-YAIPA LOVIOT VIFAA VYA OFISI
Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
Katika kutambua umuhimu wa kuwasaidia watu wenye uono hafifu, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limetoa vifaa na samani za ofisi kwa asasi ya Low Vision Organization of Tanzania (LOVIOT) lengo likiwa kusaidia kuimarisha uwezo wa taasisi hiyo kuwahudumia watu wenye uono hafifu nchini.
Msaada huo umekabidhiwa, Septemba 10, 2026, jijini Dar es Salaam, ikiwa sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Huduma kwa Jamii ya NHC, inayolenga kugusa maisha ya wananchi na kuunga mkono makundi yenye mahitaji maalumu nchini.
NHC imekabidhi meza na viti vya ofisi, viti vya wageni, kompyuta pamoja na printa, vifaa ambavyo vitasaidia kuboresha mazingira ya kazi ya LOVIOT na kurahisisha shughuli zake za kila siku katika kuwafikia na kuwahudumia walengwa wake.
Akikabidhi msaada huo kwa niaba ya NHC, Afisa Uhusiano wa NHC, Yamlihery Ndullah, amesema Shirika linaamini kuwa wajibu wake hauishii katika kujenga nyumba na majengo pekee, bali pia unahusisha kushiriki katika juhudi zinazoboresha maisha ya jamii inayolihudumia.
Amesema chini ya uongozi wa Mkurugenzi Mkuu, Hamad Abdallah, NHC inaendelea kutekeleza shughuli mbalimbali za huduma kwa jamii, ikiwemo kusaidia taasisi na makundi yenye mahitaji maalumu.
“Tunafurahi kuwa sehemu ya kurejesha tabasamu kwa jamii yetu. Huu ni utaratibu ambao Shirika limekuwa likiutekeleza mara kwa mara katika kuwahudumia na kuwaunga mkono wananchi,” amesema Ndullah.
LOVIOT, nayo imeeleza kuwa msaada huo siyo tu vifaa vya ofisi, bali pia ni nyenzo zitakazosaidia taasisi hiyo kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi na kuwafikia watu wengi zaidi wenye uono hafifu.
Mwenyekiti wa LOVIOT, Mark Hamis, ameishukuru NHC pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo kwa kutambua mahitaji ya taasisi yao na kuchukua hatua ya kuwasaidia.
“Kwa upande wetu, Shirika la Nyumba la Taifa limekuwa baraka kubwa. Tunawashukuru kwa kutukumbuka na kutukumbatia, hasa kwa kutambua mahitaji yetu. Tunaomba waendelee na moyo huo huo wa kuisaidia jamii,” amesema Hamis.
Amesema msaada huo umefika katika wakati muafaka na utarahisisha shughuli za taasisi hiyo, huku ukiwapa moyo wanufaika wake kuona kuwa mahitaji yao yanatambuliwa na taasisi mbalimbali katika jamii.
Kwa NHC, hatua hiyo ni sehemu ya dhamira pana ya kuhakikisha kuwa pamoja na kutekeleza miradi ya nyumba na majengo, Shirika linaendelea kuwa sehemu ya maendeleo ya jamii kwa vitendo.
Kwa LOVIOT na watu wenye uono hafifu wanaohudumiwa na taasisi hiyo, meza, kiti, kompyuta au printa inaweza kuonekana kuwa kifaa cha kawaida cha ofisi; lakini inapowezesha huduma kufika kwa mtu anayehitaji msaada, thamani yake huwa kubwa zaidi ya kifaa chenyewe.

Chapisha Maoni