KARDINALI PENGO-MWAMBA WA IMANI, MAADILI ULIOLALA
-Atajwa shuhuda wa majadiliano kidini, kisiasa na kitamaduni
Mwamba wa imani na maadili umelala. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Yuda Thadei Ruwa’ichi kutangaza kifo cha mtangulizi wake, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, akieleza kuwa ametwaliwa na Mungu usiku wa saa 4, Februari 19, mwaka 2026.
Kwa mujibu wa Askofu
Ruwai’chi, Kardinali Pengo ametwaliwa wakati akipatiwa matibabu katika Taasisi
ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dar es Salaam.
“Ninayo masikitiko
makubwa kuwatangazieni kwamba, leo 19/02/2026, saa 04.00 usiku huu, mpendwa baba
yetu Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu la Dar
es Salaam, ameitwa nyumbani kwa Baba wa Milele, akiwa katika Taaisisi ya Moyo
ya Jakaya Kikwete (JKCI), jijini Dar es Salaam,” amesema Askofu Ruwa’ichi
katika taarifa yake.
Taarifa hiyo imetolewa Kwenda kwa Mwadhama Kardinali Protas Rugambwa, Maaskofu wakuu wote, maaskofu, mapadri, watawa na waamini wote walei ikifafanua kwamba; “Taarifa za mazishi zitawajia baada ya mipango kukamilika.”
Hata hivyo, enzi za uhai wake, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, amewahi kueleza kuwa; Kaburi lake lipo Pugu, na ndipo mahali alipokuwa akipenda kwenda kusali, akaomba utashi wake huo uheshimiwe.
Kardinali Pengo ni nani?
Pengine unaweza kujiuliza anayeelezewa hapa ni nani, lakini majibu yapo wazi kwamba;
Mwadhama Polycarp Pengo ni kardinali wa pili kutoka Tanzania, ambaye aliteuliwa mara baada ya kifo cha mtangulizi wake, Mwadhama Laurean Rugambwa, kardinali wa kwanza kutoka kusini Jangwa la Sahara.
Historia inataja kuwa
Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo alizaliwa katika eneo la Mwazye (Wilaya ya Kalambo, Mkoa wa Rukwa, Agosti
5, mwaka 1944.
Kardinali Pengo
alipewa Daraja Takatifu ya Upadri Juni 20, mwaka 1971, mikononi mwa Hayati
Askofu Charles Msakila wa Jimbo Katoliki la Sumbawanga, aliyeishi kati ya mwaka
1958 na 1994, siku ambayo mwenyewe Pengo,
alieelezea kwamba kamwe hataweza kuisahau kwani tangu mwanzo kabisa alimwambia
Mama yake kwamba, angetamani kuwa Padre na shuhuda wa imani kama alivyokuwa
Mtakatifu Polycarp.
Akasoma teolojia ya maadili huko Roma, Italia, akapata Shahada ya Udaktari mwaka 1977, kisha kufundisha somo hilo kwa muda mfupi kwenye Seminari Kuu ya Kipalapala (Mkoani Tabora), baadae akachaguliwa kuwa Gombera wa Seminari Kuu ya Segerea Jimbo Kuu la Dar es Salaam hadi mwaka 1983.
Katika eneo hilo la
maadili Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo anatajwa kubobea ambapo hakuishia
katika malezi ya vijana pekee, bali pia kanisa kwa ujumla na taifa kutokana na
misimamo yake.
Wakati Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo akitimiza miaka 50 ya upadri Juni mwaka 2021, Askofu Mkuu Gervas Nyaisonga, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, (TEC), alipohijiwa na Radio Vatican alimwelezea Kardinali Pengo akisema;
“Katika maisha na
utume wake kama Padre na Askofu kuanzia: Nachingwea na Tunduru-Masasi,
Kardinali Pengo ameweza kusimama imara bila kuteteleka katika masuala ya imani,
maadili na utu wema. Na kwa njia ya msimamo wake, akaweza kuiepusha Tanzania
katika dhoruba na mawimbi makali yaliyokuwa yanaisonga nchi.
Amekuwa ni chombo na
shuhuda wa majadiliano ya kiekumene, kidini, kisiasa na kitamaduni.”
