M-PESA SASA MIAKA 18; SHUJAA ANAYEWAKOMBOA WATANZANIA

- Vodacom Tanzania yaimarisha ukuaji M-Pesa sasa yawekeza Dola milioni 28

Exuperius Kachenje, daimatznews@gmail.com

Kwa kawaida mtoto anapotimiza umri wa miaka 18 hutazamwa kwa matumaini mapya, makubwa zaidi ya kuivusha familia au jamii husika kutoka ilipokuwa awali kwenda juu zaidi katika kufanikiwa kimaendeleo.

Hali hiyo huwezi kuitenganisha, bali kuifananisha na huduma ya M-Pesa, inayotolewa na Kampuni ya Vodacom Tanzania, ambayo inatimiza miaka 18 ya huduma zake nchini, Aprili hii 2026, ikiwa na nguvu zaidi na nafasi kubwa zaidi ya kuchagiza maendeleo ya Watanzania, wanaotumia huduma ya M-Pesa kupitisha miamala ya fedha kwa madhumuni mbalimbali.

Hakika katika miaka 18 ya M-Pesa kuhudumia Watanzania, Vodacom Tanzania inaonesha ukomavu wake, ambapo sasa imeingia hatua mpya kwa kufanya uwekezaji mkubwa wa Dola za Marekani milioni 28 takriban Sh75.6 bilioni.

Uwekezaji huo unalenga kuimarisha zaidi jukwaa hilo la kidijitali na kuhakikisha linaendana na kasi ya ukuaji wa uchumi wa kidijitali nchini.

Mtendaji Mkuu wa Vodacom Tanzania, Philip Besiimire, (pichani chini), anasisitiza dhamira ya kampuni hiyo akieleza kuwa ni kuendelea kuwahudumia Watanzania kwa viwango vya juu zaidi.

“Baada ya miaka 18 ya M-Pesa, tunaangalia mbele kwa kuhakikisha jukwaa hili linaendelea kuwa salama, imara na lenye uwezo wa kuhimili mahitaji ya wateja ya kesho," anasema Besiimire.

Anaongeza: "Uwekezaji huu ni hatua ya kimkakati, kuhakikisha wateja wetu wanaendelea kupata huduma bora inayokua pamoja nao.”

Anasema Vodacom pia imefanya maandalizi ya uhamisho wa kwenda katika mfumo mpya kwa umakini mkubwa, yakihusisha majaribio ya kina ya mifumo na watumiaji, ili kuhakikisha mabadiliko yanafanyika bila kuathiri huduma.

"Taarifa zote za wateja, ikiwemo salio na historia ya miamala, zitaendelea kubaki salama," anasema Besimire.

Uwekezaji huo wa dola milioni 28 utawezesha uboreshaji wa jukwaa la M-Pesa kutoka mfumo wa zamani wa G2 kwenda katika usanifu wa kisasa unaolenga kuongeza uwezo, uthabiti na kasi ya ubunifu.

Kwa mujibu wa Vodacom Tanzania, jukwaa hilo jipya litaongeza uwezo wa kushughulikia maelfu ya miamala kwa sekunde, huku teknolojia ya “active-active” ikipunguza kwa kiasi kikubwa muda wa mteja kusimama akisubiri huduma n kwamba  maboresho ya usalama yataimarisha zaidi ulinzi wa taarifa za wateja.

Naye Mkurugenzi wa TEHAMA na Malipo wa Vodacom Tanzania, Athumani Mlinga, anabainisha kwamba maboresho hayo yataongeza ufanisi wa utoaji huduma akieleza:

“Mabadiliko hayo yatatuwezesha kuleta huduma na maboresho mapya kwa haraka zaidi, huku tukihakikisha uthabiti waliouzoea wateja wetu unaendelea kuwepo.”

Kwa Watanzania mamilioni wanaotegemea M-Pesa kila siku, hatua hiyo inaibua  matarajio ya huduma bora zaidi za M-Pesa, ikiwa ni pamoja na kasi ya miamala, usalama wa taarifa na upatikanaji wa bidhaa mpya za kifedha kama vile akiba, mikopo na suluhisho za biashara.

