-Waziri ashuhudia uwekaji saini makubaliano
Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com
Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa (Mb), amefanya ziara rasmi nchini Italia ikilenga kuimarisha ushirikiano wa kiufundi kati ya Tanzania na Italia.
Ziara hiyo inafuatia mwaliko wa Waziri wa Miundombinu na Uchukuzi wa Italia ampapo pia pande hizo zilishuhudia utiaji saini wa Hati ya Makubaliano (MoU) kati ya Shirika la Reli Tanzania (TRC), FS Engineering S.p.A na ITS Engineering S.r.l na kujionea matumizi ya teknolojia za kisasa katika usimamizi wa miundombinu ya reli, pamoja na kutembelea miradi ya kimkakati inayosimamiwa na FS Engineering.
Prof. Mbarawa pamoja na Naibu Waziri wa Miundombinu na Uchukuzi wa Italia, Edoardo Rixi, aliyemwakilisha Waziri wa Miundombinu na Uchukuzi wa Italia, walishuhudia pia utiaji saini wa Hati ya Makubaliano iliyosainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Mhandisi Machibya Shiwa, Dario Lo Bosco kwa niaba ya FS Engineering S.p.A. na Michele Titton kwa niaba ya ITS Engineering S.r.l.
FS Engineering ni kampuni tanzu ya Ferrovie dello Stato Italiane (FS Group), Shirika la Kitaifa la Reli la Italia, linalotoa huduma za ushauri wa kihandisi, usanifu, usimamizi wa miradi na ujenzi wa miundombinu ya usafiri.
Kwa kushirikiana na ITS Engineering, taasisi hizo zitabadilishana utaalamu, kujenga uwezo wa wataalamu wa TRC, kuimarisha matumizi ya teknolojia za kisasa katika kubuni, kupanga, kusimamia na kufuatilia miradi ya reli, pamoja na kuendeleza suluhisho bunifu za kuboresha ufanisi, ushindani na uendelevu wa sekta ya reli.
Ujumbe wa Tanzania pia ulipata fursa ya kujifunza matumizi ya teknolojia kama LiDAR Survey, Building Information Modelling (BIM), Artificial Intelligence (AI) na Digital Control Room, zinazowezesha ukusanyaji na uchambuzi wa taarifa za miradi kwa wakati halisi, ufuatiliaji wa maendeleo ya kazi, udhibiti wa ubora, usimamizi wa mikataba na kufanya maamuzi sahihi yanayoongeza ufanisi wa utekelezaji wa miradi.
Ushirikiano huu unafungua fursa za uhamishaji wa teknolojia, kujengewa uwezo wa wataalamu wa TRC na kuimarisha huduma za ushauri wa kihandisi kupitia kitengo cha Engineering Consultancy, hatua inayounga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuimarisha sekta ya reli kwa matumizi ya teknolojia za kisasa, usimamizi bora wa miradi na maendeleo endelevu ya miundombinu.




Chapisha Maoni