NHC YAPANUA FURSA UMILIKI WA NYUMBA KUPITIA MIKOPO NA TEKNOLOJIA

-Wiki ya Huduma kwa Wateja ilivyokutanisha wadau wa nyumba

-Kutoka Dar Kawe 711, hadi mikoani NHC yachochea mageuzi ya nyumba na biashara

Na Exuperius Kachenje,daimatznews@gmail.com

Kuanzia huduma kwa wateja hadi ujenzi wa makazi ya kisasa, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), linazidi kuimarisha mkakati wake wa kupanua fursa za Watanzania kumiliki nyumba bora za kisasa, huku likitumia mikopo ya benki, ubia na teknolojia  kuboresha huduma na kuendeleza miji.

Mkakati huo umewekwa wazi katika kilele cha Wiki ya Huduma kwa Wateja, kilichofanyika Oktoba 16, 2026, eneo la Mradi wa Kawe 711, Dar es Salaam, ambapo NHC imewakutanisha wadau wa nyumba zikiwamo taasisi za kifedha, zilizoeleza namna ushirikiano huo unavyoweza kurahisisha ununuzi wa nyumba kwa malipo ya awamu, hivyo kuwapa unafuu wananchi.

Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah, aliyezungumza katika hafla hiyo, amesema juhudi hizo zinaunga mkono azma ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kuwawezesha Watanzania wengi zaidi kumiliki nyumba bora.

“Tunataka kutimiza ndoto ya Mheshimiwa Rais ya kuwawezesha Watanzania wengi zaidi kumiliki nyumba bora. Hili linawezekana kupitia ushirikiano imara kati ya NHC na benki zinazotoa mikopo ya nyumba kwa Watanzania waliopo nchini na wanaoishi nje ya nchi,” amesema.

Kawe 711 yaonesha sura ya makazi ya kisasa

Mradi wa Kawe 711, uliopewa jina hilo kutokana na namba ya kiwanja ulipo, ni miongoni mwa miradi ambayo NHC inaitumia kuonesha mwelekeo wake wa kujenga makazi yenye huduma za kisasa. Mradi huo una nyumba 422 na upo karibu na Bahari ya Hindi umbaki wa mita 50.

Kwa mujibu wa Hamad, mradi huo una bwawa la kuogelea, viwanja vya michezo vilivyopo ghorofani, mifumo ya kuhifadhi maji, jenereta za umeme wa dharura na vifaa vya tahadhari ya moto.

Amesema huduma hizo zinalenga kuboresha usalama na mazingira ya makazi, huku eneo la mradi likiongeza mvuto kwa wanunuzi. Hamad amewahimiza wananchi kuchangamkia fursa za kununua nyumba Kawe 711 na katika miradi mingine ya shirika.

Awali, Meneja wa Mauzo na Masoko wa NHC, Deogratius Batakanwa aliwaambia wananchi waliohuduria hafla hiyo akieleza kwamba;

 “NHC inaongeza thamani ya mradi huo  kwa kuboresha hatua zake za kukamilika hali inayoufanya kuwa bora zaidi na kwamba ifikapo Desemba 2026 nyumba hizo zitakabidhiwa kwa wateja,”

Kwa Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa NHC anabainisha kwamba shirika hilo pia lina miradi wa Ras Kilomoni, karibu na Mbweni, huku Golden Premier Residence (GPR) ikiwa miongoni mwa miradi mipya inayopanua chaguo kwa wanaotafuta nyumba za kisasa.

Mikopo ya muda mrefu kupanua umiliki

Wakati awali gharama za ununuzi wa nyumba za NHC zilionekana kama kikwazo kwa baadhi ya wananchi wasioweza kulipia nyumba kwa fedha taslimu, sasa Shirika linasema ushirikiano wake na benki takribani 20, unalenga kupunguza changamoto hiyo na kuwawezesha wanunuzi kupata mikopo kulingana na vigezo vya taasisi husika.

