WABUNGE WA PIC WASHUHUDIA NHC ILIVYOTEKELEZA MIRADI SAMIA HOUSING, KAWE 711

-Waelezwa nyumba 560 zauzwa kabla ya kukamilika

-NHC yaokoa Sh24 bilioni kwa kukopa Sh6 bilioni badala ya Sh30 bilioni 

-Mradi wazalisha ajira 1,800, uwanja wa michezo, soko kujengwa

Mwandishi Wetu, daimatznews@gmail.com

Ukiangalia miradi ya Samia Housing Scheme Kawe na Kawe 711 inayotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa(NHC), utagundua kuwa haikuota kama uyoga, bali ni matokeo ya juhudi, nidhamu na usimamizi bora wa kazi zake, ambazo sasa zimeleta matokeo chanya.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Hamad Abdallah (aliyesimama mbele), akitoa maelezo kuhusu Mradi wa Samia Housing wa Kawe Dar es Salaam, mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji Mitaji ya Serikali(PIC), iliyofanya ziara kwenye miradi ya NHC Machi 25,2026.

Bila shaka, hali hiyo imempa nguvu na msukumo Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Hamad Abdallah, kuieleza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji Mitaji ya Serikali (PIC) kuwa jumla ya nyumba 560 zilizojengwa katika Mradi wa Samia Housing Scheme, Kawe, zimeuzwa zote kabla hata ya kukamilika kwa ujenzi wake.

Hatua hiyo imedhihirisha mafanikio makubwa ya mkakati wa mauzo ya mapema ya nyumba hizo bora za kisasa kwa wananchi katika kutekeleza sera ya makazi bora kwa wananchi, lakini pia imeimarisha uwezo wa NHC kujiendesha kifedha bila utegemezi mkubwa wa mikopo ya benki.

Akizungumza wakati wa ziara ya Kamati ya PIC iliyofanyika Machi 25, 2026, jijini Dar es Saaam, Hamad amesema nyumba hizo ni sehemu ya utekelezaji wa mpango mpana wa ujenzi wa nyumba 5,000 chini ya Mpango wa Samia Housing Scheme, unaoendelea maeneo mbalimbali nchini.

Mradi wa Samia Housing, una lengo la kupanua upatikanaji wa makazi bora, ya kisasa na yenye viwango vinavyokidhi mahitaji ya Watanzania wa kipato cha kati na kawaida.

Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa mafanikio ya kuuza nyumba hizo kabla ya kukamilika kwake yamekuwa nguzo muhimu ya mafanikio ya kifedha ya mradi huo, na mfano wa ubunifu katika uendeshaji wa miradi mikubwa ya kimkakati.

“Mauzo ya nyumba hizi kabla ya kukamilika yalitusaidia kwa kiwango kikubwa sana na hatukulazimika kukopa fedha nyingi kama ilivyotakiwa awali kimahesabu. 

Tulikuwa na mpango wa kukopa Sh30 bilioni kutoka benki ili fufanikisha mradi huu, lakini kutokana na mwitikio mkubwa wa wanunuzi, tulikopa Sh6 bilioni pekee. 

Hapo tumeokoa Sh24 bilioni na imetuwezesha pia kukwepa mzigo wa riba ya benki ambayo ingetokana na mkopo mkubwa zaidi,” amesema Hamad.

Ameongeza kuwa hatua hiyo si tu imeimarisha mtiririko wa fedha wa mradi, bali pia imeongeza imani ya wawekezaji na wanunuzi katika miradi ya NHC.

Kwa mujibu wa Hamad, tayari idadi kubwa ya wanunuzi wamehamia katika nyumba hizo, huku wengine wakizitumia kama vitega uchumi kwa kuzipangisha na kujipatia mapato ya kudumu kupitia kodi, jambo linaloonesha mvuto mkubwa wa soko la nyumba za kisasa katika Jiji la Dar es Salaam.

“Hadi utakapokamilika, mradi huu wa nyumba 560 unatarajiwa kufikia thamani ya Sh49 bilioni, ambapo hadi sasa zaidi ya Sh45 bilioni tayari zimetumika katika utekelezaji wake,” ameongeza Hamad.

Akijibu swali la Mbunge Jason Rweikiza kuhusu uwepo wa huduma za kijamii ndani ya mradi huo, Hamad amesema ramani ya mradi huo imezingatia kwa kina mahitaji ya kijamii, ikiwa ni pamoja na kutenga maeneo kwa ajili ya shule za kisasa, huduma nyingine muhimu pamoja na ujenzi wa uwanja mkubwa wa michezo wenye uwezo wa kuhudumia wananchi takriban 15,000.

Mwenyekiti wa PIC, Masanja Kadogosa(Mbunge), akizungumza wakati walipofanya ziara kukagua miradi inayotekelezwa na NHC Dar es Salaam, Machi 25,2026.

Ameieleza Kamati hiyo kuwa NHC imejipanga kuboresha majengo ya zamani ya ilichokuwa Kiwanda cha Kusindika Nyama cha Tanganyika Packers ili kulinda historia ya eneo hilo kwa kuyaboresha na kuwa masoko ya kisasa (bazaar), yatakayouza bidhaa za kila siku kwa familia, hatua inayotarajiwa kukuza shughuli za kiuchumi, ajira na upatikanaji wa huduma katika eneo hilo.

Katika kuonesha umuhimu wa kuwajengea uwezo wataalamu wazawa na kukuza ujuzi wa ndani, Hamad alikatisha maelezo yake na kuwaomba wabunge amkaribisha Mhandisi wa mradi huo, Grace Msita ambaye ni kijana kutoa maelezo ya kina kuhusu utekelezaji wa mradi huo.

