Hussein Ndubikile, daimatznews@gmail.com
Mkurugenzi wa Kampuni ya Zan Securities Limited, Raphael Masumbuko, amesema Mfuko wa Timiza umeendelea kukua kwa kasi, kutoka mtaji wa awali wa Sh bilioni 10.3 ulipoanzishwa mwaka 2012 hadi kufikia zaidi ya Sh bilioni 50.
![]() |
| Mkurugenzi wa Kampuni ya Zan Securities Limited, Raphael Masumbuko, akizungumza na wanahabari (hawapo pichani) |
Aidha, amebainisha kuwa kampuni hiyo imezindua mifuko miwili ikiwemo ZanTimiza ETF Fund of Funds na Timiza Fund Plus na kwamba wananchi wataweza kujiunga kwa gharama nafuu kwa vipande.
Ameyasema hayo Agosti 17, 2026 jijini humo katika uzinduzi wa mifuko miwili mipya ya uwekezaji ya Zan Securities jijini Dar es Salaam, Masumbuko amesema ukuaji huo unaonyesha kuongezeka kwa ushiriki wa Watanzania katika uwekezaji kupitia masoko ya mitaji.
Amesema mfuko huo pia umeendelea kuwa na wawekezaji zaidi ya 13,000 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, huku ukitoa faida ya wastani wa asilimia 15 kwa mwaka 2025.
Ameeleza kuwa mafanikio hayo yameipa Zan Securities ujasiri wa kuzindua ZanTimiza ETF Fund of Funds na Timiza Fund Plus, yenye malengo tofauti kwa wawekezaji.
Kwa upande wake, Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar, Dk. Juma Malik Akil ameipongeza kampuni hiyo kwa kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayozinzgatia ukuaji wa uchumi wa wananchi wake kupitia uwekezaji.
Nae, Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini, Clayton Revocatus Chipando 'Baba Levo' amesema kuwa atakuwa balozi wa kampuni kwa kuhakikisha elimu ya uwekezaji katika mifuko hiyo inawafikia wananchi wake.
Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Peter Nalitolela amesema kuwa uzinduzi wa mifuko hiyo imekuja wakati mwafaka ambapo Serikali inaendelea na jitihada za kuwakwamua wananchi kupitia uwekezaji wa mifuko ya masoko na mitaji.
Gladness Deogratius kutoka Benki ya NMB amefafanua kuwa benki hiyo imepewa jukumu la kuisimamia mifuko hiyo na kwamba watahakikisha wanasimamia kikamilifu ili wananchi wanunue vipande vya uwekezaji.

Chapisha Maoni