Kupitia baadhi ya benki washirika, muda wa marejesho umeboreshwa na sasa unaweza kufikia miaka 25, ikilinganishwa na miaka mitatu hadi mitano katika baadhi ya taasisi za fedha na benki, awali.

Fursa hizo za sasa pia zinawalenga Watanzania wanaoishi nje ya nchi (Diaspora), wanaotaka kununua nyumba nchini. Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa NHC, utaratibu wa kutumia nyumba inayokusudiwa kununuliwa kama dhamana, unaweza kuwasaidia wateja wasiokuwa na mali nyingine ya kuweka dhamana, kadri ya masharti ya benki.

Katika Wiki ya Huduma kwa Wateja, taasisi za kifedha zilipata nafasi ya kueleza huduma zao kwa wanunuzi watarajiwa wa nyumba za NHC, huku ushindani wa benki hizo ukiwapa wateja fursa ya kulinganisha viwango vya riba, kiasi cha mkopo, muda wa marejesho na gharama nyingine kabla ya kufanya uamuzi.

Benki zilizoshiriki hitimisho la Wiki ya Huduma kwa Mteja iliyoandaliwa na NHC ni pamoja na  Bank of Africa, Azania Bank, NBC, NMB, CRDB, Fast Housing Bank, ABSA, Equity Bank na TCB Bank, ambapo takriban kila moja ilipata nafasi kueleza kwa kifupi nafasi yake katika kuwawezesha Watanzania kumiliki nyumba za NHC kwa njia ya mikopo na muda wa marejesho.

Maelezo ya wawakilishi wa benki hizo, yameacha wananchi na hamasa iliyozungukwa na fursa za kuchagua kwa kukopa na muda wa marejesho, NHC ikitia nguvu mpango huo kwa kuruhusu nyumba inayonunuliwa kuwa dhamana ya mkopo katika benki hizo.

Sauti za Wananchi/wateja

Akizungumzia NHC na Mradi wa Kawe 711, Mamruk Ambali aliyezungumza kwa niaba ya wananchi amesema tukio hilo ni sehemu ya wananchi kujifunza na kutiana moyo na kufanya uamuzi.

“Tumekuja  kuona na kufanya uamuzi. Tunaishukuru NHC, hapa nawtia moyo Watanzania wote tuchangamkie fursa hii. Mimi nimefanya uamuzi, nimenunua nyumba, unaweza kuishi au kupangisha ukapata chanzo cha uhakika cha fedha,” amesema Ambali.

Mwananchi mwingine, Theresia Lutufyo amewashauri wananwake kutoogopa bali waende NHC, watumia fursa ya mikopo benki wamiliki nyumba zinazoweza pia kutumika kama kitegauchumi. “Wanawake tusiogope, njooni NHC kununua nyumba kupitia benki na kulipa kwa miaka mingi,” amesema.

Kariakoo kubadilika kupitia ubia

Mbali na makazi, NHC inaendeleza mageuzi ya majengo ya biashara kupitia ubia kati ya sekta ya umma na binafsi.

Mkurugenzi wa NHC, Hamad Abdallah anasema shirika lina miradi takribani 22 ya ubia Kariakoo, Dar es Salaam, inayolenga kubadilisha majengo ya zamani na kujenga majengo ya kisasa.

Ameeleza kuwa ndani ya miaka mitatu ijayo, shirika linatarajia kuondoa majengo yake yote ya zamani eneo hilo na kuwa na majengo mengi mapya ya kisasa, huku matatu tayari yakiwa yamekamilika na wapangaji kuanza kuyatumia.

Majengo hayo mapya yanatarajiwa kuwa na angalau ghorofa 10, hatua inayolenga kuongeza matumizi bora ya ardhi, kuongeza idadi ya wafanyabiashara, kuboresha mazingira ya biashara na kuongeza thamani ya mali. Mpango huo pia unaonesha namna ubia unavyoweza kusaidia kutekeleza miradi mikubwa ya majengo.

