'TUMEPATA UKWELI TUMEBADILI MTAZAMO KUHUSU NHC'

Mwandishi Wetu

Wabanchi waliotembelea Banda la Shirika la Nyumba la Taifa(NHC) katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba 2026), wamesema wamebadili mtazamo wao kuhusu NHC na huduma inazozitoa kuhusu makazi bora nchini, baada ya elimu waliyopewa katika banda hilo. 

Wakizungumza ndani ya Banda la NHC katika viwanja hivyo vilivyopo Barabara ya Kilwa Dar es Salaam, kwa nyakati tofauti wamesema; "Tulikuwa tunasikia mengi kuhusu NHC, lakini leo tumepata ukweli."

 Wameeleza kuwa walipata fursa ya kuzungumza na wataalamu wa NHC na kujifunza kuhusu miradi ya kisasa ya makazi inayotekelezwa nchini, pamoja na kufahamishwa taratibu za kupanga na kununua nyumba zinazomilikiwa na shirika hilo.

Mmoja wa wananchi hao, Erasto Golan ame
sema alikuwa na dhana kuwa nyumba za NHC ni kwa ajili ya watu wachache wenye uwezo mkubwa wa kifedha, lakini baada ya kupata maelezo kutoka kwa wataalamu wa Shirika, amebaini kwamba kila Mtanzania anayekidhi vigezo ana nafasi ya kupata huduma kwa kufuata taratibu zilizowekwa.

Naye Elias George amesema; "Leo tumepata majibu ya maswali tuliyokuwa nayo kwa muda mrefu. Sasa naelewa kuwa mfumo wa NHC uko wazi na unatoa fursa kwa Watanzania wote bila ubaguzi,"

Kwa upande wake, Alex Chonya amesema maelezo aliyopata kutoka kwa watumishi wa NHC ndani ya banda lao la maonyesho, yamemjengea imani zaidi kuhusu huduma za NHC na kwamba yuko tayari kuwahamasisha wengine kutembelea banda hilo ili wajionee fursa zilizopo badala ya kutegemea taarifa zisizo rasmi.

Maonesho ya Sabasaba yanaendelea kuwa jukwaa muhimu kwa wananchi kupata taarifa sahihi kuhusu huduma za NHC, kuzungumza na wataalamu wake na kujionea fursa mbalimbali za makazi na uwekezaji zinazotolewa na Shirika.

Katika Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (Sabasaba 2026), Banda la NHC lipo Mtaa wa Biashara, karibu na Banda la TCB, ambapo watendaji wake wananendelea kutoa elimu, ushauri wa kitaalamu na taarifa za miradi mbalimbali ya makazi na biashara inayotekelezwa nchini 

Post a Comment

Mpya zaidi Nzee zaidi