadhi
wanyamapori na mimea zinavyofanyika.
Akizungumzia zaidi maadhimisho ya Siku ya Wanyamapori
Duniani, Kamanda huyo wa Uhifadhi Kanda Maaluma ya Dar es Salaam amesema chimbuko
lake ni Kikao cha 68 cha Baraza Umoja wa Mataifa wa mwaka 2013, ambapo Tanzania
imesaini mkataba huo unaozuia uwindaji na usafirishaji wa Wanyama na mimea
iliyo katika hatari ya kutoweka.
Naye Ofisa Mhifadhi Mwandamizi anayeshughulikia pia Ujirani Mwema TAWA Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Sanjo Mafuru (pichani chini), ametaja baadhi ya wnyama walio katika hatari ya kutoweka kuwa ni Pamoja na Mbwa mwitu, tembo, faru weusi na sokwe.
Amesisitiza kwamba wananchi wanapaswa kupata uelewa wa
manufaa ya wanyamapori na mimea lakini pia kushiriki katika kuwalinda wanyama hao.
“TAWA inawakumbusha vijana, wanawake na wazee kwamba ni
muhimu kufuatilia elimu ya uhifadhi na kushiriki kweny uhifadhi kwa kuwa
uhifadhi wa Wanyama na mimea una faida kiuchumi, kiutamaduni, kimazingira. Bila
wanyamapori hakuna utalii, tukumbuke asilimia 17 ya Uchumi unachangiwa na utalii,”
amesema Sanjo na kuongeza;
“Tushikamane katika kuhifadhi misitu na wanyamapori, kuna
faida katika kuhifadhi wanyamapori na misitu kwani pia katika mzunguko wa
maisha, binadamu, mime ana Wanyama tunategemeana.”



Chapisha Maoni