Na Hussein Ndubikile, daimatznews@gmail.com
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Prof. Godius Kahyarara, wakati akizungumza kwenye Kongamano la 11 la Wahitimu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), ambapo pia wahitimu waliofanya vizuri katika masomo yao walitunukiwa zawadi.
Amesema kuwa wanafunzi wameonyesha uwezo mkubwa wa kubuni vifaa muhimu kwa sekta ya usafirishaji na kwamba serikali itafuatilia vifaa hivyo kwa kina ili kuona jinsi vinavyoweza kusaidia maendeleo ya sekta hiyo. Alisisitiza kuwa mchango wa wanafunzi unapaswa kuanza kutumika kwa ngazi ndogo na kupanda taratibu hadi kuwa sehemu muhimu ya maendeleo ya uchumi wa nchi.
Amebainisha kuwa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) ni chuo muhimu kwa sekta ya usafirishaji, kikitoa mafunzo kwa marubani, mafundi wa ndege, na wataalamu wa fani nyingine muhimu. Alihimiza wanafunzi kutumia fursa za kiubunifu walizonazo ili kuingia sokoni na kuongeza thamani kwenye sekta.
“Wanafunzi watambue kuwa elimu wanayopata ni fursa kubwa. Ubunifu ni njia muhimu ya kujipatia nafasi katika soko la ajira na serikali iko tayari kusaidia juhudi hizi kufanikisha maendeleo,” amesema Prof. Kahyarara.
Kwa upande wake,Mkuu wa Chuo cha NIT, Dk. Prosper Lutangilo, ameishukuru serikali kwa kuwekeza katika miundombinu ya chuo hicho, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa mabweni, madarasa, na ununuzi wa vifaa kupitia mradi wa Benki ya Dunia.
Kwa upande wake, aliyekuwa Mkuu wa Chuo hicho ambaye pia ni Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Profesa Zacharia Mganilwa, ametoa wito wa kuweka mipango thabiti na utekelezaji wenye uthubutu ili kuhakikisha nchi inanufaika na maendeleo haya.
“Mipango ikifanywa kwa umakini na utekelezaji ukawa wa bidii, changamoto zilizopo zinaweza kushughulikiwa kwa mafanikio makubwa,” amesema Mganilwa.
Hatua hiyo ya Serikali inalenga kukuza talanta za wanafunzi na kuimarisha sekta ya usafirishaji, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kujenga uchumi endelevu.
0 Maoni