Askofu Mkuu Nyaisonga amefafanua; “Mambo hayo yalisaidia kujenga na kuimarisha maridhiano, umoja na mshikamano wa kitaifa; daima ni kiongozi aliyesimamia: ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wengi! Ni kiongozi aliyebahatika kuwa na kipaji cha unyenyekevu na usikivu, kiasi kwamba, alikuwa tayari kupokea watu, kuwasikiliza, kung’amua pamoja na kuwapatia ushauri.”
Amesema kwa wale ambao wametekeleza kikamilifu ushauri wake, wamefanikiwa kupata suluhu ya changamoto zilizokuwa zinawaandama.Kardinali Polycarp Pengo ni kiongozi aliyebahatika kuwa na ushauri chanya katika changamoto za maisha.
Katika maisha
na utume wake, hasa kwa Jimbo kuu la Dar es Salaam, mafanikio makubwa
yameonekana chini ya uongozi wake. Idadi kubwa ya Maaskofu walioko nchini
Tanzania, wengi wao wamepitia katika mikono mwake, kama wanafunzi na hata
akawaweka wakfu kuwa Maaskofu, ili waweze kufundisha, kuongoza na
kuwatakatifuza watu wa Mungu.
Amemtaja Kardinali
Pengo kwamba amekuwa ni kiongozi aliyewathamini sana vijana, akawawekeza amana,
utajiri, uzoefu na mang’amuzi yake katika malezi.
“Leo hii, Jimbo kuu la Dar es Salaam linaendelea kuwa na idadi kubwa ya miito mitakatifu si tu kwa watawa na watu wa ndoa, bali hata kwa wingi wa Mapadre. Ameimarisha malezi, makuzi na majiundo endelevu na fungamani kwa Mapadre wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam kama kielelezo cha ukomavu wa imani na mwanzo wa mchakato wa kujitegemea kwa rasimali watu, bila kusahau pia rasimali fedha,” amesema Askofu Nyaisonga pichani chini.
Ameeleza Jimbo Kuu la
Dar es Salaam ni kati ya majimbo yaliyo na mwamko mkubwa katika kulitegemeza
Jimbo kwa rasilimali fedha na vitu.
“Hizi ni juhudi za
Kardinali Polycarp Pengo katika utume wake,” amesema.
Askofu Mkuu Nyaisonga
aliendelea kufafanua kwamba, Kardinali Pengo ni mtu mwenye msimamo na malengo
katika maisha na amejitahidi kuhakikisha kwamba, anatekeleza malengo yake kwa
wakati.
“Kabla ya kung’atuka
kutoka madarakani, alijipangia kwamba, Jimbo kuu la Dar es Salaam liwe
limefikia Parokia 100, lakini hadi kufikia tarehe 15 Agosti 2019, Parokia za
Jimbo kuu la Dar es Salaam zimeongezeka zaidi ya namba aliyokuwa amekusudia.
Nia ilikuwa ni njema, kuhakikisha kwamba, waamini wa Jimbo kuu la Dar es Salaam
wanapata huduma ya kichungaji kwa karibu zaidi,” Rais huyo wa TEC amesema.
Pengo aliteuliwa kuwa
Askofu wa Jimbo Katoliki la Nachingwea Novemba
11, mwaka 1983, akapewa daraja hilo takatifu hiyo na Papa Yohane Paulo II Januari
6, mwaka 1984, lakini, Oktoba 17, mwaka 1986 alihamishiwa jimbo jipya Katoliki la Tunduru-Masasi.
Januari 22 mwaka 1990 aliteuliwa kuwa Askofu Mwandamizi wa Jimbo Kuu la Dar-es-Salaam na mwaka 1992, Kardinali Laurean Rugambwa alipostaafu, Pengo akawa Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu hilo.
Historia ya Kardinali Pengo katika utume ndani ya Kanisa Katoliki iliendelea kupaa baada ya Papa Yohane Paulo II kumteua kuwa kardinali Februari 21, mwaka 1998, akikabidhiwa parokia ya Nostra Signora de La Salette mjini Roma.Pamoja na majukumu mbalimbali katika idara za Papa, tangu mwaka 2007 hadi 2013 Kardinali Pengo alikuwa mwenyekiti wa Umoja wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki ya Afrika na Madagaska.










Maoni
Chapisha Maoni