Hot Posts

6/recent/ticker-posts

Tanzania, Oman zasaini kuondoa utozaji kodi mara mbili

 Benny Mwaipaja, Oman

Serikali ya Tanzania na Serikali ya Kisultan ya Oman, zimetiliana saini Mkataba wa Kuondoa Utozaji Kodi ya Mapato Mara Mbili na Kuzuia Ukwepaji Kodi, ujulikanao kama Agreement for the Elimination of Double Taxation with Respect to Taxes on Income and Prevention of Tax Avoidance and Evasion.

Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba (Mb), na Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mapato ya Oman, Nasser Al-Jashmi wakionyesha hati za makubaliano kuondoa utozaji kodi mara mbili kati ya nchi hizo.

Mkataba huo umesainiwa Mjini Mascut, Oman na Waziri wa Fedha wa Tanzania, Dk. Mwigulu Nchemba (Mb), na Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mapato ya Oman, Nasser Al-Jashmi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Dk. Nchemba amesema kusainiwa kwa mkataba huo ni hatua muhimu katika jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Dk. Samia Suluhu Hassan za kufungua uchumi wa taifa kwa kuvutia uwekezaji wa kimataifa.

"Mkataba huo utawezesha wawekezaji na wafanyabiashara wanaofanya shughuli kati ya Tanzania na Oman kutozwa kodi mara moja pekee, badala ya kutozwa mara mbili kwa mapato ya aina moja, hali ambayo awali ilikuwa ikikwaza ustawi wa biashara kwa pande zote mbili." amesema Dk.Nchemba..

Kwa mujibu waziri huyo wa fedha, mkataba huo pia unalenga kuvutia mitaji mikubwa kutoka Oman kuja kuwekeza Tanzania, hasa kupitia kampuni kubwa zinazomilikiwa na familia za kifalme, sanjari na wawekezaji binafsi ambapo kupitia uwekezaji huo, Tanzania inatarajia kunufaika na ukuaji wa sekta za uzalishaji, maendeleo ya viwanda na kuongezeka ajira kwa wananchi.

"Wawekezaji wa Kitanzania sasa wataweza kuwekeza Oman bila vizuizi vya kikodi, huku wakilindwa na mkataba huo ili kuepusha kulipishwa kodi mara mbili," amesema k. Nchemba.. 

Hatua hiyo pia inatoa fursa kwa wafanyabiashara wa Tanzania kupanua shughuli zao katika masoko ya kimataifa, hasa katika ukanda wa Ghuba.

Dk. Nchemba amefafanua kwamba mkataba huo unatarajiwa kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Oman, huku Oman ikivutiwa zaidi na fursa za uwekezaji nchini Tanzania kutokana na jiografia yake ya kimkakati, vivutio vyake vya kiuchumi na mazingira bora ya uwekezaji ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.


Chapisha Maoni

0 Maoni