Akitoa maelezo zaidi ya mradi wa Samia Housing Kawe, mbele ya Kamati hiyo, Mhandisi Grace amesema nyumba hizo 560 zimejengwa katika majengo ya maghorofa 10, kuanzia Block A hadi Block J, kila jengo likiwa na ghorofa 10 kuanzia chini hadi ya juu, yakionyesha ubora wa usanifu na ujenzi wa kisasa.

Amefafanua kuwa kati ya nyumba hizo; nyumba 240 ni za vyumba vitatu (sqm 89), kila moja ikiuzwa kwa Sh192.7 milioni, na zote zimeshauzwa, zikizalisha takriban Sh46.24 bilioni.

Msimamizi wa Mradi wa Samia Housing Kawe, Mhandishi Grace Msita wa NHC(mbele), akitoa maelezo kuhusu mradi huo kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji Mitaji ya Serikali Machi 25, 2026 katika eneo la mradi.

Nyumba 160 ni za vyumba viwili (sqm 68), kila moja ikiuzwa kwa Sh147 milioni, na zote zimeshauzwa, zikizalisha takriban Sh23.52 bilioni

Nyumba 160 ni za chumba kimoja (sqm 21.2), kila moja ikiuzwa kwa Sh38.8 milioni, na zote zimeshauzwa, zikizalisha takriban Sh6.2 bilioni

Grace amesisitiza kuwa NHC yenyewe ndiyo iliyokuwa mkandarasi mkuu wa mradi huo, hatua iliyosaidia kupunguza gharama na kuongeza udhibiti wa ubora wa ujenzi.

Ameongeza kuwa vifaa vilivyotumika vilizalishwa na mitambo ya shirika hilo na kuthibitishwa ubora wake na taasisi huru zikiwamo Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pamoja na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Kwa upande wa ajira na maendeleo ya rasilimali watu, amesema mradi huo umezalisha zaidi ya ajira 1,800 kwa makundi mbalimbali, ikiwamo mafundi nondo, mafundi rangi, mafundi umeme pamoja na watoa huduma wengine kama mama lishe, hatua inayochangia moja kwa moja katika kukuza uchumi wa wananchi wa kawaida.

“Mbali na ajira, mradi huu umekuwa darasa la vitendo kwa wanafunzi wa vyuo mbalimbali vya ufundi na elimu ya juu. Tangu kuanza kwake mwaka 2023 hadi sasa, zaidi ya wanafunzi 630 kutoka taasisi kama Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) wamepata mafunzo ya vitendo hapa,” amesema Grace.

Ameongeza kuwa wahitimu 47 wa stashahada na shahada wamepata ajira, wengine za kudumu na wengine za muda, huku pia takriban watu 100 wasiokuwa na ujuzi maalum wakipewa fursa za kufanya kazi ndogo ndogo ndani ya mradi huo, jambo linaloonesha mchango mpana wa mradi huo katika ujumuishaji wa kijamii.


Akizungumzia mauzo ya nyumba katika Mradi wa Samia Kawe Housing Scheme, Ofisa Mauzo wa NHC, Daniel Kure (pichani juu),amesema nyumba zote 560 zimeuzwa na wamiliki wameshahamia.

"Wapo walioamua kuzipangisha kwa watu wengine, wamezipangisha na wameanza kufaidi kodi kwa uwekezaji walioufanya. Niendelee kuwakaribisha wanaotaka kununua nyumba za NHC, mradi huu umekalika, lakini unakuja mradi wa awamu ya pili , na miradi mingine mingi, watanzania changamkieni fursa za kumiliki nyumba bora za kisasa kupitia NHC," amesema Kure.  

Wajumbe wa Kamati ya PIC walipata fursa ya kujionea maendeleo ya mradi huo pamoja na Mradi wa Kawe 711, na kueleza kuridhishwa na kasi, ubora na uwazi wa utekelezaji wake. 

Hata hivyo, walilazimika kukatisha ziara hiyo kufuatia taarifa ya kifo cha mbunge mwenzao na aliyekuwa Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Watu wenye Ulemavu), William Lukuvi, aliyefariki Machi 25, 2026 katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dodoma alipokuwa akipatiwa matibabu.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Masanja Kadogosa, alitangaza kusitishwa kwa ziara hiyo kwa mujibu wa kanuni za Bunge ili kupisha maombolezo na taratibu nyingine rasmi za kibunge.

Katika hatua nyingine, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii nayo imewahi kukutana na NHC ambapo ilipongeza kwa utendaji wake mzuri, huku ikiitaka kuendelea kufanya tafiti za kina kuhusu matumizi ya teknolojia za kisasa zitakazosaidia kupunguza gharama za ujenzi na kuongeza upatikanaji wa nyumba nafuu kwa Watanzania wengi zaidi.

Akizungumza katika kikao hicho, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Timotheo Mzava, alisema Bunge linaiona NHC kama taasisi ya kimkakati yenye jukumu muhimu katika utekelezaji wa sera ya makazi na maendeleo ya miji nchini, na kwamba mafanikio ya miradi kama Samia Housing Scheme yanaashiria mwelekeo sahihi wa sekta ya makazi nchini.

 

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

Sanamu ya Bikira Maria yaonekana ndani ya Hifadhi ya Taifa Saadani

Kapteni Traole afuata huduma za afya nchini

Wawekezaji wa Oman watua nchini, wateta na NHC kuchochea mapinduzi sekta ya makazi