Hot Posts

6/recent/ticker-posts

Wakatoliki sasa wafikia bilioni 1.4

 -Ni katika mwaka mmoja
 -Papa Francis aunda majimbo saba 

Mwandishi Wetu,daimatznews@gmail.com

Takwimu za Kanisa Katoliki duniani, zinaonyesha kuwa ya idadi ya Waamini wa kanisa hilo imeongezeka hadi bilioni 1.406 kufikia mwaka 2025. 

Baba Mtakatifu, Papa Francis akitoa baraka kwa waumini wa kanisa hilo kwenye moja ya matukio.

Kwa mujibu wa habari hizo kupitia mtandao rasmi wa Vatican, ongezeko hilo linaloihusu pia Tanzania, limemwezesha Kiongozi wa Kanisa hilo duniani, Papa Francis kuunda majimbo makuu mapya matatu; akiunda majimbo mapya saba, likiwemo Jimbo Katoliki la Bagamoyo hapa nchini.
Habari hizo zimeeleza kuwa Papa Francis ameunda majimbo hayo mapya lengo kuu likiwa kusogeza huduma za kichungaji kwa watu wa Mungu mahali walipo.
“Takwimu hizo zilizotolewa na Idara ya Takwimu za Kanisa Katoliki Ulimwenguni “Annuarium Statisticum Ecclesiae” zinaonesha kwamba, idadi ya Waamini wa Kanisa Katoliki Ulimwenguni imeongezeka kutoka bilioni 1. 39 mwaka 2024 hadi kufikia bilioni 1.406 katika mwaka 2025,” zimeeleza habari hizo. 
Ikumbukwe kwamba, idadi ya Waumini wa Kanisa Katoliki Ulimwenguni kati ya mwaka 2022 hadi mwaka 2023 ilikuwa ni bilioni 1.39. 
Bara la Afrika limetajwa kuwa na asilimia 20 ya Waumini wote wa Kanisa Katoliki duniani na kwamba, huku nchi zinazoongoza kwa idadi kubwa ya Waumini wa kanisa hilo barani humo ikiwa ni DRC Congo, yenye Wakatoliki milioni 55, Nigeria waamini milioni 35 huku nchi nyingine zenye idadi kubwa ya Waumini wa Kanisa Katoliki Afrika Mashariki zikitajwa kuwa ni Tanzania, Uganda na Kenya.

Mwadhama Protas Kardinali Rugambwa, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki laTabora

Taarifa hiyo imeeleza kuwa ukuaji wa idadi ya Waumini wa Kanisa Katoliki Barani Afrika ni sawa na asilimia 3.31, idadi ya Maaskofu ikiongezeka kwa asilimia 1.4 kutoka Maaskofu 5, 353 hadi kufikia Maaskofu 5, 430. 
“Idadi ya Maaskofu Barani Afrika imeongezeka kutoka asilimia 13.8 hadi asilimia 14.2 ya mwaka 2023,” zimeeleza habari hizo. 
Moja ya maaskofu waliongezeka ni Askofu Stephano Msomba,(Pichani chini), aliyeteuliwa na Papa Francis kuongoza Jimbo Katoliki jipya la Bagamoyo. 

Kanisa Katoliki Ulimwenguni lina majimbo makuu 3, 041 na majimbo 406, 996,huku idadi ya Mapadre barani ikitajwa kuongozeka kwa asilimia 2.7, ambapo pia idadi ya Mashemasi wa kudumu katika kipindi cha Mwaka 2023 imeongezeka kutoka 50,150 hadi kufikia Mashemasi 51, 433. 
Hata hivyo, takwimu zinaonesha kwamba, kuna idadi ndogo ya Mashemasi wa kudumu Barani Afrika.
Idadi ya watawa wa kiume na wa kike imetajwa kuendelea kupungua, ingawa barani Afrika inaendelea kuongezeka.
Barani Ulaya idadi ya watawa imepungua katika kipindi cha mwaka 2023,huku barani Afrika kukiwa na ongezeko la asilimia 2.2. 
Idadi ya waseminari walioko Seminari Kuu imetajwa kupungua kwa asilimia 1.8, kutoka  Waseminari 108,481 hadi kufikia Waseminari 106, 495, lakini barani Afrika idadi ya Waseminari ikiongezeka kwa asilimia 1.1 kutoka Waseminari 34, 541 hadi kufikia Waseminari 34, 924.

Chapisha Maoni

0 Maoni