Kwa jicho la kimaendeleo, uwekezaji huo wa Vodacom Tanzania sio tu unahusu teknolojia, bali ni mchango katika kuimarisha miundombinu ya kidijitali ya taifa. 

Katika kipindi cha miaka 18, tangu ilipozinduliwa nchini Aprili mwaka 2008, huduma ya M-Pesa imejidhihirisha kuwa muhimu kwa umma, ikiwezesha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa mamilioni ya Watanzania kupitia simu zao za mkononi.

Kuimarishwa kwa jukwaa hilo kunamaanisha kuimarishwa pia kwa uchumi mzima, kuanzia kwa wafanyabiashara wadogo vijijini hadi kampuni kubwa mijini, ikiwa pia ni ushahidi wa namna Vodacom Tanzania ilivyokomaa na kuendelea kujipanga kwa mustakabali, ikihakikisha kuwa M-Pesa inaendelea kuwa injini ya maendeleo katika enzi za sasa za uchumi wa kidijitali.

Hayo yanafanyika huku miamala ya fedha kwa njia ya simu ikitajwa kuwa zaidi ya bilioni sita kwa mwaka huku idadi ya watu milioni 71 wakiishi maisha yanayotegemea mifumo ya kidijitali.

Uwekezaji huo mpya wa miundombinu unaashiria dhamira ya Vodacom kuendelea kuwa nguzo muhimu katika maisha ya kifedha ya Watanzania.

Ikumbukwe kuwa safari ya M-Pesa nchini, ilianza karibu miongo miwili iliyopita, wakati ambapo kutuma fedha kwa simu kulionekana kama jambo la ajabu. 

Wakati huo, mfumo wa kifedha ulitegemea zaidi fedha taslimu, huku njia mbadala ikiwa ni kununua muda wa maongezi na kuutuma kwa ndugu ili ubadilishwe kuwa fedha taslimu, mbinu ambayo kwa wakati huo ilionekana bunifu ingawa haikuwa na  na uhakika.

Leo, Aprili Mosi 2026, simulizi hiyo imebadilika kabisa huku Tanzania ikiwa imejijengea moja ya mifumo imara zaidi ya fedha kwa njia ya simu duniani. 

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), akaunti hai za fedha kwa simu ziliongezeka kwa asilimia 116 kati ya mwaka 2021 na 2025, kutoka milioni 35.3 hadi milioni 76.5.

Katika kipindi hicho, miamala ya kila mwaka ilipanda kutoka bilioni 3.75 hadi bilioni 6.31, huku kufikia mwisho wa mwaka 2025 karibu robo tatu ya laini zote za simu zikiwa zimeunganishwa na huduma za fedha kwa simu. Hizo si takwimu za kawaida, bali unaweza kusema zinaakisi mfumo mkuu unaoendesha uchumi wa taifa.

Ni katika mazingira hayo ambapo Vodacom Tanzania, ikiwa na takribani asilimia 41.2 ya soko la fedha kwa simu, inaonesha ukomavu wake kwa kuwekeza katika mustakabali wa huduma zake. 

Uchumi wa Tanzania unaendelea kuimarika, ukitarajiwa kukua kwa asilimia 6.3 mwaka 2026, kulingana na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF). 

Wakati huo huo, matumizi ya simu janja yamefikia zaidi ya asilimia 41, huku mtandao wa 5G ukifikia asilimia 30 ya wananchi na idadi ya laini za simu ikifikia milioni 106.9, viashiria vinavyoonesha wazi kuwa huduma za kidijitali zimekuwa sehemu ya maisha ya kila siku.

Kwa mujibu wa ripoti ya GeoPoll ya mwaka 2025, asilimia 94 ya Watanzania wanatumia huduma za fedha kwa simu, wengi wao wakizitumia kwa kutuma, kupokea na kulipa bili. Zaidi ya asilimia 60 hutumia huduma hizo kila siku, na kwa wengi hasa vijijini, M-Pesa imekuwa akaunti yao kuu ya kifedha.


Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Sanamu ya Bikira Maria yaonekana ndani ya Hifadhi ya Taifa Saadani

Kapteni Traole afuata huduma za afya nchini

Wawekezaji wa Oman watua nchini, wateta na NHC kuchochea mapinduzi sekta ya makazi