C-CEOs FORUM CHACHU UTEKELEZAJI DIRA2050

Mwandishi wa OTR

Arusha. Mkutano wa Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma (C-CEOs Forum) 2026, utakaowakutanisha viongozi wa mashirika ya umma zaidi ya 300, wawakilishi wa Sekta Binafsi na washiriki wengine zaidi ya 700 umetajwa kwamba utakuwa chachu ya utekelezaji Dira 2050.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Amos Makalla.

Chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina, mkutano huo utakaokuwa wa nne tangu kuanzishwa mwaka 2023, umepangwa kufanyika Septemba 28 hadi 30, 2026, ukielezewa kwamba utakuwa jukwaa muhimu la kuimarisha utendaji, tija na mchango wa mashirika hayo.

Mkutano huo unalenga kujadili namna ya kuongeza ufanisi wa taasisi hizo na kuhakikisha mipango na shughuli zao inaendana na vipaumbele vya kitaifa vilivyoainishwa katika Dira 2050.

Akizungumzia mkutano huo ofisini kwake, Septemba 25, 2026, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, CPA Amos Makalla, amesema kuwakutanisha viongozi wa Mashirika ya Umma katika jukwaa moja kunatoa fursa ya kujenga uelewa wa pamoja, kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano kwa lengo la kuongeza tija na mchango wa mashirika hayo katika maendeleo ya Taifa.

“Tunataka mkutano huu uwe na manufaa yanayoonekana pia nje ya ukumbi wa mikutano, kwa kuwafungulia fursa wafanyabiashara, watoa huduma na wananchi wa Arusha,” amesema.

Ameongeza kuwa ni muhimu Mashirika ya Umma kuhakikisha mipango na shughuli zao zinaendana na malengo ya Dira 2050, ili rasilimali na uwekezaji unaosimamiwa na Serikali uweze kuzalisha matokeo yenye thamani zaidi kwa uchumi na wananchi

Kwa mujibu wa Makalla Mkoa wa Arusha una uzoefu wa kuhudumia mikutano mikubwa ya kitaifa na kimataifa na kwamba uko tayari kuwapokea washiriki wa C-CEOs Forum 2026, huku akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha mazingira ya usalama, utulivu na ukarimu kwa wageni.

“Watakaohudumia wageni wawe wakarimu ili warudi tena,” amesema, akieleza kuwa ujio wa washiriki zaidi ya 700 utatoa fursa kwa sekta mbalimbali za kiuchumi, ikiwemo hoteli, migahawa, usafiri, utalii, biashara na huduma nyingine.

Naye, Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, amesema utekelezaji wa Dira 2050 unahitaji mabadiliko katika namna Mashirika ya Umma yanavyotazama utendaji wao, kutoka kwenye kuendesha taasisi na shughuli zake kwenda kwenye kuzalisha matokeo yanayopimika na yenye thamani kwa Taifa.

Msajili wa Hazina,Nehemia Mchechu

Mchechu amesema ufanisi wa juu unapaswa kuonekana katika uwezo wa Mashirika ya Umma kwa kutumia rasilimali na uwekezaji waliokabidhiwa kwa tija, kujenga ushindani, uimara wa kifedha na kutoa huduma zenye ubora, huku yakichangia kikamilifu katika ukuaji wa uchumi.

“Tunataka Mashirika ya Umma yenye ufanisi wa juu, shindani na imara katika kutekeleza Dira 2050,” amesema Mchechu.

Amesema thamani ya uwekezaji wa Serikali katika mashirika na kampuni zake imeongezeka kutoka Sh67.95 trilioni mwaka 2020/21 hadi Sh92.28 trilioni mwaka 2024/25, sawa na ongezeko la asilimia 35.8, hali inayoongeza umuhimu wa kuhakikisha uwekezaji huo unazalisha matokeo makubwa zaidi.

Amesema matokeo hayo hayawezi kupimwa kwa gawio pekee, bali yanapaswa kuangaliwa kwa upana kupitia tija, ubora wa huduma, ufanisi wa matumizi ya rasilimali, uimara wa kifedha, ubunifu, matumizi ya teknolojia, uwezo wa kushindana na athari ya taasisi katika uchumi.

Amesema Mashirika ya Umma yanapaswa kujenga uwezo wa kubadilika kulingana na mazingira ya uchumi, teknolojia na mahitaji ya wananchi, huku uongozi na bodi zikibeba jukumu muhimu la kuweka mwelekeo wa utendaji na uwajibikaji.

“C-CEOs Forum inalenga kuangalia kwa upana zaidi jinsi ya kubadilisha rasilimali na uwekezaji kuwa utendaji na matokeo yenye thamani zaidi,” amesema.

Mchechu amesema ongezeko la mapato yasiyo ya kodi linalotokana na mashirika na taasisi zinazochangia kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina, linaonesha pia umuhimu wa kuendelea kuboresha utendaji wa taasisi hizo. 

Mapato hayo yameongezeka kutoka Sh637.7 bilioni mwaka 2020/21 hadi Sh1.327 trilioni mwaka 2025/26, sawa na ongezeko la asilimia 108.3.

Amesema kutokana na hali hiyo mjadala kuhusu Mashirika ya Umma haupaswi kuishia kwenye suala la kiasi cha fedha kinachowasilishwa serikalini, bali kwa kuangalia thamani pana inayozalishwa na uwekezaji wa umma, ikiwemo huduma, ajira, uzalishaji, ubunifu, ushindani na mchango katika uchumi.

Msajili huyo wa Hazina amesema maeneo hayo yanahitaji uongozi wenye mwelekeo wa kimkakati, utawala bora, matumizi makubwa zaidi ya teknolojia za kidijitali na akili bandia, mifumo endelevu ya upatikanaji wa fedha, pamoja na ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi.

Amesema mashirika pia yanahitaji kuwekeza katika rasilimali watu na ujuzi wa baadaye, ili yaweze kukabiliana na mabadiliko ya kiteknolojia, kiuchumi na kimazingira, sambamba na kuzingatia masuala ya mazingira, jamii na utawala bora.

Post a Comment

Mpya zaidi Nzee zaidi