-Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
Mkururugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Hamad
Abdallah amesema shirika hilo linaendelea kutimiza ndoto ya Rais Samia Suluhu
Hassan ya kuwawezesha Watanzania wengi zaidi kumiliki nyumba bora kupitia
miradi yake mbalimbali inayoitekeleza nchini.
Mkuugenzi Mkuu wa NHC, Hamad abdallah akizungumza katika kilele cha Wiki ya Huduma kwa Mteja, Oktoba 16,2026 Dar es Salaam.
Akizungumza katika kilele cha Wiki ya Huduma kwa Wateja katika
eneo ulipo Mradi wa Kawe 711 unaotekelezwa na shirika hilo Oktoba 16,2026,
Hamad amesema NHC inatekeleza ndoto hiyo ikishirikiana na benki mbalimbali
zaidi ya 20,ambazo wameingia makubaliano kuwawezesha wananchi kununua nyumba kupitia
benki hizo baada ya kulipia asilimia 10 ya bei huku nyumba husika ikiwa ndiyo
dhamana.
“Tunataka kutimiza
ndoto ya Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ya kuwawezesha Watanzania
wengi zaidi kumiliki nyumba bora. Hili linawezekana kupitia ushirikiano imara
kati ya NHC na benki zinazotoa mikopo ya nyumba kwa Watanzania waliopo nchini
na wanaoishi nje ya nchi (Diaspora).”
Amefafanua kuwa kupitia mpango huo, NHC inawawezesh
watanzania kumiliki nyumba bora na za kisasa bila kuumiza vichwa kwa kutafuta
dhamana, huku wakiongezewa mud awa kulipa mikopo hiyo na benki, kutoka miaka
mitatu hadi mitano ya awali na kufikia kati ya miaka 20 na 25.
Hamadi amesema NHC inaendelea kuimarisha ushirikiano na taasisi za fedha ili
kurahisisha upatikanaji wa mikopo ya nyumba, hivyo kuwawezesha wananchi wengi
zaidi kutimiza ndoto ya kuwa na makazi yao wenyewe na kwamba ushirikiano huo ni
muhimu katika kuhakikisha wananchi hawazuiliwi na changamoto ya kutokuwa na
fedha zote za kununua nyumba kwa wakati mmoja.
“Tunataka Watanzania wengi zaidi wawe wamiliki wa nyumba, na mabenki ni
washirika muhimu katika kufanikisha azma hiyo,” amesisitiza Hamad.
Mkurugenzi huyo amewahimiza wananchi kuendelea kujitokeza
kwa wingi na kununua nyumba katika mradi huo wa 711, akieleza kuwa ni mradi wa kisasa
zaidi ambapo kila mwenye nyumba, atamiliki pia maegesho ya gari lake, huku
wageni pia wakitengewa maegesho yao.
“Huu ni mradi wa kwanza wa nyumba za makazi wenye viwanja
vya michezo na mabwawa ya kuogelea yakiwa ghorofani, hakuna mwingine. Lakini
pia utakuwa na eneo litakalowawezesha wamiliki wa nyumba hizo kupata huduma za
kijamii ikiwamo maduka na za kibenki,” amesema.
Amesema katika eneo hilo kuna viwanja vya mchezo wa Mpira wa
Kikapu na mpira wa meza hivyo kuwa chanzo kizuri kwa wakazi wa eneo hilo kushiriki
katika michezo ivyo kulinda na kuimarisha afya zao na kuepuka magonjwa yanayoepukika.
Wateja kula Krismasi 711
Kuhusu kukamilika na kuhamia katika nyumba za Mradi wa Kawe
711 Hamad amesema kuwa jambo jema kwa wateja wa nyumba hizo ni kwamba, watakula
sikukuu ya Krisimasi na Mwaka Mpya wakiwa ndani ya nyumba zao mpya akieleza
kuwa kinachokamilishwa sasa ni maeneo ya huduma za kijamii zilizopo chine
kwenye eneo hilo.
Chapisha Maoni