Mwandishi Maalum, Italia
Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, ameongoza ujumbe wa Tanzania kutembelea Kituo cha Kitaifa cha Usimamizi wa Uendeshaji wa Reli (National Control Room) cha Rete Ferroviaria Italiana (RFI), nchini Italia kinachosimamia uendeshaji wa mtandao wa reli nchini humo kwa wakati halisi kupitia mfumo unaounganisha vituo vya udhibiti vya kikanda, ikitajwa kufungua fursa mpya kati ya Tanzania na Italia.
Katika ziara hiyo, ujumbe ulijifunza namna kituo hicho kinavyoratibu uendeshaji wa treni za abiria na mizigo, kusimamia mtiririko wa trafiki ya reli, kuratibu matengenezo ya miundombinu na kushughulikia changamoto za kiutendaji ili kuhakikisha usalama, ufanisi na mwendelezo wa huduma.
Wakati wa ziara hiyo ujumbe wa Tanzania ulielezwa kuwa matengenezo hupangwa kwa muda mrefu na kuratibiwa kwa karibu na idara za uendeshaji, biashara na udhibiti wa trafiki, ili kupunguza athari kwa huduma na kuhakikisha matumizi bora ya miundombinu.
Ujumbe huo pia ulitembelea mradi wa miundombinu jijini Florence unaosimamiwa na FS Engineering, ambapo ulijionea matumizi ya teknolojia za kisasa katika usanifu, upangaji, usimamizi wa ujenzi na ukaguzi wa ubora wa kazi. Teknolojia zilizowasilishwa ni pamoja na Building Information Modelling (BIM), LiDAR Survey, Artificial Intelligence (AI) na Digital Control Room, zinazowezesha ukusanyaji, uchambuzi na uwasilishaji wa taarifa za mradi kwa wakati halisi.
Mifumo hiyo hufuatilia maendeleo ya kazi za wakandarasi, hutathmini ubora wa kazi, hubaini changamoto mapema, husimamia utekelezaji wa mikataba kwa kuzingatia viwango vilivyowekwa, huboresha matumizi ya rasilimali na kuwezesha maamuzi yanayotokana na taarifa sahihi na za wakati halisi, hivyo kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi wa usimamizi wa miradi.
Aidha, ujumbe ulifanya majadiliano ya kiufundi na wataalamu wa FS Engineering kuhusu mbinu bora za usimamizi wa miradi na namna teknolojia hizo zinavyoweza kutumika kuimarisha usimamizi wa miradi ya reli nchini Tanzania.
Kupitia Hati ya Makubaliano iliyosainiwa kati ya Tanzania na Italia, TRC itanufaika na uhamishaji wa teknolojia, kubadilishana uzoefu, kujengewa uwezo wa wataalamu na kuimarisha mifumo ya usimamizi wa miradi ya reli.
Ushirikiano huo pia unaenda sanjari na juhudi za TRC za kuimarisha huduma za Engineering Consultancy, huku ukiunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita za kuimarisha sekta ya reli kupitia matumizi ya teknolojia za kisasa, kuongeza uwezo wa wataalamu, kuboresha usimamizi wa miradi ya kimkakati na kuhakikisha uendelevu wa miundombinu ya reli kwa manufaa ya Taifa.



Chapisha Maoni