TRC YAIPA 'BINGO' SEKTA BINAFSI MRADI TRENI ZA ABIRIA DAR


Shirika la Reli Tanzania (TRC) limeipa 'Bingo'(nafasi kubwa) sekta binafsi nchini, ambapo Mkurugenzi wa shirika hilo, Mhandisi Machibya Shiwa ameeleza kuwa sekta hiyo ndiyo itakayotekeleza mradi wa Reli za Mijini, jijini Dar es Salaam ulio katika hatua za matayarisho.

Katika maandalizi ya mradi huo tayari kikao cha kwanza kimefanyika Septemba 17, 2026 kati ya TRC na mshauri mwelezi kampuni ya SYSTRA ya nchini Ufaransa, itakayofanya upembuzi yakinifu wa mradi wa reli za mjini (Monorail), unaolenga kuboresha usafiri wa umma na kupunguza msongamano wa magari katika jiji hilo la biashara.

"Sekta binafsi imepewa takribani asilimia 70 katika utekelezaji wa dira 2025, hivyo hii ni fursa kwa sekta hiyo kutekeleza mradi huu," amesema Mhandisi Shiwa alipozungumza na waandishi wa habari baada ya wasilisho la Kampuni ya SYSTRA kuhusu hatua hiyo na kuongeza;

“Natoa wito kwa sekta binafsi kujitokeza kuchangamkia fursa hiyo kufutia nafasi kubwa waliyonayo ya kuongeza uwekezaji nchini, ikizingatiwa kuwa Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi ya kisheria, kisera na kitaasisi ili kuvutia uwekezaji wa ndani na nje ya nchi.’’

Mhandisi Shiwa amesema mradi huo wa ujenzi wa reli moja,  unalenga kukabiliana na ongezeko la mahitaji ya usafiri linalotokana na ukuaji wa Jiji la Dar es Salaam, ambapo kufikia mwaka 2030 idadi ya watu inatrajiwa kufikia milioni kumi (10) jijini humo.

Mkurugenzi huyo wa TRC amesema; “Kuanza kwa mchakato huu ni hatua muhimu katika maandalizi ya kujenga mfumo wa kisasa wa usafiri wa mijini."

Amefafanua kuwa upembuzi yakinifu utatoa msingi wa kitaalamu wa kubaini namna bora ya kutekeleza mradi  huo kwa kuzingatia mahitaji ya wananchi na ukuaji wa jiji la Dar es Salaam.

Mhandisi Shiwa, utaongeza ukuaji wa uchumi, kuongeza ufanisi wa biashara, kufungua fursa za ajira na uwekezaji, pia kuongeza thamani ya maeneo yanayohudumiwa na reli huku ukipunguza hasara zinazotokana na muda unaopotea katika foleni mijini.


Post a Comment

Mpya zaidi Nzee zaidi