Miradi ya mikoani yaongeza fursa

Mkakati wa NHC unaenea nje ya Dar es Salaam, ambako shirika linaunganisha makazi na maeneo ya biashara katika miji mbalimbali.

Kwa.mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa NHC,Hamad Abdallah Mkoani Ruvuma, NHC ina Songea Plaza,jengo la ghorofa sita katikati ya Songea, lenye maeneo ya biashara na makazi. Iringa kuna Iringa Commercial Complex nayo inaunganisha matumizi hayo, huku Uluguru Plaza mkoani Morogoro ikiwa na maeneo ya biashara na nyumba za makazi katika ghorofa za juu.

Hamad anaeleza kuwa nyumba zote za Uluguru Plaza zimeuzwa wakati ujenzi ukiendelea, jambo linaloonesha kuwa baadhi ya wateja wako tayari kununua nyumba kabla ya mradi kukamilika, hali inayoonyesha NHC kuaminika zadi na wateja.

Mkurugenzi huyo anasema katika Mkoa wa Tanga, NHC imejenga Mkwakwani Plaza, karibu na Uwanja wa Mkwakwani, ambao pia umeshapata wapangaji katika maeneo yake ya biashara na makazi. “Kutokana na mahitaji, NHC imeanzisha awamu ya pili ya ujenzi katika eneo jirani na Mkwawani Plaza II.

Kwa mujibu wa Hamad, sambamba na miradi mipya, NHC linaendelea kukarabati nyumba zake za kupangisha mikoa mbalimbali nchini, zikiwemo zilizopo Upanga jijini Dar es Salaam na Bukoba mkoani Kagera, ili kuboresha ubora wa makazi na huduma kwa wapangaji.

APP mpya kuleta huduma karibu na wateja

Katika hatua nyingine, Hamad amebainisha shirika hilo kuwa katika maandalizi ya kuzindua programu ya simu ya National Housing App, inayotarajiwa kurahisisha upatikanaji wa taarifa kuhusu miradi na huduma za NHC.

Kwa mujibu wa Hamad, programu hiyo itamwezesha mteja kupata taarifa za nyumba, kuanza taratibu za ununuzi na kuwasilisha changamoto bila kulazimika kufika ofisini au eneo la mradi.

“Wateja wanaohitaji mikopo wataweza kuunganishwa na benki washirika wanazochagua ili kufanikisha uwezekano wa kupata fedha za kununulia nyumba.

Mkurugenzi Hamad anasema programu hiyo pia inatarajiwa kusaidia wapangaji kuwasilisha taarifa za changamoto, huku misimbo ya QR na utambulisho wa kidijitali vikisaidia kufuatilia watumishi wanaoshughulikia maombi na muda unaotumika kuyatatua.

Teknolojia hiyo inalenga kuongeza uwajibikaji na kupunguza muda wa kupata huduma. Hata hivyo, mafanikio yake yatategemea utekelezaji mzuri na utatuzi wa changamoto za wateja kwa wakati.

Safari ya umiliki wa nyumba

Kutoka Kawe 711 hadi Kariakoo na miradi ya mikoani, NHC inaunganisha ujenzi wa makazi, uwekezaji wa majengo, mikopo kutoka taasisi za fedha na benki, pia teknolojia katika mkakati mmoja wa kuboresha huduma.

Kwa wananchi, mafanikio ya juhudi hizo yatategemea upatikanaji wa nyumba zinazolingana na uwezo wao wa kifedha, masharti ya mikopo yanayoeleweka na huduma bora baada ya ununuzi.

Katika kuunga mkono Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, NHC inalenga kupanua fursa za umiliki wa nyumba na kuboresha mazingira ya makazi na biashara nchini. Changamoto iliyopo ni kuhakikisha kuwa uwekezaji na mifumo mipya inatafsiriwa kuwa huduma zinazofikika kwa wananchi wengi zaidi.

 

Post a Comment

Mpya zaidi Nzee zaidi